24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Array

Sekou-Toure wajivunia kupunguza vifo vya uzazi

Aveline Kitomary – Mwanza

HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou-Toure, imefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutokana na kuboreshwa kwa huduma za uzazi.

Akizungumza jana jijini Mwanza wakati wa kampeni ya ‘Tunaboresha sekta ya afya’ inayoendeshwa na maofisa habari wa taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Afya, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Uzazi na Vizazi, Clement Morabu, alisema hospitali hiyo inatoa huduma ya uzazi kwa kina mama 700 kwa mwezi.

“Idadi ya kina mama wanaojifungua imeongezeka, miaka ya nyuma ilikuwa chini ya 500 kwa mwezi, lakini sasa ni 700 kwa mwezi.

“Pia vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua. Mwaka 2017 vifo vilikuwa 21, mwaka 2018 vilikuwa 14 na mwaka 2019 ni 10. Mpango wetu ni kutokomeza kabisa vifo vitokanavyo na uzazi.

“Uboreshwaji wa huduma za afya umesaidia sana kuwafanya kina mama waendelee kuja kwa wingi na pia tunawahudumia haraka zaidi, na hii imechangia kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi,” alisema Dk. Morabu.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne cha uongozi wa Serikali ya awamu ya tano, Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Engelbert Rauya alisema wameanza ujenzi wa jengo la mama na mtoto lenye urefu wa ghorofa tano.

“Jengo hilo mpaka sasa limeshatumia Sh bilioni 4 na tunatarajia kutumia Sh bilioni 10.

“Kwa sasa hospitali inatumia vitanda 315 ambavyo havitoshi, lakini jengo hili kutakuwa na vitanda 565. Hii itasaidia kupunguza msongamano na pia idadi ya kina mama itaongezeka.

“Hospitali inahudumia wagonjwa 450 mpaka 500 kwa siku, wagonjwa wanaolazwa ni 50 mpaka 100, huku watoto wakiwa 10 mpaka 20 na kina mama wanaojifungua kwa siku ni 25 mpaka 30,” alibainisha Dk. Rauya.

Alisema kuwa hospitali imeendelea kuongeza mapato ambayo yamesaidia kuboresha miundombinu, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba pamoja na kulipa watumishi.

“Awali mwaka 2015 mapato yalikuwa Sh milioni 43 hadi 50, lakini sasa yamefikia Sh milioni 350 kwa mwezi, na kati ya hizo Sh milioni 13 tunatumia kuwalipa watumishi wa hospitali,” alisema Dk. Rauya.

Alisema hospitali hiyo inatarajia kupata huduma  ya mashine ya kisasa ya X-ray na tayari jengo  limeshakamilika.

“Katika kuimarisha huduma zetu, sasa tuna huduma nne za kibingwa na pia sasa tuna kitengo cha dharura, upatikanaji wa dawa umeongezeka ambapo sasa zinapatikana kwa asilimia 80,” alieleza Dk. Rauya.

Alisema katika hospitali hiyo pia waraibu wa dawa za kulevya wanapata huduma za dawa.

Dk. Rauya alisema kwa mwaka jana jumla ya waraibu 357 walianzishiwa huduma ya dawa, huku 236 wakiendelea na huduma za matibabu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles