23.8 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

JUHUDI ZIFANYIKE KUTATUA CHANGAMOTO YA KUJUA KUSOMA, KUANDIKA

ndalichakoKIWANGO cha watu wanaojua kusoma na kuandika kimefikia asilimia 71.8 kwa mujibu wa Shirika la Taifa la Takwimu Tanzania wakati Shirika la Ujasusi la CIA la Amerika likisema idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika hapa nchini ni asilimia 70.6, kwa hiyo kwa wastani mtu anaweza kusema wanaojua kusoma na kuandika hapa nchini ni asilimia 70 wakati asilimia 30 nzima ya Watanzania hawajui kusoma wala kuandika.

Asilimia 70 ya raia wanaoweza kusoma na kuandika inatosha kabisa kuwafanya raia hawa kupata taarifa kuhusu uendeshaji wa Serikali yao na pia kunaweza kuwafanya wawe wadadisi. Japokuwa kujua kusoma na kuandika pekee hakutoshi kumfanya mtu kuwa na ufahamu mpana, uwezo wa kufikiri kwa kina na uwezo wa kupambanua masuala na kubaini mambo ya msingi na yasiyo ya msingi.

Ni mzigo kwa Taifa katika karne ya 21 kuwa na idadi kubwa tu ya watu wasioweza kujua kusoma wala kuandika. Mzigo huu ndio unaolifanya Taifa kupiga hatua za maendeleo kwa kasi ndogo, kuwa na mzigo wa watu wengi ambao hutegemea wengine kitaaluma.

Pia kuwa na asilimia 70 ya Watanzania wanaojua kusoma na kuandika ni fursa kwao kuanza kuwa wadadisi na wachunguzi wa mambo. Juhudi zozote za kuwazuia hawa watu kufikiri kwa kina ni juhudi za kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Leo hii kuna mitandao ya wavuti ambayo mtu anayejua kusoma na kuandika anaweza kuitumia kufanya tafiti ndogo tu na kujua mambo, isitoshe pia sasa hivi idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika imeongezeka hivyo kutotarajia watu wasihoji ni uzembe tu wa kuendelea kubakia usingizini kwa kudhani bado tupo kwenye zama za ‘zidumu fikra sahihi za Mwenyekiti wa TANU’.

Bado kuna watu zaidi ya asilimia 30 hawajui kusoma wala kuandika kwa hiyo kuna kazi kubwa ya kufanywa ya kupunguza ujinga. Lakini pia lazima cheche za fikra za wale wanaojua kusoma na kuandika zionekane. Ili kuziona lazima kuangalia uwezo wao wa kudadisi masuala, kujihusisha na shughuli za kiuchumi na kutatua changamoto za kimaisha!

Ushauri wangu kwa wahusika ni kuwa miaka minne hii ya awamu ya tano iliyosalia tuitumie kufanya kazi moja tu kubwa nayo ni kujenga msingi wa maendeleo ya nchi kwa kuamua kwa moyo wa dhati kupunguza ujinga. Msingi wowote imara wa ujenzi wa nchi ni kuwekeza katika watu wake hasa kuwapa elimu bora na sahihi.

Tupunguze idadi ya watu wasiojua kusoma wala kuandika ili tuongeze idadi ya raia wenye uwezo wa kudadisi, kufikiri kwa usahihi na kuweza kupambanua mambo! Mambo mengine yote yanaweza kuendelea kama kawaida ila uwekezaji mkubwa ufanywe kwenye eneo hili la kuongeza idadi ya watu wanaoweza kusoma na kuandika.

Madhara ya kuwa na idadi kubwa ya watu wasioweza kusoma na kuandika huathiri hata maamuzi ya viongozi kwenye vyombo vya maamuzi. Unakuta watu wazima kabisa wanapitisha sheria na sera ambazo wao wenyewe hawajazisoma wala kuzichambua kwa kina na kujua madhara yake kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.

Wasomi wachache ni rahisi kuwarubuni wajinga wengi kwa kupitisha sheria, kanuni na sera kandamizi kwa kuwa tu mchakato mzima wa upitishaji wake umejawa na mambumbumbu wengi. Lazima juhudi za makusudi zifanyike kutatua changamoto hii ya watu wasioweza kusoma wala kuandika!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,718FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles