24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 29, 2023

Contact us: [email protected]

Maaskofu KKKT wajifungia kutafuta mkuu wa kanisa

Upendo Mosha – Moshi

KANISA la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) limeanza vikao vyake vya mkutano wa 20, unaotarajiwa kufanyika Agosti 23 ambao pamoja na mambo mengine utamchagua mkuu wa kanisa hilo na kamati mbalimbali zitakazoliongoza kwa kipindi cha miaka minne.

Mkuu wa kanisa hilo kwa sasa ni Askofu Dk. Fredrick Shoo, aliyechaguliwa Agosti mwaka 2015.

Mkutano huo unafanyika Chuo Kikuu cha kanisa hilo cha Makumira mkoani Arusha.

Katibu wa Idara ya Mawasiliano Dayosisi ya Kaskazini, Mchungaji Mathoyo Saruma, alipotafutwa kuzungumzia mkutano huo, alisema kwa sasa bado ni mapema na taarifa rasmi ataitoa Alhamisi.

 Dk. Shoo ambaye ndiye aliyefungua mkutano huo jana, anapewa nafasi ya kurudi kuliongoza kanisa hilo kwa awamu ya pili ingawa pia kuna baadhi ya maaskofu wanatajwa kuwa wanaweza kuchaguliwa kuchukua nafasi hiyo.

 Baadhi ya majina ya maaskofu wanaotajwa kuwa wanaweza kuchaguliwa kumrithi Dk. Shoo ni pamoja na Askofu wa Dayosisi ya Iringa, Braston Gavile, Askofu Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dk. Abednego Keshomshahara na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa.

“Malasusa naye anatajwa kwamba anaweza kurudi kwa sababu bado hajafikisha miaka 65 ambayo kwa mujibu wa Katiba ya Kanisa hilo ndio umri wa askofu kustaafu,” alisema mmoja wa wachungaji wa kanisa hilo.

Dk. Shoo ambaye pia ni askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, alichaguliwa Agosti 2015 baada ya kuwashinda maaskofu wenzake wawili.

Maaskofu waliochuana na Dk. Shoo kuwania nafasi hiyo baada ya kupendekezwa na Halmashauri Kuu ya KKKT, ni Askofu Dk. Stephen Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na Askofu Charles Mjema wa Dayosisi ya Pare.

Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Dk. Malasusa, alimtangaza Dk. Shoo kuwa mkuu wa kanisa hilo kwa kipindi cha miaka minne baada ya kupata kura 153, huku Dk. Munga akipata kura 67, ikiwa ni baada ya uchaguzi huo kurudiwa mara tatu kutokana na mshindi kutopata zaidi ya theluthi mbili ya kura zote.

Kanuni za uchaguzi za KKKT zinaeleza kuwa mshindi atapatikana kwa kupata kura zisizopungua theluthi mbili ya zote zilizopigwa na iwapo mshindi hatapatikana katika duru la kwanza, majina mawili yaliyopata kura nyingi ndiyo yatakayopigiwa tena kura.

Iwapo theluthi mbili haitapatikana katika duru la pili, kura ya wingi au uchache itatumika kwa duru la tatu ili kumpata mshindi.

Katika kuhakikisha mshindi anapatikana, mkutano huo ulilazimika kutumia hatua ya wingi wa kura na Dk. Shoo kuibuka mshindi.

Katika awamu ya kwanza, Askofu Mjema alipata kura 53, Dk. Munga 81 na Dk. Shoo kura 86, idadi ambayo haikufika theluthi mbili ya kura zote kulingana na kanuni za kanisa hilo jambo lililosababisha uchaguzi kurudiwa mara ya pili.

Dk. Malasusa alitangaza matokeo ya awamu ya pili ya kura zilizopigwa ambapo Askofu Munga alipata 94 na Dk. Shoo 124. Kura moja ikiharibika.

Kabla ya kuanza kwa mkutano huo wajumbe wa Halmashauri Kuu walipitisha majina hayo matatu ya maaskofu waliowania nafasi hiyo na kuyapeleka kwenye mkutano huo ili yapigiwe kura.

Wajumbe hao mara baada ya kupewa karatasi za kupigia kura, walikwenda katika vyumba maalumu kumchagua askofu wanayemtaka, na baada ya kuchagua walitakiwa kurejea ukumbini na kutumbukiza karatasi hizo katika vifaa vilivyoandaliwa kuhifadhia kura hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,259FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles