23 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

SAA MOJA YA WASIOJULIKANA NYUMBANI KWA MEYA DAR

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


WATU wasiojulikana wanadaiwa kuvamia nyumbani kwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob na kufanya upekuzi, huku familia yake ikiwekwa chini ya ulinzi.

Tukio hilo lilitokea juzi usiku nyumbani kwa meya huyo, Ubungo Makoka, Dar es Salaam.

Watu hao wanaodaiwa walivalia sare na kijeshi, baada ya kufika waligonga mlango na kujitambulisha wanatoka Hospitali ya Jeshi la Lugalo na wana taarifa kuhusu mgonjwa wao ambaye ni mdogo wa Meya Jacob.

Akizungumzia tukio hilo jana, Meya Jacob, alisema watu hao walivamia kati ya 12:45 hadi saa 2 usiku wa juzi, wakaiweka familia yake chini ya ulinzi na kuingia vyumbani kufanya upekuzi huku wakirekodi kila hatua.

“Nilipokea simu kutoka kwa familia na nikarudi nyumbani, nilifanikiwa kufika nyumbani usiku uleule nikitokea kwenye Televisheni ya Kenya ya KTN kwa mahojiano na kukuta wanafamilia, majirani wote wakiwa kweye taharuki.

“Ni kweli wanaodhaniwa kuwa askari wawili waliovalia sare za jeshi na wengine watatu waliokuwa wamevalia nguo za kiraia walioongezeka baadaye, waliingia ndani ya nyumba na kuiweka familia yangu chini ya ulinzi.

“Walidumu kwa takribani muda wa saa moja kati ya mida ya saa moja kasorobo hadi saa 2 usiku.

“Wakati huo mimi sipo nyumbani, hakuna jirani, wala polisi aliyeshuhudia zoezi hilo la ukaguzi wa nyumbani kwangu, wamerekodi video na kupiga picha kila walichopekua na wanayemuhoji kwa kuwalazimisha,’’ alisema.

Alisema watu hao walipofika waligonga geti na kudai wametokea Hospitali ya Lugalo, ambako mdogo wake amelazwa na kwamba kuna taarifa muhimu wanataka kuwapatia familia.

“Na walipoingia ndani ya geti wakawageuzia kibao na kuwaweka chini ya ulinzi na kuanza zoezi la kupekua kinyume cha sheria za nchi, bila kuwa na kibali cha ukaguzi na mashahidi,’’ alisema Meya Jacob.

Akieleza jinsi watu hao walivyofika nyumbani, alisema askari waliokuwa wamevalia sare za jeshi, walimfuatilia nyuma kwa pikipiki aina ya Boxer binti yake tangu alipokuwa ametoka Hospitali ya Lugalo.

“Kabla ya kuvamia nyumbani, walipofika walimtaka asipige kelele na kumweka chini ya ulinzi nje ya uzio wa nyumbani mpaka walipomaliza zoezi lao.

“Baada ya wao kuondoka na sisi tumekagua maeneo yote waliyopekua kuangalia kama kuna kitu cha aina yoyote wameweka au kuficha, pamoja na vitu walivyoondoka navyo, lakini kwa macho ya kawaida hatujatambua jambo lolote kwa wakati huu,’’ alisema.

Alisema baada ya hapo aliondoka na kurudi Lugalo haraka usiku huo kuhakiki kama watu hao wanajulikana kama walivyojitambulisha walipoingia nyumbani kwake.

Meya Jacob alisema alipofika Lugalo alionana na daktari wa zamu, ambaye alimwambia hospitali haina utaratibu huo wala hawajawahi kufanya jambo hilo.

“Na mgonjwa wangu hana jambo la kufanya nipekuliwe nyumbani kinyume na sheria, hivyo tangu saa saba mchana mpaka sasa saa nne, yeye bado ndiye aliyempokea na ndiye anayemtibu mgonjwa wangu.

“Alisema hakuna mtu yeyote aliyetumwa rasmi na Hospitali ya Lugalo wala jeshi kwenda nyumbani kwangu kunifanyia upekuzi na ni kinyume na taratibu zao za jeshi,’’ alisema Meya Jacob.

Alisema baada ya matukio yote hayo, alikwenda Kituo cha Polisi Urafiki kutoa taarifa ya kuvamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni askari wa jeshi.

Meya Jacob alisema baada ya kuripoti, alipewa RB Na. URP/RB/3028/2018 na kurejea nyumbani kwake saa 8 usiku.

Alisema anahusisha tukio hilo na matukio mengine ya kisiasa ambayo yanaendelea kutokea siku hadi siku nchini.

Alifananisha tukio hilo na lile la kutekwa kwa mwandishi wa Mwananchi, Azory Gwanda na kuvamiwa kwa kituo cha Clouds.

Alisema hata hivyo watu hao walisikika wakimtuhumu kuwa ndani kwake kuna mitambo ya simu inasikiliza watu jambo ambalo si kweli.

 

MKE WA MEYA

Mke wa Meya Jacob, Sauda Saleh, alisema aliwaona watu watatu wakiingia ndani ya nyumba yao baada ya kujitambulisha wametoka Lugalo jeshini.

Alisema kati ya watu hao, wawili walikuwa wamevalia vazi la jeshi na mmoja alikuwa amevaa kiraia, na baada ya muda mfupi waliingia watu wengine wawili nao wakiwa wamevalia kiraia.

“Walitukusanya kwa pamoja kisha walianza ukaguzi katika nyumba yote, walinyanyua magodoro huku mtu mmoja kati yao alikuwa akipiga picha na kuchukua video.

“Walikagua vyumba vyote, lakini hatukujua wamechukua au kuweka nini kwa kuwa tuliingiwa na hofu wote kwani hatukuwahi kuona tukio kama hilo, wala halijawahi kutokea tangu mume wangu alipokuwa kiongozi anayetokana na siasa,’’ alisema Sauda.

Alisema baada ya majirani kujaa, kila mmoja alikuwa akiongea lake na kikubwa zaidi walisema watu hao walifika na usafiri wa bodaboda ambazo waliziegesha nje ya nyumba yao.

 

MAJIRANI WA MEYA

MTANZANIA ilizungumza na majirani wa Meya Jacob, akiwamo Mwajuma Jumbe aliyesema alishangaa kuziona pikipiki hizo ambazo zilishusha watu hao na kuingia ndani ya nyumba hiyo ya meya.

“Hapakuwa na kelele, lakini kwa kuwa tuko jirani na nyumba zetu zimebanana, tulikuwa tukisikia amri za kukaa kimya, lakini hatukujua nini tufanye kwa kuwa hata meya alipotafutwa kwa simu hakupatikana muda huo,” alisema.

 

KAULI YA POLISI

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Sweetbert Njewike, aliliambia MTANZANIA hajapokea taarifa za tukio hilo.

“Hilo tukio sina taarifa nalo, na hatuna taarifa ya hilo tukio hata kidogo na jiji letu kumekucha shwari kabisa,” alisema Njiwike.

Hata hivyo, ilipofika jana jioni, polisi wa Kituo cha Urafiki walifika nyumbani kwa Meya Jacob kuchunguza tukio hilo.

 

ACT WATUA POLISI

Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema anachukua tahadhari kubwa juu ya usalama wake na kwamba tayari wameshaandika barua Jeshi la Polisi kuelezea hali hiyo ya hatari.

“Chama ndio kimeandika barua na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Chama pia ameandika barua kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro,’’ alieleza Zitto.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Mohamed Babu, alisema kuna tishio la kiongozi wao na wamelazimika kuliarifu Jeshi la Polisi.

“Tumelitaarifu jeshi juu ya tishio, lakini pia waangalie maisha ya kiongozi wetu anakuwa salama na wao ndio wenye uwezo wa kuchunguza na kufahamu hilo tishio likoje,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,250FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles