24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka mitano jela kwa wizi wa mtoto

Na IBRAHIM YASSIN-MBEYA

MAHAKAMA ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka mitano jela Jordan Mgena (30), mkazi wa Kahama mkoani Shinyanga kwa kosa la kuiba mtoto wa kiume (jina linahifadhiwa) mkazi wa Kijiji cha Chalangwa wilayani hapa.

Mwendesha Mashtaka Fredrick Ndosi, aliiambia mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Chunya, Osmund Ngatunga kuwa mshtakiwa alimwiba mtoto huyo nyumbani kwa wazazi wake Novemba 8, mwaka jana baada ya kufika hapo akijifanya ni mmoja wa wanafamilia hiyo akitokea Kahama.

Alisema mbinu aliyoitumia ni kuwa alikuja kumtafuta baba yake mzazi baada ya kuambiwa na mama yake kuwa yupo mkoani Mbeya katika Wilaya ya Chunya.

Ndosi ameiambia mahakama kuwa kosa hilo ni kinyume cha sheria, kifungu cha 169(1) (a)(b) sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Mshtakiwa alikamatwa Rungwa Kambikatoto Novemba 9, mwaka jana akiwa katika basi la Singida Line akielekea Shinyanga.

Mmoja wa mashahidi katika kesi hiyo, Mkuu wa Kituo cha Polisi Chunya, Mratibu Msaidizi wa Polisi Janeth Mwakabungu, akitoa ushahidi wake mahakamani, alisema alipata taarifa za kuibwa kwa mtoto kutoka kwa familia hiyo ndipo walipoanza msako wakiwa na picha ya mtoto.

Alisema walisambaza picha ya mtoto kwa njia ya simu na kuweka vizuizi katika barabara zinazoingia na kutoka katika Wilaya ya Chunya na ndipo walifanikiwa kumkamata mshtakiwa akiwa na mtoto huyo Kituo cha Rungwa Kambikatoto katika basi la Singida Line.

Janeth aliiambia mahakama kuwa awali mshtakiwa alifika hapo nyumbani Chalangwa kwa wazazi wa mtoto akitokea Isanga, Mbeya ambako aliambiwa kuwa familia yake ipo Chalangwa ndipo alipokwenda hapo na kujitambulisha kuwa ni mwanafamilia.

“Mheshimiwa hakimu, mshtakiwa ni mzoefu kutokana na namna alivyotengeneza mazingira ya kuaminiwa katika familia hatimaye kufanikiwa kumwiba mtoto na kukamatwa katika basi akiwa anakwenda Mkoa wa Shinyanga,” alisema shahidi Mwakabungu.

Kwa upande wake, mshtakiwa Mgena alikana kutenda kosa hilo na kwamba huyo ni mtoto wake ambaye alimfuata kumchukua na kwamba siku ya tukio la kukamatwa, mtoto alikuwa na shangazi yake aitwaye Helena Kahawa, hivyo hahusiki na wizi wa mtoto.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili za mashtaka na utetezi, Hakimu Ngatunga alimtia hatiani mshtakiwa na kumtaka kujitetea.

Katika utetezi wake, mshtakiwa ameiambia mahakama kuwa hilo ni kosa la kwanza, pia ana mke, mtoto na mama yake ambaye ni mgonjwa wanamtegemea, hivyo anaomba kupunguziwa adhabu.

Mwendesha mashtaka Ndosi aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili kudhibiti vitendo vya wizi vilivyokithiri nchini.

Hakimu Ngatunga alisema mahakama imemtia hatiani mshitakiwa hivyo imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka mitano jela ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia kama hiyo na rufaa ipo wazi kwa upande usioridhishwa na uamuzi wa mahakama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles