23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Rais wa Angola hataki mazungumzo na dos Santos

LUANDA, ANGOLA

RAIS wa Angola, Joao Lourenco amesema hakutakuwa na mazungumzo yoyote na familia ya mtangulizi wake, Jose Edouardo dos Santos, kuhusiana na tuhuma za ubadhirifu zinazomuandama binti wa rais huyo mstaafu, Isabel.

Shutuma za ubadhirifu zimeiandama serikali ya Angola inayoongozwa na Rais Joao Lourenco tangu ilipoingia madarakani mwaka 2017, licha ya ahadi zake wakati wa kampeni kwamba angeleta mageuzi ya kiuchumi na kupambana na ufisadi.

Isabel ambaye ni mwanamke tajiri zaidi barani Afrika anatuhumiwa kutumia ushawishi wa baba yake kujenga himaya ya kiuchumi yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni mbili.

Wiki chache zilizopita, ripoti ya wachunguzi wa kimataifa walibainisha kuwepo njama ya kuyachota mamilioni ya dola kutoka katika hazina ya serikali na kuhamishiwa katika akaunti za watu binafsi kupitia hila zinazowahusisha maofisa wa serikali. 

Aidha, tetesi zilienea kuwa mshukiwa mkuu katika njama hizo, Isabel dos Santos, alikuwa akijadiliana na serikali ili aweze kuzirudisha fedha anazodaiwa kuziiba. 

Katika mazungumzo na DW, Rais Lourenco amesema taarifa zote hizo hazina msingi.

”Tungependa kusema wazi kuwa hakuna majadiliano, na hakutakuwepo majadiliano. Watu wanaohusika walipewa muda wa miezi sita kurejesha mali waliyoipata kwa njia haramu kutoka hazina ya taifa. Wale ambao hawakuutumia muda huo, watawajibika kwa hatua zinazoweza kufuata,” amesema Lourenco.

Mali ya Isabel iliyoko nchini Angola hivi sasa inashikiliwa, na Januari 22 Mwendesha Mashtaka mkuu alimfungulia mashtaka ya utakatishaji wa fedha, matumizi mabaya, kughushi nyaraka pamoja na uhalifu mwingine wa kifedha alipokuwa kiongozi wa kampuni ya taifa ya mafuta ya Angola. 

Alipoulizwa kama angependa kumwona Isabel dos Santos akipandishwa kizimbani, Rais Lourenco alisema; “hiyo ni kazi ya mahakama, sio ya mwanasiasa,”. 

Jibu lilikuwa hilo hilo, alipoulizwa ikiwa mtangulizi wake, Jose Edouardo dos Santos anaweza kufunguliwa mashtaka baada ya kinga ya miaka mitano kumalizika.

”Ni taasisi za kisheria ambazo huwachunguza washukiwa wa uhalifu. Kazi ya wanasiasa ni kuweka sera ambazo zinahakikisha uhuru wa mahakama, na kuzifanya mahakama kufanya kazi ndani ya mipaka yake. Rais hawapeleki watu mahakamani. Kuna kesi nyingi nchini.,” ameongeza Lourenco.

Alipoulizwa kuhusu shutuma za upinzani kwamba hakuna mabadiliko yoyote katika mfumo wa mahakama, Rais Lourenco amesema hiyo sio kweli. 

Aidha, amekiri mchango wake kama ofisa wa ngazi ya juu katika serikali ya mtangulizi wake, na kusema uzoefu huo umemwezesha kujua kuwepo kwa ufisadi katika ngazi za juu, ambao sasa anasema amepata fursa ya kuupiga vita.

Marais wa Angola na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wamemtaka binti wa rais wa zamani wa Angola, Isabel dos Santos na mumewe Sindika Dokolo kushirikiana na mahakama baada ya mali zao kuzuiwa na serikali.

Isabel amekuwa akikanusha madai ya ufisadi  baada ya mahakama mjini Luanda kuifunga akaunti yake ya benki. Amesema madai hayo dhidi yake yamechochewa kisiasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles