25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Putin, Kim wakutana kwa mara ya kwanza

MOSCOW, URUSI

RAIS Vladimir Putin na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong un wamekutana kwa mara ya kwanza wote wakiahidi kuimarisha uhusiano wa karibu wenye lengo la kukabiliana na ushawishi wa Marekani.

Mkutano baina ya viongozi hao wawili katika mji wa mashariki ya Urusi wa Vladivostok umekuja wakati Kim anajaribu kukabiliana na Marekani kuhusu mpango wake wa nyuklia na wakati Putin analenga kuifanya Urusi kuwa taifa la mstari wa mbele katika mvutano huo.

Viongozi hao walipeana mikono na kutabasamu kabla ya kuelekea katika mazungumzo ya faragha yaliyodumu kwa saa mbili.

Katika taarifa fupi iliyotolewa kabla ya kuanza kwa mkutano huo, Kim na Putin walisema wanalenga kuimarisha uhusiano baina yao kwa kiwango sawa na enzi za muungano wa zamani wa Kisovieti ambao ulimuunga mkono kiongozi mwasisi wa Korea Kaskazini na babu wa Kim, marehemu Kim Ill Sung.

Kim alisema anatumaini kubadili uhusiano wa sasa na Urusi kuwa imara na wenye mashiko wakati Putin alisema ziara hiyo inakoleza uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kwa mataifa hayo mawili.

Wakati wanadiplomasia kutoka pande zote mbili walipojiunga na viongozi hao kwa mazungumzo ya ngazi ya juu Kim alisema: “Ndugu Rais, tumekuwa na mazungumzo ya manufaa na ya ana kwa ana kuhusu masuala ya masilahi yetu ya pamoja na matatizo yetu ya sasa. Nakushukuru sana kwa muda uliotenga.”

Mkutano huo ulikuwa wa kwanza kwa Kim na kiongozi wa nchi nyingine tangu aliporejea kutoka mkutano wa Hanoi, Vietnam na Rais wa Marekani, Donald Trump Februari mwaka huu, ambao ulivunjika bila ya kufikia makubaliano kuhusu hatima ya silaha za nyuklia za nchi yake.

Rais Putin alisema suala la hali ya usalama katika rasi ya Korea ilikuwa sehemu ya ajenda za mazungumzo yao.

 “Bila shaka tumezungumzia hali katika rasi ya Korea na tumebadilishana mawazo juu ya vipi na nini kinapaswa kufanywa kuimarisha hali iliyopo kwa ajili ya siku bora za baadae,” alisema.

Aidha alisema Korea Kaskazini ina haki ya kuhakikishiwa usalama wake kabla ya suala la kuachana na nyuklia.

Aliendelea kusema kuwa atamweleza Rais Trump msimamo wa taifa hilo na namna nzuri ya kufikia mwafaka kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Tangu Machi mwaka jana, Kim amekwishafanya mikutano minne na rais wa China, mitatu na rais wa Korea Kusini pamoja na miwili na Trump.

Wakati wa mkutano na Trump, Marekani ilisema makubaliano hayakufikiwa kwa sababu Korea Kaskazini ilitoa masharti ya kuondolewa vikwazo vyote bila kueleza yenyewe itafanya nini kuhusu silaha zake za nyuklia.

Urusi imekwishatoa wito wa kuondolewa vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini wakati Marekani inaituhumu nchi hiyo kwa kuvikiuka madai ambayo Moscow imeyakanusha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles