24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

RUFAA YA LEMA KUSIKILIZWA LEO

Na JANETH MUSHI, ARUSHA


godbless-lemaMAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha, leo inatarajia kusikiliza rufaa ya maombi ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), anayeshikiliwa katika mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo, jijini hapa.

Kusikilizwa kwa rufaa hiyo kunatokana na uamuzi wa mahakama hiyo uliotolewa Desemba 20, mwaka huu na Jaji Dk. Modesta Opiyo, ambaye alikubali maombi namba 69 ya Lema ya kuomba kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa ya dhamana yake.

Wakati akikubali maombi hayo, Jaji Dk. Opiyo alitoa siku 10 kwa ajili ya mleta maombi ambaye ni Lema, kuwasilisha notisi hiyo.

Rufaa hiyo namba 126 ya mwaka huu, iliyokatwa na mawakili wa Lema, wakiongozwa na Sheck Mfinanga, inatarajiwa kusikilizwa na Jaji Salma Maghimbi wa mahakama hiyo, leo saa tatu asubuhi.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Wakili Mfinanga alisema kuwa, lengo la rufaa hiyo ni kupinga na kudai haki ya dhamana ya Lema aliyonyimwa kutokana na makosa ya kisheria yaliyofanywa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Novemba 8, mwaka huu.

Wakili Mfinanga alisema kuwa, wameamua kukata rufaa hiyo ili kujua ni kwanini Lema amekosa dhamana ambayo awali katika mahakama hiyo, alipewa na kuwa hawaridhiki na uamuzi uliotolewa na Hakimu Desderi Kamugisha, aliyemnyima dhamana.

Alisema kwamba, Hakimu Kamugisha alisema mahakama hiyo inampa Lema dhamana kwa masharti itakayoyaweka, lakini kabla hajamalizia kutoa uamuzi wake, mawakili wa Serikali walisema wameandaa notisi ya rufaa juu ya uamuzi huo na hoja hiyo ikakubaliwa na hakimu huyo.

Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka huu, nje ya Bunge mjini Dodoma na tangu wakati huo, yuko mahabusu akituhumiwa kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli kupitia mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali jijini hapa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles