
NA FERDNANDA MBAMILA, DAR ES SALAAM.
MAMLAKA ya Mapato (TRA) na wadau wa kodi (TRA) imesema imejipanga vizuri kuhakikisha kuna umakini zaidi katika kukadiria kodi ili kuepuka migogoro zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema kwa kipindi cha mwaka 2001 hadi Agosti mwaka huu rufaa za kodi 1,354 zimewasilishwa mbele ya Baraza la Rufaa ambapo kati ya hizo ni kodi ya mapato.
“Wadau wa kodi hasa washauri wafanye kazi zao kwa weledi, hasa katika kuwashauri wafanyabiashara kutimiza wajibu wao ili kuondoa ubishi usiokuwa na msingi wa kulipa kodi na kuepuka kuathiri ubora wa maamuzi yanayotolewa na TRA,” alisema Dk. Ashatu.
Alisema kuna ongezeko la thamani na ushuru wa forodha na rufaa zinajumuisha jumla ya kodi ya shilingi trilioni 4 lakini kutokana na hilo kuna kesi ambazo kodi yake iko kwenye dola milioni 443 kati ya rufaa 914 zilizonyimwa maamuzi.
“Mpaka sasa kuna rufaa 440 ambazo bado ziko katika hatua mbalimbali za usikilizwaji kabla ya kufanyiwa maamuzi, na idadi hii ya kesi ni kubwa kulinganisha na wingi wa kesi ambazo zinazidi kuwasilishwa katika Baraza la Rufaa kila mwaka,” alisema.
Alisema kwa mwaka 2013 na 2015 kulikuwa na kiwango cha pamoja cha kodi ya Sh milioni 894 kilichobishaniwa hadi kufikia Agosti mwaka huu.
“Kiwango hicho cha kodi ambacho kipo katika kesi za mwaka huu peke yake ni shilingi trioni 2.4 na kutokana na takwimu hiyo, kiwango cha kodi kinacholalamikiwa hadi sasa kitazidi kuendelea kupanda mwaka hadi mwaka,” alisema.