23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Lukuvi atatua mgogoro wa wafugaji, mwekezaji

Na MWANDISHI WETU-MONDULI

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi,  amemaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu baina ya wananchi wa vijiji vya Lengiloriti na Naalarami vilivyopo wilayani Monduli mkoani Arusha na wawekezaji wa mashamba yanayomilikiwa na Tanfoam na Sluis kwa kuamua kumega sehemu za mashamba na kuwapatia wananchi wa vijiji hivyo.

Lukuvi alifikia uamuzi huo baada ya kukutana na pande zote mbili  juzi wilayani humo na kujadiliana kwa kina kwa takriban saa tano kwa lengo la kupata suluhu ya mgogoro huo ambao umeleta sintofahamu kati ya wananchi wa vijiji hivyo na wawekezaji wa mashamba.

Katika makubaliano hayo, iliamuliwa ekari kati ya 850 hadi 900 zimegwe kutoka kwa mwekezaji Tanfoam na kugawiwa kwa Kijiji cha Lengiloriti  wilayani Monduli  kutoka shamba namba 44 lenye ukubwa wa  ekari 3098.

Aidha, upande wa mwekezaji Sluis, jumla ya ekari 2000 za mwekezaji zimetolewa kwa Kijiji cha Naaralami, Nafco, Lokisari na Tukusi ambapo sasa mwekezaji atabaki na ekari 2217 badala ya 4,217 alizokuwa nazo awali.

Kwa mujibu wa Lukuvi, ardhi iliyomegwa na kurudishwa katika vijiji hivyo itakuwa chini ya mamlaka ya kijiji ambacho ndicho kitakuwa na jukumu la kuigawa upya kwa wananchi wa vijiji husika na baadaye kupangwa matumizi bora ya ardhi.

Akizungumzia Kijiji cha Lengiloriti, Waziri wa Ardhi aliwataka wananchi wenye maboma yaliyokuwa ndani ya eneo la shamba la mwekezaji Tanfoam kuhamia eneo jipya walilotengewa katika kipindi cha miezi mitatu ili kupisha mwekezaji kuendelea na shughuli za kilimo na kutotekelezwa kwa aina yoyote agizo hilo kutaifanya Serikali kuchukua hatua.

Pamoja na hali hiyo, aliagiza kuanzia wiki hii timu ya upimaji ardhi mkoani Arusha iende ktika eneo hilo kwa ajili ya kuweka mipaka/alama za kudumu ili kuepuka uvamizi mwingine unaoweza kutokea na kuagiza wawekezaji na wananchi wa vijiji vilivyopatiwa ekari hizo kuchangia fedha kwa ajili ya upimaji, ambapo mwekezaji na wananchi walikubali kutoa milioni tano kwa ajili ya upimaji.

Kuhusu mgogoro wa mwekezaji Sluis, Lukuvi alisema mwekezaji huyo amekubali  kutoa ekari 520 kwa Kijiji cha Naaralami pamoja na ekari 300 kwa ajili ya kupitishia mifugo ya wananchi wa kijiji hicho, huku ekari 513 zikitolewa kwa Nafco, 366 kwa Lokisari na ekari 301 kwa Kijiji cha Tukusi.

Lukuvi alisema Serikali inawaheshimu sana wawekezaji wa sekta ya ardhi kwa kuwa wanalipa kodi inayosaidia utoaji wa huduma za jamii, huku wananchi nao wakipata ajira na kusisisitiza kuwa wawekezaji wanaomiliki mashamba kisheria, Serikali itawalinda na kuonya baadhi ya viongozi wa vijiji kujigawia maeneo bila ya kushirikisha wananchi wa vijiji husika. “Nimekuja kusuluhisha mgogoro  na si kunyang’anya wawekezaji mashamba, wawekezaji wamekubali kupunguza mashamba yao na hayo mashamba si mali ya wananchi wanaoishi katika maboma yaliyohamishwa, bali ni mali ya kijiji ambacho kitakuwa na jukumu la kugawa maeneo hayo,” alisema Lukuvi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles