31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif kugombea nafasi ya Zitto

 Mwandishi wetu -Dar es Salaam 

MSHAURI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, leo anajitosa na kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya kiongozi wa chama ndani ya chama hicho.

Nafasi hiyo kwa sasa inashikiliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ambaye huenda akajitosa kuwania uenyekiti wa ACT Wazalendo.

Taarifa kutoka ndani ya ACT Wazalendo, ziliiambia RAI kuwa hatua ya Maalim Seif kuchukua fomu ya kiongozi wa chama ni sehemu ya makubaliano yaliyo baina ya viongozi hao wawili.

Jana Maalim Seif alikuwa kiongozi wa kwanza wa juu wa chama hicho kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kujipanga kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Hatua hiyo itatokea siku chache tangu Kaimu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Doroth Semu, kutangaza kufanyika kwa uchaguzi wa chama kwa ngazi ya taifa. Aliwataka wanachama wenye sifa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

“Kama inavyofahamika, chama cha ACT Wazalendo tayari kimetangaza rasmi kuanza kwa uchaguzi wa viongozi wa kitaifa ndani ya chama baada ya kukamilika chaguzi katika ngazi za chini. Shughuli ya kuchukua na kurejesha fomu kwa nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi ya taifa imetangazwa kufanyika kuanzia tarehe 27 Januari hadi Februari 26 mwaka huu.

“Kwa taarifa hii, tunawajulisha kuwa kesho (leo) siku ya Alhamis, Februari 30, 2020 saa 5 asubuhi Maalim Seif Sharif Hamad anatarajia kuchukua fomu ya kugombea nafasi mojawapo kati ya nafasi za uongozi zilizotangazwa kugombewa katika chama cha ACT Wazalendo. Shughuli hiyo itafanyika ofisi ndogo ya chama iliyopo Vuga, Zanzibar.

“Maalim Seif pia anatarajia kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu dira na mwelekeo wake juu ya nafasi ya uongozi anayokusudia kuiomba katika chama,” ilieleza taarifa hiyo ya ACT.

Nafasi zinazowaniwa ni pamoja na Naibu Kiongozi wa Chama, Makamu Mwenyekiti Taifa-Tanzania Bara, Makamu Mwenyekiti Taifa-Zanzibar, wajumbe wa Halmashauri Kuu nafasi 15 na wajumbe wa Kamati Kuu nafasi nane. Nyingine ni Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake na makamu wake wawili, Katibu wa Ngome na naibu wake, wajumbe watatu wa Halmashauri Kuu Taifa na wajumbe watano wa Mkutano Mkuu Taifa wa ngome hiyo.

Katika Ngome ya Vijana Taifa, nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti wa Ngome, makamu wake wawili yaani wa Bara na wa Zanzibar, Katibu wa Ngome na naibu wake, wajumbe watatu wa Halmashauri Kuu Taifa na wajumbe watano wa Mkutano Mkuu Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles