20.5 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Wawekezaji sasa kutumia mtandao kuomba kuwekeza nchini

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema ofisi yake imeanzisha mfumo wa kielektroniki ambao mwekezaji anaweza kuomba kuwekeza nchini akiwa popote duniani.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni wakati akijibu swali la papo kwa papo la Mbunge wa Viti Maalum, Dk. Jasmine Tiisekwa (CCM).

Dk. Tiisekwa alisema kwa kuwa dira ya maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025 ni kufikia uchumi wa kati na uchumi wa viwanda ni kigezo kimojawapo.

“Na kwa kuwa Serikali ya awamu ya tano imejielekeza kwenye uchumi wa viwanda na imejitahidi kutengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji ili waweze kuja kuwekeza, hata hivyo wawekezaji wengi wanakwamishwa na kusumbuliwa sana.

“Je, nini kauli ya Serikali kuhusu suala hili?” aliuliza Dk. Tiisekwa.

Akijibu, Waziri Mkuu alisema ofisi yake imeanzisha mfumo mpya wa kielektroniki ambao mwekezaji anaweza kuomba kuwekeza nchini akiwa popote duniani.

“Ofisi ya Waziri Mkuu tumeanzisha mfumo wa kielektroniki ambao sasa mwekezaji anaweza kuomba kutoka popote alipo.

“Tunatambua wawekezaji wako nje ya nchi, haimlazimishi yeye kuja moja kwa moja Tanzania kuanza kujaza makaratasi, anajaza huko huko Marekani kuomba nafasi ya kupata ardhi, kupata ithibati ya uwekezaji hapa nchini,” alisema Majaliwa.

Alisema Serikali imetengeneza haya yote kurahisisha mfumo wa uwekezaji kwa lengo la kupanua wigo wa uchumi hapa nchini kupitia viwanda.

“Lakini pia kufungua kupitia kilimo, kupitia madini lakini eneo maalumu mwekezaji anataka kuwekeza, sasa Tanzania imefungua fursa na kutengeneza mazingira rahisi ya uwekezaji,” alisema.

Waziri Mkuu alitoa wito kwa wawekezaji kuja  kuwekeza Tanzania, ambako alidai fursa ipo na ardhi ipo.

“Na fursa hizi sasa tumezikaribisha katika mikoa na wilaya, tunayo ardhi kwa ajili ya kukaribisha wawekezaji ili kuendelea kuongeza mapato ya halmashauri yenyewe, mikoa yenyewe na taifa kwa ujumla,” alisema.

Majaliwa alisema Tanzania imejikita katika kuboresha uchumi wake kupitia viwanda ambavyo wametoa fursa kwa Watanzania na kwa mtu yeyote kutoka taifa lolote kuja kuwekeza hapa nchini.

“Suala la uwekezaji tumelipa umuhimu mkubwa sana, hasa kwenye viwanda na awali tulikuwa tunatumia tu Taasisi ya Uwekezaji Nchini (TIC), lakini Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye uwekezaji ambapo Rais wetu, Dk. John Pombe Magufuli alipoianzisha Wizara Maaalumu ya Uwekezaji na kumteua mheshimiwa Angela Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na kumteua pia Katibu Mkuu ili kusimamia uwekezaji kwa ukaribu zaidi.

“Lengo hapa ni kuhakikisha kwamba tunaondoa usumbufu ambao wanaupata wawekezaji hao ili kuweza kuwekeza kwa urahisi zaidi.

“Hata hivyo kwenye uwekezaji sasa, tumefikia hatua nzuri sana, moja, tumetengeneza andiko maalumu (Blue Print) ambalo limeonyesha njia rahisi za uwekezaji hapa nchini kwa lengo la kuondoa usumbufu kwa wawekezaji wetu na kwahiyo tumetengeneza mazingira rahisi juu ya uwekezaji.

“Lakini mbili, tumeboresha Kituo cha Uwekezaji kwa kukaribisha wizara zote zinazoguswa na uwekezaji kwa kuwa na mtu wao pale taasisi ili mwekezaji anapokuja huduma zote kama alitakiwa kwenda Wizara ya Ardhi, ukitaka kwenda Brela, Brela yuko pale, tuna idara kama 10, 11 ambazo ziko pale za kumhudumia mwekezaji,” alisema Waziri Mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles