28.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

JPM: Laini za simu zisajiliwe hadi Desemba

Waandishi Wetu-Dar es Salaam/Mbeya

RAIS Dk. John Magufuli, ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kufanya usajili wa laini za simu kwa kutumia Vitambulisho vya Taifa hadi Desemba mwaka huu, kwa sababu Watanzania walivyo navyo ni zaidi ya milioni 13 au milioni 14 kati ya milioni 55.

Akizungumza katika viwanja vya Ruanda Nzovwe, Mbeya jana, ikiwa ni siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaotimiza miaka 55, Magufuli alisema mpango huo hauwezekani iwapo vitambulisho hivyo havijatolewa kwa Watanzania wote.

“Katika logic ya kawaida, Tanzania tuko milioni 55, vitambulisho vya taifa nafikiri vimeshatolewa milioni 13 au milioni 14, ukishazungumza watu wote wasajiliwe kwa vitambulisho vya taifa wakati Nida haijamaliza kutoa vitambulisho, maana yake unawaeleza baadhi ya Watanzania zaidi ya milioni 20 wasiwe na simu.

“Hatuwezi tukaenda kwa utaratibu huo, kama vitambulisho vya taifa havijatolewa kwa Watanzania wote, ile statement ya kwamba mtu mwenye simu lazima asajiliwe kwa kutumia kitambulisho cha taifa haiwezekani,” alisema.

Magufuli alisema suala hilo linalofanywa na TCRA na wizara husika ni zuri kwa kuwa nchi zilizoendelea zinafanya hivyo kupunguza uhalifu, lakini linapaswa kwenda sambamba na usajili wa vitambulisho kupitia Nida.

“Waanze kwa wale wenye vitambulisho ambao wako milioni 13, 14 ambao hawana wawape muda hadi Desemba. Ili mpango wa kutoa vitambulisho uendane na zoezi la kusajili. Vitambulisho visipotolewa kwa Watanzania wote hakuna kuwahukumu watu kwa sababu hawajasajili. Sijasema watu wasisajili simu zao, lakini haya yote ya usajili wa vitambulisho na usajili wa simu iende kwa pamoja na kwa uharaka,” alisema.

Akizungumzia Muungano, alisema unapaswa kuendelea kulindwa na kwamba yeyote mwenye nia ya kuuvunja atavunjika mwenyewe.

Aliwapongeza waasisi wa Muungano huo, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume, huku akieleza kuwa kulikuwa na sababu nne za kuwa nao.

Alizitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na maono ya watangulizi ambao ni Mwalimu Nyerere na Karume, jiografia baina ya maeneo hayo, uhusiano wa kindugu na uhusiano wa kirafiki kati ya vyama viwili, Tanu na ASP, ambavyo navyo viliungana mwaka 1977 na kutengeneza CCM.

Pia aliwapongeza viongozi waliofuata, vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kuulinda Muungano.

Alisema ingawa hakuna shamrashamra lakini ni siku muhimu ya kutafakari tulikotoka na aliwahakikishia Watanzania kuendelea kuulinda Muungano akiwa pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Alisema katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu, Serikali imejitahidi kutekeleza ahadi na kubwa ikiwa kudumisha amani pamoja na Muungano.

Alisema katika kipindi hiki mafanikio ni mengi na kwamba mapato yameongezeka kutoka Sh bilioni 850 hadi Sh trilioni 1.3.

Akizungumzia miundombinu mkoani Mbeya, alisema Barabara ya Chunya imekamilika na ataweka jiwe la msingi.

Alisema alichoka kuona kila siku magari yanaanguka na kusababisha vifo hivyo atatumia fedha za Serikali kukamilisha ujenzi wa barabara husika.

Alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, kwa mafanikio na kusisitiza hakuna wa kumtoa ni yeye na Mungu, hivyo atabaki Mbeya.

Alisema kuongoza ni msalaba kwa sababu hata mitume walipata shida si kila mmoja atampenda.

“Makusanyo kabla ya mkuu wa mkoa hajaja ilikuwa shilingi bilioni 2.5, leo ni shilingi bilioni tano, ndiyo maana na mkurugenzi nikaleta polisi. Nilifanya kwa makusudi sikujaribu, nilitaka mkusanya fedha awe polisi ili akisumbua anachukua hatua, ana nyota zake,” alisema.

Magufuli alisema wakati miradi inatekelezwa lengo lilikuwa kutekeleza shughuli za uchumi na uzalishaji ambavyo vinategemea miundombinu ndiyo maana Serikali ilinunua ndege.

Pia alisema Mbeya kuna vivutio vingi vya utalii ambavyo havitangazwi ikiwamo Hifadhi ya Ruaha, Ziwa Ngosi, Hifadhi ya Kitulo au Bustani ya Mungu na kwamba asilimia 70 ya watalii husafiri kwa ndege hivyo Serikali iliamua kuzinunua nane, kujenga rada nne na kupanua viwanja 11 nchi nzima ikiwamo cha Songwe.

Alimwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, kukamilisha baadhi ya mambo yaliyobaki ili jiji hilo liweze kufanya biashara ya utalii kwa ndege kutua hapo na kurudi nchi nyingine.

HUDUMA ZA JAMII

Alisema Mbeya imeimarishiwa vituo vya afya 14 pamoja na hospitali na kuongeza bajeti ya dawa.

Kuhusu suala la elimu bure, alisema Sh bilioni 23.867 zinatolewa kila mwezi kwa ajili ya kusomesha wanafunzi nchini.

Alisema tozo 80 zimefutiwa ushuru ikiwamo kusafirisha mazao yasiyozidi tani moja hivyo kuwataka wahusika akiwamo Chalamila kushughulika na wanaoendelea kuwatoza.

Kiwanda cha nyama

Alisema kuna kiwanda cha nyama kilichojengwa tangu enzi za Mwalimu Nyerere kikiwa na heka 9,000 hivyo kishughulikiwe ikiwamo kutafuta mwekezaji mpya ili kukiendeleza.

ATOA ENEO LA MACHINGA

Alisema tayari kuna vitambulisho vilivyotolewa ili kuwawezesha kufanya biashara kwa uhuru na kwamba vile vya mwanzo vilimalizika na kuongezwa vingine 80,000.

Aliwataka wafanyabiashara wadogo wasikubali kutumiwa na wafanyabiashara wakubwa ili kukwepa kodi.

“Naibu Spika ameeleza kuwa vijana zaidi ya laki tatu, maeneo yao ya biashara yaliungua moto, moto ni kawaida Mbeya inawezekana makusudi au bahati mbaya na mimi nimekuwa nawatetea waendelee kukaa mjini.

Miji hii ni ya Watanzania wote ikiwamo hao machinga, ninatambua changamoto za machinga wa Mbeya na Mkuu wa Mkoa amekuwa akielezea akiwamo Naibu Spika na Mbunge wa Viti Maalumu.

“Ukishaombwa hivyo na wote, kwa sababu ninyi wananchi wa Mbeya wakiwamo wamachinga mlinifanya kiongozi, mnahitaji mahali pa biashara na ambako ni mjini, wanaotaka kufanya nane nane wakafanye na hilo eneo la Uwanja wa Ndege wa Mbeya lina hekta zaidi ya tano, uongozi wa mkoa uko hapa, utakwenda kumweleza Waziri wa Ujenzi tunabadili matumizi hapa hapa, hilo eneo mliandae vizuri ndilo litakuwa eneo la wamachinga wa Mbeya,” alisema.

Alitaka eneo hilo kuwe na kituo cha daladala au mabasi ya mikoani na iwapo nafasi itabaki kuwe na masoko ikiwamo la dhahabu kama Geita.

Alisema wakiwa huko wakivaa vitambulisho wasidaiwe fedha yoyote na wapatiwe nafasi ya kufanya biashara.

Aliwataka wafanyabiashara kufanyia maeneo sahihi na si popote, lakini pia kila uongozi wa mkoa utengeneze mazingira ya kuwafanya wabaki mjini.

UCHUMI

Alisema hatua mbalimbali zinazochukuliwa zimesaidia uchumi wa nchi kukua kutoka asilimia saba mwaka jana na mwaka huu na iwapo mambo yakienda vyema utakuwa kwa asilimia 7.1 na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tano Afrika ambazo unakuwa kwa kasi.

Alisema mfumuko wa bei umedhibitiwa kutoka wastani wa asilimia tatu kwa mwaka jana ikiwa ni kiwango kidogo kutokea kwa zaidi ya miaka 40.

Pia alisema mwaka jana nchi iliongoza kwa Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji wa dola bilioni 1.8 za Marekani na kasi ya uwezo wa viwanda inaendelea vyema zaidi ya viwanda 3,000 vimejengwa.

Aliwataka wana CCM Mkoa wa Mbeya kuacha kupigana vita na kumtaka Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya kujenga umoja kwa wanachama.

Katika hatua nyingine, alifungua jengo la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unaoongozwa na Mwenyekiti wake wa bodi, Spika mstaafu, Anna Makinda, ambalo tayari limepata wapangaji asilimia 91.

Alisema kujenga majengo ni vyema lakini alimtaka Makinda kujenga viwanda vya dawa vitakavyosaidia vizazi hata vizazi.

Alisema walio na bima ameambiwa hawafiki milioni 14, hivyo ni vyema kujikita kuendeleza ili kila mmoja apate.

MWANAMKE

Katika mkutano huo aliibuka mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Swaumu Swatiman, aliyedai kuwa mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka minne alilawitiwa na mtu mwenye miaka 53.

Mama huyo ambaye alikabidhiwa Sh milioni moja, alisema alitembea ofisi mbalimbali za Serikali ikiwamo kwa Jaji Mkuu, IGP ili kufanikisha kesi hiyo lakini ilikuwa bado inapigwa danadana.

Swaumu ambaye alisema alihama na familia yake kutoka Tunduma na kuja Mbeya, alimweleza Rais kuwa askari walikuwa wakimweka ndani.

Rais aliwataka RPC wa Songwe kushughulikia suala hilo pamoja na kumpatia ulinzi mhusika.

SUGU

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu, akiwa katika mkutano huo wa Rais, alisema anamuunga mkono na anampenda Magufuli.

Alisema Mbeya inapata asilimia 60 ya maji na wataalamu walitaka yatoke Mto Kiwila lakini zinahitajika Sh bilioni 70.

Alisema maji hayo yakiletwa yatasaidia kufika maeneo mbalimbali hadi Mbalizi hata Tunduma.

Alisema hawapingi kila kitu lakini vipo vingi wanavyomuunga mkono ikiwamo suala la wamachinga.

“Mwisho kwa unyenyekevu, hata tulivyokaa hapa kuna mgawanyiko. Watu wetu wa Chadema wapo hapa lakini wamekaa nyuma na wewe umesema hutaki vyama na mimi nimekushika, nakufuata na mimi ni kati ya watu wanaokuunga mkono bila kuhama chama, nitaendelea kukuunga mkono hadi mwisho. Kwa kuwa mimi ni rafiki yako na kijana wako.

“Wasikwambie mambo haya Rais, eti matusi, sijui hatukupendi, sio kweli. Walikuwa wanasema sijui ukiwa Mbeya, sijui jana (juzi) kuna mwenyekiti wangu amekamatwa kwamba anapanga wafanye fujo Mbeya, hakiwezekani hicho kitu na wewe umeona.

Hakiwezekani, watu na akili zao wapange kumfanyia fujo Rais. Nakuomba sana mimi ni kijana wako najitolea ikikupendeza niwe chaneli ya mazungumzo ili kuondoa haya mafundofundo ya kisiasa kwa levo ya Mbeya hata kitaifa ikiwezekana,” alisema Sugu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,908FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles