Rufaa mtoto aliyehukumiwa kifungo yatua Mahakama Kuu

0
500

Na ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

WAKATI viongozi wa Serikali wakiwa kimya katika suala la rufaa ya kijana Baraka Nkoko aliyehukumiwa kifungo cha maisha gerezani baada ya kukamatwa akiwa chini ya umri wa miaka 18, tayari asasi za raia zimefungua rufaa hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Wakili wa kijana huyo, Fabian Mluge, alisema wakati wakiendelea na taratibu nyingine za utawala na kukusanya ushahidi, tayari wameshafungua rufaa hiyo.

Kijana huyo aliyekamatwa kwa tuhuma za kushiriki kuchoma Kituo cha Polisi Bunju, Dar es Salaam, Julai 10, 2015 alihukumiwa kifungo cha maisha jela Februari 22 mwaka huu, katika kesi iliyoendeshwa kwa karibu miaka mitatu na nusu.

Taarifa za awali ambazo MTANZANIA lilizipata baada ya kutolewa hukumu hiyo, zilieleza kuwa kijana huyo alikamatwa akiwa na umri wa miaka 17 ukiwamo uthibitisho wa cheti cha kuzaliwa na kadi ya kliniki vilivyoonesha kuwa alizaliwa Januari 24, 1997.

Hadi anakamatwa alikuwa ameishi katika eneo hilo la Bunju kwa wiki moja, akiwa mtoto asiye na uangalizi wa uhakika kutokana na kuwa mbali na familia yake.

Wakili wa kujitegemea, Mluge alisema tayari wameshawasilisha rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kwa sasa wanasubiri ipangiwe jaji kwa ajili ya kusikilizwa.

“Tayari tulishawasilisha nia ya kukata rufaa awali, na kwa sasa tumeshafungua rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na ilishasainiwa kupokewa, sasa hivi tunasubiri tu ipangiwe jaji wa kuisikiliza.

“Pia tumewasilisha barua ya maombi ya dhamana chini ya utaratibu wa hati ya dharura, ambayo itaruhusu mtuhumiwa kuachiwa kwa dhamana na kutolewa gerezani shauri hilo litakapoanza kusikilizwa na litasikilizwa akiwa nje,” alisema.

Alisema hatua ya rufaa ilielekea kukwama awali kutokana na kutopatikana nyaraka zinazothibitisha kuwa Baraka alikuwa chini ya umri wa miaka 18, lakini walijiridhisha na kuchukua hatua baada ya taarifa zilizochapwa na gazeti hili Aprili 14, mwaka huu.

  Mwanasheria wa Shirika la Wanasheria Watetezi wa Mazingira (LEAT), Stanslaus Nyembea, alisema   tayari wameanza kulifuatilia suala hilo baada ya kupata mwanga mpya kutokana na taarifa hiyo kuhusu nyaraka za kijana huyo zilizochapishwa na gazeti hili.

Alisema tayari LEAT kwa kushirikiana na mashirika mengine yanayotetea haki za binadamu ipo katika mchakato wa kuhakikisha suala la rufaa ya kijana huyo linawezeshwa kuona haki ikipatikana.

Katika hatua nyingine, Ofisa Ustawi wa Jamii, Kata ya Bunju, Michael Mihayo, alisema amekuwa akiendelea kufanya mahojiano na mmoja wa watuhumiwa ambaye aliachiwa huru na kubaini kuwa ingawa alikuwa na umri mkubwa kuliko Baraka ana athari za saikolojia zinazotokana na tukio hilo.

Alisema katika uchunguzi wake amebaini kwa mazingira aliyokuwa nayo kijana huyo wakati wa tukio hilo, ni wazi hakuwa na mtetezi kwa kuwa alisafirishwa kutoka Kigoma na mtu ambaye alimwahidi kumpa ajira na alipofika Dar es Salaam alimtelekeza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here