24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Propaganda zinavyoyumbisha, kuinua wapigakura

Mwalimu Nyerere
Mwalimu Nyerere

Na FRANK BANKA,

IMEBAKI miaka minne tu tuingie kwenye uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na udiwani. Uchaguzi mkuu utafanyika Oktoba 25, mwaka 2020. Kabla ya uchaguzi mkuu kutakuwa na mwingine wa serikali za mitaa ifikapo mwaka 2019, ambapo vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu vitakuwa vinashindana kupata ushindi na kuongoza serikali za mitaa.

Uchaguzi wa mwaka jana tumeona mpambano na msisimko mkubwa miongoni mwa wapigakura, lakini jambo moja kubwa ambalo linatumiwa wakati wa uchaguzi ni propaganda.

Tunafahamu kila uchaguzi au ndani ya vyama vya siasa zipo idara zinazohusika na masuala ya propaganda.  Kuna propaganda nzuri ambazo zinakuwa tija katika jamii. Kuna propaganda mbaya ambazo zinaeneza uwongo dhidi ya kundi fulani ili kuvutia wapigakura au wasikilizaji.

Propaganda ni msingi mkubwa wa vyama vya siasa, makampuni ya biashara, michezo, wanasiasa, watu binafsi na makundi mbalimbali ya kijamii. Kimsingi uhalisi wake inategemeana na madhumuni ya matumizi ya propaganda husika kwa wakati, mahali na walengwa.

Vilevile propaganda hutumiwa na utawala wowote kuvuta usikivu au kutengeneza ajenda ya kuzungumzwa. Hata katika utawala wa awamu ya tano hapa nchini tumeshuhudia mara kadhaa matumizi ya propaganda ili kuvuta hadhira ambazo zimeinufaisha katika siasa za ndani na nje.

Aidha, propaganda hutumiwa na vyama vya upinzani hapa nchini kwa lengo la kuwavutia wananchi na watu mbalimbali. Mifano ni mingi, ikiwemo Operesheni Ukuta, kususia bunge, kupambana na Naibu Spika, pamoja na kuwatumia viongozi wa dini kama nyenzo ya usuluhishi wa mizozo ya kisiasa.

Propaganda ni zao la siasa za chama cha Nazi chini ya aliyekuwa waziri mtiifu wa propaganda, Dk. Joseph Goebbles. Kuongoza kwa kiasi kikubwa ni mafanikio ya habari kuenea za kuzungumzia utawala ulioko madarakani kwa mazuri, lakini wananchi kuishi na kuimba itikadi za chama husika zinazosimamiwa na kiongozi aliyeko madarakani.

Maisha ya Adolf  Hitler yasingewezekana bila akili kubwa ya Joseph Goebbles. Binafsi napenda kumwita Mbwa Mwitu mwenye meno ya Kiboko.

Joseph Goebbels alikuwa waziri wa propaganda nchini Ujerumani chini ya serikali katili ya Nazi, iliyoongozwa na Adolf Hitler. Goebbels alikuwa stadi wa kunena na mwerevu wa kupumbaza umma.

HISTORIA YA PROPAGANDA

Neno ‘Propaganda’ ni la lugha ya Kiingereza, ambalo linatokana na jina la Kilatini la kikundi cha makadinali wa Kanisa Katoliki, Congregatio de Propaganda Fide (Kundi la Kueneza Imani).

Kamati hiyo iliyoitwa Propaganda kwa ufupi ilianzishwa na Papa Gregory wa Kumi na Tano mwaka wa 1622 ili kusimamia wamishonari. Hatua kwa hatua, neno la Kiingereza “propaganda” likaja kumaanisha jitihada yoyote ya kueneza itikadi fulani.

Propaganda na kueneza habari ndio kama damu na maji, vyote vinakwenda pamoja lakini dhana ya uenezaji habari haikuanza katika karne ya 17. Tokea nyakati za kale, watu wametumia njia zozote zilizopo kueneza mawazo au kuboresha umashuhuri na uwezo.

Kwa mfano, waeneza habari wametumia sanaa kujipambanua tangu siku za mafarao wa Misri. Wafalme hao walijenga piramidi zao ili kuonyesha waziwazi tawala zao, huu pia ni mfano wa propaganda.

Jicho langu kisiasa na propaganda naona kizazi chetu leo kina watu wachache wenye roho ya Dk Joseph Goebbles, mtu ambaye kama angekufa kabla ya vuguvugu la vita ya pili au kama angefuata ushauri wa mama yake kuwa mchungaji wa Kanisa, basi sidhani kama chama cha NAZI kingepata umaarufu duniani, lakini pia ingekuwa vigumu Wajerumani kumtukuza Adolf Hitler.

Hitler aligundua umuhimu wa Dk. Goebbles, ndiyo maana maisha yake yote hakuhitaji gwiji huyo wa propaganda awe mbali na macho yake.

KUFANIKIWA KISIASA KWA KUISHI KWA PROPAGANDA 

Utawala wowote ili ufanikiwe unapitia changamoto nyingi, mfano kwenye ulimwengu wa sasa kisiasa inabidi kiongozi aweze kushinda vitu viwili vikuu; mosi ni vyama na siasa na pili ni ushawishi wa mataifa ya nje.

VYAMA NA SIASA 

Siasa ni ushindani wa mawazo kati ya kundi moja au mawili au zaidi zenye mrengo mmoja wa kuleta changamoto za kimaendeleo. Kwenye propaganda mtu kama Goebbles ana  nafasi kubwa kuenda sambamba na vyama ndani ya nchi na mwelekeo wa siasa.

Hitler aliweza kufanikiwa kwa msaada wa bingwa wa propaganda, Goebbles, kwa kuweza kupanga nini watu wasikie na nini watu wasisikie. Hivi ndiyo namna unavyoweza kwenda sawa na matukio ya kisiasa ndani ya nchi.

Propaganda ndiyo inayotengeneza adui wa kitaifa, mfano zile nyimbo za nduli Idd Amin na roho ya Idd Amin ilivyokuwa inapambanuliwa ndani ya nchi, mfano Idd anakula nyama za watu, Idd anabaka watu, Idd anatupa vilema kwenye mto waliwe na mamba.

Pia propaganda kama ina mtu makini inaweza ikawa na msaada sana kwa kizazi chetu cha sasa, ambacho kinafanya siasa za harakati ambazo kila mmoja anapinga jambo la mwenzake linalohusu utaifa.

Vyama vimetugawa, lakini propaganda nzuri zinaweza kuwarudisha watu pamoja na kuimba wimbo mmoja wa Utanzania, tofauti na ilivyo sasa ndani ya nchi siasa za vyama zimetugawa kila mmoja anaimba wimbo wake.

Kwenye uongozi wowote duniani, nje ya tofauti ya siasa zetu inabidi kuwe na jambo linaloonyesha sisi wote ni Watanzania.  Hivi sasa Utanzania unakuja kwenye maafa mbalimbali kama tetemeko la hivi karibuni Kagera au ajali mbaya ya vyombo vya usafiri au mafuriko.

Nchi inahitaji kuzalisha akina Goebbles wengi ambao watakuwa radhi kufia utaifa hata kwa kumeza uongo kuwa ukweli, maana kuna kauli inasema uongo ukizungumzwa kwa muda mrefu unakuwa ukweli.

Siasa maana yake ni propaganda, ila leo tunafanya siasa zinazokosa kina, watu kama Goebbles ambao watakuwa radhi kusimama kwa ajili ya taifa lao hata kwa kutoa tone la mwisho la damu.

Propaganda inabidi itengeneze muunganiko kati ya mwananchi, serikali na kiongozi ili kwa pamoja kua na kauli moja ya maendeleo.

USHAWISHI WA MATAIFA YA NJE 

Propaganda za Dk. Joseph Goebbles zilimsaidia kupata watu walioamini na kuungana na mawazo ya chama cha NAZI.  Bila nguli huyo kungekuwa na mataifa mengi ambayo yangempinga Hitler pale alipowaua Waisraeli zaidi ya milioni. Kazi ya Goebbles haikuishia hapo, propaganda ilisaidia Ujerumani kupata washiriki wenzake kutoka mataifa ya nje walioshirikiana naye katika vita ya pili ya dunia mwaka 1945.

Hapa nchini hatuna mtu atakayetueleza ni nani bora kwetu na nani si bora kwetu, lakini pia hatujafundishwa jinsi ushawishi wa mataifa ya nje unavyokwamisha maendeleo ya nchi.

Ili kujua haya, nchi inahitaji mtu ambaye anapaswa kutuambia jinsi dunia inavyojiendesha kisiasa. Mfano leo unapata ARV bure, ila inawezekana kuna wagonjwa wachache wa ukimwi ambao wanajua kwanini dawa hizo zinapatikana bure.

Nchi ilipaswa ipate mtu atakayetuambia Watanzania ni nini maana ya misaada yenye masharti magumu. Nchi leo ilibidi ipate mtu wa kutuambia ni kwanini vita ya mashoga inatushinda.

Kila chenye uhai lazima kionje mauti, leo Dk. Goebbles na msimamo wake yuko ardhini na roho yake inajibu matokeo ya alichofanya duniani kama tunavyoamini kwenye dini zetu, ila leo natamani kama roho yake ingeishi miongoni mwetu.

Tukiangalia matumizi ya propaganda miongoni mwa vyama vya siasa nchini yanavyowagawa Watanzania siku hadi siku, napata hofu na kujiuliza, nani atatuimbisha tena nyimbo za utaifa?

Mwalimu Nyerere aliweza kazi zote, alikuwa kiongozi, lakini alikuwa waziri wa propaganda katika utawala wake. Kwahiyo, tumeona propaganda inayumbisha au kuinua nchi kwa wakati mmoja.

Maoni: 0719 889 308

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles