30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara yazindua mwongozo wa saratani

Aveline Kitomary – Dar es Salaam

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imezindua mwongozo wa taifa wa matibabu ya saratani, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kupunguza ugonjwa huo na athari zake.

Mwongozo huo pia umelenga mfumo mmoja wenye ubora wa utoaji huduma za matibabu ya ugonjwa wa saratani katika hospitali zote zilizopo nchini.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani ambayo hufanyika Februari 4 ya kila mwaka, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema hatua hii imekuja kutokana na kuendelea kuongezeka kasi ya ugonjwa huo duniani.

“Ni matumaini yangu mwongozo huu utarahisisha mawasiliano kati madaktari bingwa na wataalamu wengine wa saratani, utatoa dira ya nchi nzima kulingana na ubora wa matibabu ya saratani.

“Mwongozo unasema kabla mgonjwa hajaanza matibabu wataalamu watakaa kumjadili mgonjwa na wataamua ni jinsi gani waweze kumtibu na watakaa halafu waamue atumie matibabu gani, utarahisisha uandaaji wa maoteo ya ununuzi wa dawa na vitendanishi na vinavyotumika kutibu  saratani, utoaji wa matibabu bila madhara ya kiteknolojia ya mionzi,” alisema Ummy.

Alisema mwongozo huo pia utatoa maelekezo kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili vipimo na dawa za saratani viwepo katika vifurushi vyao.

“Mfuko wa Bima ya Afya uhakikishe unatumia mwongozo huu katika kuweka vitita vya huduma za saratani hili mliangalie kama kwenye vifurushi mnatoa huduma za CT scan halafu hapati matibabu ndo nini? Nimewaelekeza NHIF waangalie waongeze hata fedha kwani mtu anaweza hata kupata tatizo la figo, tuhakikishe watu wanapata matibabu,” alisema Ummy.

Alisema utawawezesha wananchi kupata matibabu bora kutokana na tiba zote kufanana katika hospitali zote.

“Mwongozo huu utasaidia watu kupata elimu, uhamasishaji wa kwenda kupima mapema kabla saratani zao hazijafika mbali, hii itasaidia watu wengi kuwahi hospitali na kupata matibabu kabla ugonjwa haujafikia hatua za juu,” alisema Ummy.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani, kila mwaka kati ya watu 100,000 walioko nchini, wagonjwa wapya wa saratani ni 76.

Alisema shirika hilo linakadiria wagonjwa wapya kila mwaka ni 42,060 na katika kila wagonjwa hao, vifo ni takribani asilimia 68, kwahiyo katika kila wagonjwa 100 wagonjwa 68 wanafariki, jumla ya wagonjwa 28,000 hufariki kwa mwaka.

“Takwimu za hospitali zinazohudumia wagonjwa wa saratani jumla yao ni 13,216 kwahiyo wagonjwa wengi wa saratani hawafiki katika vituo vya kutoa huduma, wanabaki majumbani au kwenda kwa waganga wa kienyeji.

“Hivyo ni changamoto, ni asilimia 31 tu wanafika kupata huduma, tunawahimiza watu  wanaohisi kuwa na ugonjwa huo kufika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Lakini tatizo jingine ni wagonjwa asilimia 70 wanaofika hospitali wanakuja wakiwa katika hatua ya juu ya saratani, hii ni hao wagonjwa asilimia 31 wanaofika kupata huduma.

 “Takwimu tulizonazo ni kuwa saratani inayoongza kwa wanaume ni ile saratani ya tezi dume asilimia 23, koo asilimia 16, saratani ya kichwa na shingo asilimia 12, saratani ya utumbo mkubwa na mdogo asilimia 11.4 na matezi asilimia 9.

“Saratani zinazokumba wanawake ni mlango wa kizazi asilimia 47, saratani ya matiti asilimia 16, saratani ya utumbo mkubwa na mdogo asilimia 5.8, saratani ya koo 5.3, saratani ya kichwa na shingo asilimia 4.2.

“Takwimu za Ocean Road wagonjwa wengi wa saratani zinasababishwa na maambukizi ya virusi, mfano zaidi ya asilimia 50 ya wanaume wenye umri kuanzia miaka 30 mpaka 49 wamekuwa wakikumbwa na saratani, sasa tunaona hata vijana wanakumbwa na saratani,” alisema Ummy.

Hata hivyo, alisema Serikali inaendelea kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuwekeza zaidi katika kinga ya saratani.

“Tutaendelea kuchukua hatua za kuboresha huduma za matibabu ya saratani, tukiwekeza zaidi katika kinga mfano saratani ya mlango wa kizazi, inaweza kuzuiwa kwa chanjo, takwimu ya mwaka 2018/2019 inaonyesha kuwa wasichana wa umri wa miaka 9 hadi 14 waliopata chanjo dozi ya kwanza ni 81, lakini kwa chanjo ya pili ni asilimia 49.

“Niwatoe hofu jamii, chanjo hii haihusiani na kinga ya uzazi wala uzazi, hivyo wahakikishe wasichana wote wapate dozi zote mbili, wakati tunazindua mwangozo. Pia tutaendelea kuboresha huduma za uchunguzi ya matibabu ya saratani katika ngazi zote kwa ajili ya kugundua mapema,” alisema Ummy.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles