22.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Kamati ya Siasa CCM Songwe yashauri mfumo wa Force Akaunti ubadilishwe

Na Denis Sinkonde, Songwe

Kamati ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Songwe kimekagua miradi ya maendeleo wilayani Ileje mkoani humo na kuridhishwa na usimamizi na matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo huku wakishauri mfumo wa usimamizi wa miradi kwa nguvu za wananchi (Force Akaunti) ubadilishwe.

Mwenyekiti wa CCM mkoani Songwe, Elynico Mkola, akiwa na baadhi ya wajumbe wakisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Akizungumza jana kwa nyakati tofauti wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo iliyofanyika Machi 24, 2022, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Elynico Mkola amesema wameridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya Chama ambayo imeendelea kuleta manufaa kwa wananchi.

Mkola amesema nguvu za wananchi zinasaidia kuokoa fedha na kuongeza miradi mingine lakini mradi unapotekelezwa nje na wakati hakuna wa kumchukulia hatua.

“Usimamizi wa miradi kwa kutumia nguvu ya wananchi ipanuliwe zaidi ikiwepo kuongeza vifungu vitakavyowabana na kuwachukulia hatua Wakandarasi watakaokwamisha miradi kutokamilika kwa wakati,” amesema Mkola.

Mkola amesema lengo la kutaka kuongeza vifungu kwenye miradi inayotekelezwa kwa nguvu za wananchi ni kubana fundi anayeshika kazi ya ujenzi ili kuchukuliwa hatua atakaposhindwa kumaliza mradi.

Mkola amesema kamati hiyo imekagua miradi yenye thamani ya zaidi Sh milioni 600 ikiwemo ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi shule ya sekondari Kakoma Sh milioni 40, vyumba viwili vya madarasa na ofisi shule ya msingi Mpaka Sh milioni 40, ujenzi wa wodi tatu za wanawake, wanaume na watoto Sh milioni 500, ujenzi wa vyumba viwili 2 vya madarasa na ofisi shule ya sekondari Steven Kibona Sh milioni 40 na vyumba vitatu vya madarasa shule ya sekondari Kafule Sh milioni 60.

Aidha, Mwenyekiti huyo amesema katika mradi wowote nguvu kazi ya mwananchi ithaminiwe sambamba na kuunda Kamati za Manunuzi, ujenzi huku akishauri viongozi wa chama na serikali kushirikiana katika kusimamia miradi pasipokudharauliana kwani maendeleo hayana chama.

Wajumbe wa Kamati ya Siasa wakikagua moja ya mradi wa wodi za wagonjwa hospitali ya Wilaya ya Ileje.

Wakizumgumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa akiwepo MNEC mkoani humo, Stanslaus Nsonjo na Job Kabigi wamempongeza Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Anna Gidarya kwa usimamizi mzuri wa miradi na kuwaomba viongozi kumuunga mkono ili kutimiza mahitaji ya wana-Ileje.

“Mmejitahidi kusimamia miradi vizuri kwa wakati lakini mnapaswa kufanya kazi kama timu kwa kushirikishana lengo likiwa ni kuipaiaha Ileje na kuondoa dhana ya awali ya miradi kutokamilika kutokana na watu wachache waliokuwa hawashirikishi,” Wamesema wajumbe hao.

Kwa upande wake, DC Gidarya ameishukuru kamati hiyo kwa kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana ili wananchi waendelee kunufaika.

“Miradi ambayo haikukamilika kwa wakati, kama viongozi wa halmashauri kupitia Baraza la Madiwani wametenga bajeti kukamilisha majengo ya wodi tatu za hospitali, sambamba na zahanati ya Chembe na mradi wa vyoo,” amesema Gidarya

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles