23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia aagiza askari Magereza waliopanda vyeo kuacha kukaa ofisini

*Asema hawezi kuajiri askari wengine, waliopo wachape kazi

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

RAIS Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Magereza kuhakikisha askari waliopanda vyeo wanaendelea kutekeleza  majukumu yao ikiwa ni pamoja na kulinda wafungwa  na kuacha tabia ya kurundikana ofisini pasipokuwa na kazi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza na Maafisa mbalimbali wa Jeshi la Magereza pamoja na Wananchi mara baada ya kuweka Mawe ya Msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya Jeshi la Magereza Makao Makuu Mkoani Dodoma leo Machi 25, 2022.

Akizungumza leo Ijumaa Machi 25, 2022 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi kwenye miradi ya Makao Makuu ya Magereza, Rais Samia amesema hawezi kuajiri askari wengine bali waliopandishwa vyeo wanatakiwa kufanya kazi ikiwemo kurudi kuwasimamia wafungwa.

Miradi aliyozindua ni pamoja Isanga Bussines Centre, nyumba 13 za askari, kiwanda cha thamani, Hospitali ya Jeshi na magari na mitambo.

“Hatuwezi kuajiri, msitulazimishe kuajiri watu wapya kwa sababu watu wengi wamepanda vyeo, vinginevyo mtanifanya sasa nisipandishe kwa sababu nikipandisha mnakuwa hamna kazi ya kufanya.

“Haina maana kama mtu ana cheo akabaki ofisini hana kazi na kama umepandishwa vyeo nina hakika kuna watu wanazurura kwenye korido za maofisini hawana kazi, warudi wakasimamie wafungwa,”amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia ameyataka Majeshi kujikita katika miradi mikubwa bila kuacha kazi zao za msingi ikiwa ni pamoja na kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza uzalishaji zaidi.

Vilivile, amesema ameona kasoro kadhaa katika miradi inayotekelezwa na jeshi hilo ikiwemo kutokuwa na uhusiano mzuri kati ya jeshi la Magereza na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

“Mngeshirikiana mngefanya vizuri zaidi. Baadhi ya miradi mmejifanyia tu mingine hamjafuata sheria. Wizara muwe karibu na Jeshi,” amesema Rais Samia.

Aidha, amemwagiza Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylivester Mwakitalu kuliangalia kwa umakini suala la mlundikano wa makabusu na zile kesi ambazo hazina ushahidi wazimalize mapema.

Kuhusiana na uvamizi wa maeneo, amesema anazotaarifa kwamba baadhi ya maafisa wamekuwa wakigawana viwanja pindi wanapokuwa wamestaafu.

“Ninazo taarifa mkistaafu mnakatiana tu maeneo wekeni eneo maalum kwamba hili mtagawana wakati wa kustaafu.Wananchi wakivamia waangalieni wasivamie,”amesema.

Kuhusiana na uhaba sare za askari,Rais amesema Serikali imeongeza bajeti katika Jeshi hilo hivyo wanatakiwa kupeleka tenda katika Jeshi la Polisi kwani wana kiwanda kikubwa cha ushonaji.

“Niwahakikishieni Serikali itakuwa pamoja na Jeshi la Magereza tutaangalia maslahi yenu mengi mazuri yanakuja Serikali inathamini mchango wenu,”amesema Rais Samia.

Aidha, amesema kuna tetesi kwamba katika Jeshi hilo hawazungumzi lugha moja na wanaombeana mabaya hivyo amewaomba kudumisha umoja na mshikamano kwani Jeshi hilo sio mali yao.

Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamadi Yusuphu Masauni amesema lazima kuwe na mageuzi katika jeshi hilo, ikiwemo Shirika kufanya shughuli zake kibiashara pamoja na kuongeza uwezo wa kujitegemea.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza, Seleman Mzee amesema kwa sasa wanatekeleza miradi mbalimbali ambayo imewasaidia kuanza kujitegemea.

Ameitaja miradi hiyo ni ufyatuaji wa matofali, viwanda vya thamani, viwanda vya kokoto, ujenzi wa miundombinu zikiwemo fremu, ujenzi wa zahanati, uzalishaji wa mbegu.

Amesema kwa sasa jeshi hilo linajitegemea kwa asilimia 82 mara baada ya kuondoa wazabuni ambapo amedai wameweza kuokoa zaidi ya Sh bilioni moja kwa mwezi.

Kamishna huyo wa Mmagereza amesema wanakabililiwa na changamoto za msongamano wa mahabusu,uhaba wa sare za maafisa,pamoja na uhaba wa askari.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles