28.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

Jafo akemea watumishi kuhamishwa vituo kwa kuonewa

RAMADHAN HASSAN – DODOMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amemwagiza Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Joseph Nyamhanga, kuwarejesha mara moja katika kituo cha kazi cha Ipogoro, Manispaa ya Iringa watumishi saba ambao walihamishwa hivi karibuni.

Jafo alitoa agizo hilo jijini hapa jana wakati akifungua mkutano wa mwaka wa waganga wakuu wa mikoa na halmashauri.

Alisema kumekuwa na uonevu wa kuwahamisha vituo vya kazi baadhi ya watumishi jambo ambalo linawafanya wapoteze morali ya kazi.

“Ipogoro watu saba wamesimamishwa na wewe DMO ni mzuri. kwanini unataka kuharibu ukubwani, naagiza wale watumishi saba warudishwe na kule nimetuma timu, hatuwezi kulea mambo ya hovyo,” alisema Jafo.

Aidha, Jafo alimwagiza  Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Zainabu Chaula, kufuatilia kama mganga mkuu wa wilaya ameondolewa kazini kwa haki, kufanya makosa au kuonewa.

“Huyo mganga mkuu wa wilaya, alikuwa anafanya kazi yake kwa moyo, lakini hivi sasa ameondolewa kazini, sasa nataka ufuatilie je ameondolewa kwa makosa yake au nini kimetokea, fuatilia unipe majibu,”alisema.

Jafo alisema pamoja na jitihada za Serikali, bado kuna kazi ya kuwekeza katika miundombinu ya afya ambapo bado haiko vizuri na kusababisha watumishi kufanya kazi katika mazingira ambayo si rafiki.

Alitumia nafasi hiyo kuwapongeza watumishi wa kada ya afya kwa kuweza kufanya kazi iliyotukuka, huku akitolea mfano wa tukio la moto lililotokea mkoani Morogoro kwa jinsi walivyofanya kazi.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alisema kuna haja ya waganga wakuu wa mikoa na halmashauri kusimamia suala la lishe kwani hawafanyi vizuri.

“Suala la lishe hatufanyi vizuri, hapa kuna lishe duni na lishe iliyopitiliza, kwani asilimia 10 ya Watanzania wana lishe iliyopitiliza, jambo la kushangaza mikoa yenye chakula kingi ndiyo pia yenye ugonjwa wa udumavu, hapa tunatakiwa kutoa elimu ya afya,” alisema Dk. Ndugulile.

Aidha aliwataka waganga hao kuwa wachapakazi na kuacha kulalamika kwani Serikali ipo pamoja nao.

“Mama mjamzito hapaswi kufariki katika kituo cha afya, tafsiri yake kwamba tumeshindwa, hili la vifo vya mama na mtoto ni lazima tuliangalie,” alisema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Chaula, alisema waganga hao wanatakiwa kutoka na maazimio ambayo yataisaidia Serikali katika utendaji kazi wake.

“Lazima tutembee pamoja, tusivurugane, kazi zetu zinajulikana. Tutoke na maazimio ambayo yataisaidia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles