27.4 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali yafuta miliki mashamba mengine Tanga

Mwandishi wetu– MKINGA

SERIKALI imefuta miliki ya mashamba matatu ya Mkomazi Plantations maarufu MOA yaliyopo Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga kutokana na kukiuka masharti ya uendelezaji ikiwemo kutelekezwa bila kufanyiwa maendelezo yaliyokusudiwa na kutolipiwa kodi ya pango la ardhi.

Uamuzi huo umetangazwa jana na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipozungumza na wananchi wa Mayomboni wilayani Mkinga mkoani Tanga alipokwenda kutatua mgogoro wa muda mrefu katika eneo hilo.

Mashamba yaliyofutiwa ni lenye hati Na 9780  na ukubwa wa ekari 14,688, shamba  Na 4268  ekari 804 na shamba lenye hati Na 9781  ekari 246 ambapo mashamba yote matatu yana ukubwa wa ekari 15,738.

Kufuatia uamuzi huo vijiji 10 vyenye kaya 3,236 zilizo na wakazi 16,450 zitanufaika na uamuzi wa Serikali kutokana na wananchi wake kuvamia mashamba hayo na kufanya maendelezo ya kujenga makazi, shule na kuendesha shughuli za kilimo cha mazao ya kudumu na ya muda mfupi.

Vijiji vilivyonufaika ni uamuzi huo ni Kilulu-Dunga, Zingibari, Mwaboza, Mwakikoya, Mhandakini, Nkanyeni, Sigaya, Mayomboni, Ndumbani pamona na kijiji cha Moa

Akizugumza wakati wa kutangaza uamuzi huo, Lukuvi alisema uamuzi wa kufuta mashamba hayo unafuatia maombi yaliyotumwa kwa Raisi John Magufuli ya kutaka kufutwa mashamba hayo kutokana na kutoendelezwa na wamiliki wake kwa muda mrefu.

Alisema, Rais aliridhia maombi hayo kwa kuwa Serikali imekuwa ikisisitiza utekelezwaji wa sheria ya Ardhi Na 4 ya mwaka 1999 ikiwemo uendelezaji wa mashamba ambayo yamemilikishwa sehemu mbalimbali nchini.

Aliagiza kufanyika upimaji katika vijiji vyote 10 vilivyopo ndani ya shamba hilo sambamba na kuanishwa miapaka ya vijiji hivyo na kupatiwa hati ambapo alitaka wananchi wanaoishi kwenye vijiji hivyo kutobughudhiwa.

Katika hatua nyingine Lukuvi aliagiza kufanyika uhakiki wa mashamba mengine ya kwa Mtili Estates Co Ltd yaliyopo Mkinga mkoani Tanga ambapo ekari 58 pekee ndizo zilizoombwa kufutwa kutokana na kutoendelezwa huku mmili wake akidaiwa kumiliki ekari  2,841.

Hatua hiyo inafuatia Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili katika halmashauri ya Wilaya ya Mkainga, Obed Katonge kueleza kuwa, kwa Mtili Estates Co Ltd inalo shamba la lenye ekari 2,841 tofauti na inavyoonekana katika kumbukumbu za ofisi ya Msajili wa Hati Kanda ya Kaskazini ambazo ni 58.

Mbunge wa Jimbo la Mkinga, Dustan Kitandula, aliishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wanaoishi eneo la shamba lililofutwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles