27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI YA HAKI ZA BINADAMU YAIBUA MAMBO MATANO MAZITO

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


RIPOTI ya haki za binadamu ya mwaka 2017, iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), imebaini ukiukwaji wa haki za binadamu kuongezeka ikilinganishwa na mwaka 2016.

Kutokana na hilo, ripoti hiyo pia imeainisha mambo mazito matano ambayo yamesababisha haki hizo kuvunjwa.

Akiwasilisha ripoti hiyo Dar es Salaam jana, Mtafiti wa LHRC, Fundikira Wazambi, alisema taarifa za kuandaa ripoti hiyo zilikusanywa kwa njia mbalimbali, ikiwamo taasisi za Serikali, Mahakama na Bunge.

Alisema taarifa pia zilikusanywa kutoka kwa maofisa katika halmashauri, Jeshi la Polisi, waangalizi wa haki za binadamu na asasi nyingine za kiraia.

Wazambi aliyataja mambo yaliyosababisha haki hizo kuvunjwa ni pamoja na haki ya kuishi, haki dhidi ya ukatili, haki ya kuwa huru na usalama wa mtu, uhuru wa kujieleza na kukusanyika na kujumuika.

“Haki ya kuishi ilivunjwa zaidi mwaka 2017 ukilinganishwa na mwaka 2016, sababu kubwa ikiwa ni kuendelea kwa mauaji yanayotokana na kujichukulia sheria mkononi, mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola na mauaji yatokanayo na imani za kishirikina,” alisema Wazambi.

Kuhusu kujichukulia sheria mkononi, alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana, idadi ya vifo ilifikia 917, vitano zaidi ya vilivyoripotiwa mwaka 2016.

Wazambi alisema kwa mujibu wa takwimu za miezi sita ya kwanza ya mwaka 2017, Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa matukio ya kujichukulia sheria mkononi ukifuatiwa na Mbeya, Mara, Geita, Tanga na Kigoma.

Kuhusu mauaji yanayotokana na imani za ushirikina, alisema vifo 307 viliripotiwa mwaka 2017 ambavyo ni 47 pungufu ya vilivyoripotiwa mwaka 2016.

“LHRC ilifanikiwa kukusanya matukio mawili ya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi na tukio moja la kuharibiwa kwa kaburi la mtu aliyekuwa na ulemavu wa ngozi.

“Jitihada za Serikali, polisi, mahakama na asasi za kiraia zimesaidia kupunguza matukio haya,” alisema Wazambi.

Kwa upande wa mauaji yatokanayo na imani za ushirikina kwa wazee, ripoti imebaini Mkoa wa Tabora unaongoza na Shinyanga ikiongoza kwa ndoa za utotoni.

Katika hatua nyingine, Wazambi alisema tangu walipoanza kutoa ripoti ya haki za binadamu, matukio ya watu kuuawa na watu wasiojulikana ambayo yalianzia Kibiti mkoani Pwani, yaliathiri ulinzi wa haki za binadamu.

 

UVUMILIVU WA KISIASA

Wazambi alisema ripoti hiyo ilibaini uvumilivu wa kisiasa umepungua hasa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hivyo kusababisha kuongezeka kwa chuki kati ya viongozi na wanachama.

“Hali hiyo imesababisha mivutano mikubwa na uvunjifu wa haki za binadamu, ikiwemo kuminywa kwa haki za msingi kinyume na sheria.

“Kauli za kibaguzi zilizotolewa na baadhi ya viongozi, hususani chama tawala, zilichangia kupungua uvumilivu wa kisiasa mwaka 2017,” alisema Wazambi.

Alitaja matatizo ya jumla yanayoathiri ulinzi wa haki za binadamu ni pamoja na kutokuwa na katiba madhubuti na kutoheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

“Matatizo mengine ni sheria mbaya zenye upungufu au zilizopitwa na wakati, uelewa mdogo wa sheria, zikiwamo zinazohusu haki za binadamu kwa pande zote na kutofuata utaratibu wa sheria.

“Nyingine ni mapungufu ya bajeti katika sekta muhimu, kutotii sheria, uelewa mdogo wa haki za binadamu baina ya wananchi na viongozi wao, kukosekana uwajibikaji wa kitaasisi na hata mtu mmoja mmoja,” alisema Wazambi.

Kutokana na hilo, LHRC imeishauri Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi, pale yanapotokea mauaji ya kujichukulia sheria mkononi na yanayofanywa na vyombo vya dola, hatua zichukuliwe haraka na wakosaji wawajibishwe na kupelekwa mbele ya vyombo vya sheria kwa wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles