29 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri viwanda atishia kujiuzulu endapo TBS haitabadilika

Elizabeth Kilindi-Njombe

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa ametishia kujiuzulu iwapo Shirika la Viwango nchini (TBS) halitabadili mwenendo wake katika kushughulikia kero na malalamiko ya wafanyabiashara.

Bachungwa aliyasema hayo mjini Makambako mkoani Njombe wakati alipokutana na wafanyabiashara kutoka mikoa saba nchini kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya biashara.

Katika mkutano huo uliotoka na maazimio ya kuiomba serikali kupunguza utitiri wa kodi, tozo na leseni kwa wafanyabiashara ili kunusuru sekta hiyo pia waziri huyo kwa mara nyingine tena aliinyooshea kidole TBS.

 “TBS nimeshawaambia kwamba nitajiudhuru uwaziri kama hamtabadilika sasa kwa umri huu na haka kakibarua nataka nifanye vizuri..

“TBS ujumbe ndio huo nataka tushirikiane kuhakikisha utitiri wa kero zilizokuwepo zisizokuwa na lazima zinakwisha, ifike mahali basi hawa wakawe mashahidi kwamba kweli TBS mmebadilika,”alisema.

Aliitaka TBS kubadilika ili kuendana na kasi ya serikali katika kushughulia kero na malalamiko ya wafanyabiashara kwa wakati bila ya urasimu.

Bashungwa pia alizungumzia uamuzi wa serikali kufuta kodi 54 zinazowagusa wafanyabiashara pamoja na kupunguza mamlaka za kutoa leseni za biashara.

“Kuna kodi 54 zimeshaondolewa, na hili sisiseme 54 tu nimeshamkabidhi mwenyekiti wenu hizo kodi kero 54 anazo hapo, sasa  na hiyo taarifa ipo kwenye kiingereza tuitafsiri kwa kushirikiana na wizara yangu tuisambaze kwa wafanyabiashara kwenye maeneo yenu wajue kwamba tunapozungumzia kodi 54 ni zipi?’’alisema.

Aliongeza kuwa;  “Maana najua biashara ndogondogo na za kati ndizo zinazoajiri watanzania kwa hiyo ni lazima tuwajali nyinyi na tushughulike na changamoto ambazo mnakabiliana nazo katika halmashuri zetu,”alisema.

Waziri huyo pia alisema serikali imefikia hatua nzuri ya kuandaa ‘blue print’ itakayokuwa mwongozo katika sekta ya biashara.

Awali akifafanua kiini cha kusuasua kwa sekta ya biashara nchini, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara JWT, Abdallah Mwinyi alitaja urasimu bandarini ambao unatengeneza mianya ya rushwa hatua ambayo inapingwa vikali na Kamishna wa TRA nchini Edwin Mhede ambaye anamtaka kila mfanyabiashara kuviripoti vitendo vyote vya rushwa kwani vinaikosesha nchi mapato.

Aidha Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Njombe, Sifael Msigala alipendekeza baadhi ya mambo yasimamiwe na TBS ili kuondoa usumbufu pindi bidhaa inapoingia nchini.

“Unakuta wakati mwingine umenunua bidhaa inakaguliwa bandarini, lakini ikifika huku dukani unakuta TBS wanaibuka wanasema hiki kitu hakina ubora, kwamba hii bidhaa haitakiwi,” alisema Msigala.

Katika mkutano huo wizara nne zenye mahusiano ya karibu na wafanyabiashara zilialikwa ikiwemo ya Viwanda na Biashara, Tamisemi, Fedha na Uwekezaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles