26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 5, 2023

Contact us: [email protected]

SADHVI DEVA: MWANAMKE ANAYEJIITA ‘MUNGU’ ANAYEUA OVYO NCHINI INDIA

*Alitaka Waislamu, Wakristo wahasiwe

ANAFAHAMIKA kama mungu wa kike wa Kihindu, lakini alijikuta akisakwa na polisi nchini India baada ya kwenda mafichoni kufuatia kitendo chake cha kufyatua risasi harusini.

Risasi hizo zilizolenga kusherehekea tukio hilo walilokuwa wamealikwa katika hekalu la maharusi la Savitrii wilayani Karnal zilisababisha kifo cha  shangazi wa bibi harusi pamoja na kujeruhi vibaya watu wengine watatu.

Huyu ni Sadhvi Deva Thakur (28), kiongozi wa Wahindu wa India wa Mahasabha, ambaye alijisalimisha polisi wiki moja baada ya kwenda mafichoni.

Kwenye video ya tukio hilo lililotokea Novemba mwaka jana wilayani humo, katika jimbo la Kaskazini la Haryana, Sadhvi akiwa na walinzi wake sita walionekana kwa pamoja wakifyatua risasi hewani kiholela.

Mpenda bunduki huyu na watu wake ingawa ni kama walifanya kitendo hicho kama sehamu ya furaha, lakini kwa walioshuhudia walisema risasi zilirushwa hovyo mno na kuzua hofu.

Ombi la ndugu na jamaa wa maharusi pamoja na meneja wa ukumbi kuwataka wasitishe ufyatuaji huo, ambao ulifanyika wakiwa jukwaani wakati wa kusakata magoma, hazikufua dafu kwani waliendeleza ujeuri na ubabe.

Vyombo vya habari nchini India vinasema Sadhvi, ambalo ni jina la Kihindi linalomaanisha mwanamke aliye mtakatifu au anajiita kuwa mungu, awali alipanda jukwaani akamuomba DJ kuchezesha wimbo alioutaka. Ombi lake lilikubaliwa akaanza kucheza densi huku risasi zikifyatuliwa.

Ni wakati shangazi yake bwana harusi mwenye umri wa miaka 50 Sunita Rani alipoangauka baada ya kupigwa rasasi na wengine watatu kujeruhiwa vibaya, ndipo ufyatuaji huo ambao unaelezwa kuhusisha raundi 30 ya risasi ukasitishwa.

Kufuatia kitendo hicho, Makamu huyo wa Rais wa Wahindu Wote wa Mahasabha na wasaidizi wake wakatoweka mara moja eneo hilo.

Polisi wakati wakiwasaka walimfungulia Sadhvi na walinzi wake sita mashitaka ya mauaji na kujeruhi.

Wiki moja baadaye, Sadhvi Deva Thakur alijisalimisha mbele ya mahakama ya Karnal, akikana kuhusika na mauaji na kwamba amesikitika kuna mtu alikufa katika tukio lile.

Akiwa mahakamani Thakur alisema hana hatia kwamba kuna njama dhidi yake. “Nahitaji matibabu, hii ni njama dhidi yangu, kulikuwa na watu wengine waliorusha risasi.”

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi katika Jiji la Karnal, Sadhvi aliiambia mahakama kuwa wana silaha sita wanazomiliki kihalali na kaka yake pia anayo.

Polisi walikuwa wakiendelea bado na msako wa kuwasaka walinzi wake sita na walikamata magari yake mawili ya kifahari na kuliweka chini ya ulinzi hekalu lake dogo.

Sadhvi Deva Thakur  amekuwa mwanamke mtata mno na hivyo si mara ya kwanza kujikuta matatani.

Mwaka juzi polisi walisajili kesi iliyofunguliwa kumlalamikia baada ya kutoa mwito wa kutaka Waislamu na Wakaristo wahasiwe kwa nguvu ili  kuzuia idadi yao kukua.

“Idadi ya Waislamu na Wakristo inakua kila siku. Kudhibiti hili, serikali inapaswa kutengeneza sheria inayozuia Waislamu na Wakristo kuzaa watoto wengi. Wanapaswa walazimishwe kuhasiwa ili wasiongezeke idadi,” aliuambia mkusanyiko wa Wahindu.

Sadhvi alisema kuwa anakubaliana na baadhi ya viongozi wazalendo wa Kihindu kwamba wanawake wa Kihindu lazima wazae sana ili kukabiliana na hatari ya kugeuka dini ya wachache katika nchi yao wenyewe dhidi ya aliowaita wakuja.

Deva Thakur pia alitoa kauli kuwa sanamu za miungu ya Kihindu ya kiume na kike iwekwe misikitini na makanisani.

Hali kadhalika alitoa mwito sanamu ya Nathuram Godse, muuaji wa mwasisi wa India huru Mahatma Gandhi, ijengwe jimboni Haryana kwa kitendo hicho cha uuaji alichokiita cha kishujaa.

Sadhvi alizaliwa na kukulia Bras, kijiji kidogo cha Wilaya Karnal, na miaka michache iliyopita alianzisha hekalu dogo kijijini hapo. Ana wafuasi wachache na wengi wao wakiwa wanakijiji wa aneo hilo.

Kwa mujibu ya wanaomfahamu anafahamika kwa mitindo yake ya mavazi akiwa na umri wa miaka 27. Anaonekana kupendelea vito vya dhahabu na bunduki ambazo haishi kupozi nazo mara kwa mara.

Ukurasa wake wa Facebook unaosimamiwa na kaka yake Rajeev Thakur, unamuelezea kama mkurugenzi wa Deva India Foundation na anajiita ‘mzalendo.’

Dharampal Siwach, mwanachama mwandamizi wa Hindu Mahasabha jimboni Haryana anasema alisafiri na Sadhvi kwenda makao makuu ya chama chao mjini Delhi miaka mitatu iliyopita.

“Aliteuliwa kuwa makamu wa rais wa chama kitaifa baada ya mimi kuendesha kampeni kwa niaba yake,” anasema.

“Lakini haikuchukua muda tukasitisha kumualika katika shughuli zetu kwa sababu alikuwa akipigwa picha akiwa na bunduki kitu kilitufehehesha.”

Tukio la urushaji risasi ni ushahidi wa mapenzi yake na silaha.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles