Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli jana amepokea hati za utambulisho za mabalozi watatu wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, iliwataja mabalozi hao ni Manfred Fanti (Umoja wa Ulaya – EU), Riitta Swan (Finland) na Meja Jenerali Charles Karamba (Rwanda).
Akizungumza na Rais Magufuli baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho, Balozi Fanti aliishukuru Tanzania kwa kumpokea kuja kuiwakilisha EU hapa nchini.
Alisema katika kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano, atajielekeza zaidi katika masuala ya maendeleo kwa kuwa anaamini kuna mambo mengi na mazuri ya kufanya yatakayoiwezesha Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kama ilivyopanga.
Balozi Fanti alisema anaamini mazungumzo ya pamoja kati ya Tanzania na EU katika masuala mbalimbali na kwamba anatarajia kutilia mkazo miradi ya kuzalisha nishati ya umeme kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na utekelezaji wa miradi mingine iliyopo katika makubaliano ya 11 ya mkataba wa Mfuko wa Maendeleo ya EU uliotengewa Sh trilioni 1.583 kuhakikisha yanatekelezwa.
Rais Magufuli alimpongeza Balozi Fanti kwa msimamo wake wa kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na EU na amesema Tanzania inatambua uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo na kwamba ipo tayari kushirikiana naye katika utekelezaji wa masuala yenye masilahi kwa pande zote mbili.
Kwa upande wake, Balozi Swan pamoja na kushukuru kwa kupokewa, alimpongeza Rais Magufuli kwa mafanikio makubwa katika kupambana na rushwa.
Alisema katika kipindi chake hapa nchini atahakikisha maeneo ya uhusiano kati ya Tanzania na Finland yanaimarishwa, ikiwamo mradi wa utunzaji wa mazingira, kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na utawala bora.
Naye Balozi Meja Jenerali Karamba aliishukuru Tanzania kwa kumkaribisha na amemhakikishia Rais Magufuli kuwa katika kipindi chake atahakikisha matarajio ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame ya kukuza zaidi uhusiano wa nchi hizo yanafanikiwa.
“Sisi ni ndugu na ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, mwenyekiti wetu ni Rais wa Rwanda, Paul Kagame, hatuna sababu ya kupoteza muda, nataka usukume sana suala la kuongeza biashara kati ya nchi ili zinufaike zaidi,” alisema Rais Magufuli.