Serikali yatangaza neema kwa watumishi

0
1590
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika

RAMADHAN HASSAN -DODOMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika, amezitaka wizara pamoja na taasisi zote kuhakikisha zinawalipa mishahara pamoja na stahili zote watumishi ambao wamepandishwa madaraja kulingana na nafasi walizo nazo sasa.

Pia ameagiza upandishaji wa madaraja kwa watumishi na wapewe nafasi ya upendeleo wale ambao wanakaribia kustaafu.

Hatua hiyo imekuja kutokana na wajumbe wa Baraza Kuu la Nne la Wafanyakazi katika Utumishi wa Umma kumlalamikia kwamba baadhi ya watumishi wamekuwa wakipandishwa madaraja, lakini hawalipwi stahiki zao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana wakati akizindua na kufungua mkutano wa baraza hilo, Waziri Mkuchika  alisema  kumekuwa na malalamiko katika maeneo mbalimbali nchini kuwa watumishi ambao Serikali ilitoa maagizo kuwa wapandishwe madaraja, mishahara yao imebaki kama ilivyokuwa awali.

“Nilikuwa mkoani Ruvuma, huko pia nimekutana na malalamiko ya kutosha, kila mtumishi analalamika kuwa kapanda daraja, lakini mshahara bado haujapanda,” alisema Mkuchika.

Alisema kutokana na hali hiyo, viongozi wa Serikali wanaohusika na suala hilo wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanalifanyia kazi ili kuweza kuwapatia stahili zao watumishi wote waliopanda madaraja.

Pia aliagiza katika upandishaji wa madaraja kwa watumishi, wapewe nafasi ya upendeleo wale ambao wanakaribia kustaafu.

“Serikali ilitangaza upandishaji wa madaraja kwa wale wenye sifa, lakini pia wanaotakiwa kupatiwa kipaumbele ni wale ambao wanakaribia kustaafu katika utumishi wa umma ili waweze kupata stahiki ambazo zitawawezesha kujikimu kule wanakokwenda,” alisema Mkuchika.

Alisema  Novemba mosi, 2017, Serikali iliidhinisha watumishi wapatao 85,000 waliokasimiwa katika bajeti ya mwaka 2015/16 kupandishwa vyeo.

“Awamu nyingine ya upandishaji wa vyeo imefanyika Mei 1, 2019 ambapo watumishi 193,166 waliokasimiwa katika bajeti ya mwaka 2017/18 wamepandishwa vyeo,” alifafanua Mkuchika.

Aliwapongeza watumishi wote wa umma nchini ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kukusanya na kusimamia mapato ya Serikali ambayo yanatumika katika kuboresha miundombinu mbalimbali.

“Nyie ndiyo mmekuwa mkikusanya haya mapato ya Serikali, niwapongeze kwa kiasi kikubwa kwani hapo zamani kabla ya hii awamu ya tano, tulikuwa tukikusanya kwa mwezi kiasi cha Sh  bilioni 800, lakini hivi sasa imefikia hadi Sh trilioni 1.7 kwa mwezi kiasi ambacho tunatakiwa kushikilia hapohapo,” alisema.

Aliwataka watumishi wa umma waliopo chini ya Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, kuhakikisha wanakuwa wa mfano katika suala la kupinga rushwa na kufanya kazi kwa uadilifu bila ya kuchagua maeneo ya kwenda kufanya kazi.

“Rushwa katika ofisi za umma imekuwa kikwazo kwa wananchi wetu tunaowatumikia, naomba katika ofisi yangu watumishi wangu muwe watu wa mfano, ambao mtakuwa hamjihusishi na rushwa hata kidogo ili kuakisi jina la utawala bora,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Leah Ulaya, alisema changamoto ambazo zimekuwa kero kwa watumishi ni upandishwaji wa madaraja bila kuzingatia stahiki nyingine ikiwemo mishahara.

“Tunakuomba mheshimiwa waziri suala hili lifanyiwe kazi ili sisi watumishi ambao tumepata fursa ya kupanda madaraja tuweze kupata stahiki zetu kulingana na miongozo ya utumishi wa umma,” alisema Ulaya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here