33.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunifu wa gari shamba aomba kumsaidia

Na Ashura Kazinja, Morogoro

Mbunifu wa zana za kilimo za kisasa na Mhitimu wa shahada ya kwanza ya Uhandisi Umwangiliaji na Rasilimali maji katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mkoani Morogoro, Musa Dotto, ameiomba serikali na wadau mbalimbali kumsaidia ili aweze kukamilisha gari shamba alilolibuni kwa ajili ya kumsaidia mkulima mdogo.

Kijana, Musa Dotto akiendesha gari shamba aliyoibuni ili kumsaidia mkulima mdogo nchini.

Akizungumza na MtanzaniaDigital leo mkoani hapa, Musa amesema gari shamba hilo ni wazo ambalo lilimjia kama suluhisho la ndani kwa wakulima wadogo ambao wanashindwa kuacha kutumia nyenzo duni katika kilimo kama vile majembe ya mikono na wanyama, kutokana na gharama kubwa za umiliki na uendeshaji wa mitambo mikubwa ya kilimo kama vile trekta, kutokana na kuwa na kipato kidogo.

”Baba alinipa injini ya pikipiki mbovu, hapo ndio wazo likaanza, nikaanza kununua tairi na vifaa vingine, hivyo wazo lilinijia 2017 nilipokuwa (Najifunza kwa vitendo) fildi.

‘‘Kwa hapa ilipofikia hii trekta ndogo inafanya kazi kadhaa kama usafiri na kuvuta mizigo, kwa kutumia gari shamba hili wakulima mpaka wanne wanaweza kusafiri umbali mpaka wa kilomita 50 kwa siku kwenda na kurudi kwa lita mbili za mafuta ya petrol yenye thamani ya Sh 4,000,’’ anasema Dotto.

Anasema kuwa pamoja na jitihada zake hizo ili kuweza kufanikisha mradi huo, lakini pia anaiomba serikali na sekta binafsi kumsaidia ili kuweza kufanikisha kumalizia gari shamba hilo, ambalo gharama za manunuzi kwa mkulima mdogo litakapo kamilika linaweza kufikia Sh milioni 12.

Aidha, anaongeza kuwa gari shamba hilo lina uwezo wa kupukuchua mahindi kutokana na kuendesha kinu cha kupukuchulia mahindi chenye uwezo wa kupukuchua magunia 50 ya mahindi yenye magunzi kwa saa moja, na kwamba ameshaanza kubuni majembe ambayo ni rahisi kuvutwa na gari shamba hilo ili kuleta urahisi kwa mkulima na kutumia muda mfupi.

Pia anasema gari hilo lina uwezo wa kutumika kupandia mazao kutokana na kuendesha mfumo wa upandaji yenye uwezo wa kupanda mistari minne kwa mazao ya punje kama vile mahindi, uwele, mtama na pamba ambayo ndio mazao makuu kwa wakulima wadogo nchini, na kwamba pia lina uwezo wa kufyekea shambani, kuwekea mbolea ikiwemo ya maji na  yabisi, kupuliza dawa kabla ya kufanya upandaji.

‘‘Vitu ambavyo bado vinanikwamisha ni vifaa kwa ajili ya kutengenezea hii mashine yangu, nahitaji fedha kwa ajili ya kutumia kununua vifaa na malipo kwa wale nitakaoshirikiana nao, kwani ni ajira kama ajira nyingine,’’ anasema Dotto.

Hata hivyo, Dotto anasema anahitaji msaada katika kumuunga mkono kufanikisha mradi wake huo ikiwemo fedha zaidi ya Sh milioni 25, ambapo hadi sasa ameshatumia zaidi ya Sh milioni tano fedha ambazo alikuwa akizikusanya kidogokidogo kupitia fedha ya mkopo wa Chuo.

Kufuatia ubunifu huo uliofanywa na mhitimu huyo wa SUA, baadhi ya  wanafunzi wenzake akiwemo, Anna Sanga, Clementina Dismas na Madila Mkunda wamemuunga mkono na kuiomba serikali na jamii kwa ujumla kumsaidia ili kuweza kutimiza ndoto zake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles