20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Trump halijui dubwana la IS?

Donald Trump
Donald Trump

Na Dennis Luambano, Dar es Salaam

RAIS mteule wa Marekani, Donald Trump, ametoa mwelekeo wa namna atakavyoiendesha nchi hiyo ndani ya siku 100 za kwanza za utawala wake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la CCN, mwelekeo huo alioutoa New York juzi, umeashiria namna atakavyolegeza baadhi ya misimamo yake, ukiwamo wa kufutilia mbali Mkataba wa Paris, unaohusu mabadiliko ya tabianchi, tofauti na alivyoahidi wakati wa kampeni za urais kabla hajachaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo, Novemba 8, mwaka huu.

Licha ya kulegeza msimamo wake katika baadhi ya mambo, lakini ahadi yake ya kuwashughulikia magaidi wa Dola ya Kiislamu (IS) iko palepale.

Ndiyo, kama alivyoahidi wakati wa kampeni zake kwamba yeye ndiye mwenye msuli na stamina ya kuwatwanga mabomu IS kuliko aliyekuwa mpinzani wake wakati wa uchaguzi huo, Hillary Clinton.

Kwamba anaamini njia pekee ya kuwatokomeza IS ni kuwapiga kwa mabomu na anasisitiza kuwa hakuna mwingine mwenye uwezo wa kuchukua uamuzi mzito kama huo zaidi yake.

Pia atawadhoofisha IS kwa kulipua vyanzo vyao vya mafuta. Wakati akiwa na msimamo huo kuhusu IS, lakini anasema dunia ingekuwa bora kama aliyekuwa Rais wa Irak, Saddam Hussein na aliyekuwa Kiongozi wa Libya, Kanali Mummar Gaddafi, wangekuwa madarakani.

Trump anaamini kuwa ili kutatua matatizo yanayoikabili dunia sasa hivi ingekuwa jambo jema zaidi kama Saddam na Gaddafi wangelikuwapo madarakani.

Kimsingi, imani hiyo ya Trump inakinzana na watangulizi wake, Rais Barrack Obama aliyeruhusu majeshi kumng’oa Gadaffi na Rais Mstaafu George W. Bush, aliyeruhusu majeshi hayo hayo kumng’oa Saddam, hasa ikizingatiwa kuwa sasa hivi ngome kuu za IS ziko Irak na Libya, huku kila siku wakiendelea kufanya mashambulizi katika nchi za Mashariki ya Kati, ikiwamo Syria.

Pamoja na msimamo wake kukinzana na watangulizi wake, lakini pengine Trump anajifanya hajui mizizi ya dubwana la IS, kwamba ni kama mradi wa nchi hiyo kwa kushirikiana na kampuni kubwa za kigeni za kutengeneza silaha za kivita.

Kwamba IS imeumbwa ili eneo la Mashariki ya Kati lionekane ni hatari kwa Serikali zilizopo madarakani katika maeneo hayo na kwa kuwa kuna utajiri mkubwa wa mafuta, ina maana biashara ya silaha za kukabiliana nao itaendelea kufanyika.

Kama hivyo ndivyo, ina maana ule msimamo wake kwamba atazifurumusha kampuni zinazoinyonya Marekani kutokana na migogoro ya Mashariki ya Kati ni kama vile hatafanikiwa kuusimamia, kwa sababu kitendo cha kutaka kuiangamiza IS ndivyo kampuni hizo zitakavyoendelea kujinufaisha. Kwa sababu kampuni kubwa za kuuza silaha nyingi kati ya hizo zikiwa za Wamarekani na Wazeyuni zitawafadhili au zitawauzia silaha kwa pande zote mbili, kwa maana ya IS na Serikali zinazokabiliana nao.

Kwa hiyo wanachokifanya IS na kinachoendelea Mashariki ya Kati ni zaidi ya ugaidi, kwa sababu kuna biashara kubwa ya kubadilisha mafuta kwa silaha.

Mchoro wa vikaragosi ukionyesha namna IS inavyotekeleza vitendo vyake vya kigaidi.
Mchoro wa vikaragosi ukionyesha namna IS inavyotekeleza vitendo vyake vya kigaidi.

Ndiyo! Licha ya watu kupoteza maisha kutokana na matendo ya IS, lakini nyuma ya pazia ni kwamba ugaidi wao ni wa ‘kiwango cha lami’, kwa maana umeboreshwa na biashara inayofanyika, hasa kwa kuzingatia kuwa ugaidi si imani moja kwa moja kama ukilinganisha matukio mengine ya kigaidi yaliyotokea siku za nyuma katika maeneo mbalimbali.

Mathalani, kitendo cha majeshi washirika yakiongozwa na Marekani kuivamia Irak mwaka 2001 na kuupiga utawala wa Saddam kisha wakamnyonga Desemba, 2006, nao ni ugaidi uliohalalishwa.

Pia kitendo cha majeshi hayo hayo cha kuivamia Libya kisha Oktoba, 2011 wakamuua Gaddafi nao ni ugaidi.

Kwa sababu licha ya kuwaua viongozi hao kwa visingizio vya kipuuzi ambavyo hadi leo havijathibitishwa, mathalani Saddam walisema ana silaha za maangamizi ya halaiki, Gaddafi walidai ni dikteta anayeminya demokrasia nchini mwake, waliharibu mali na miundombinu, huku kampuni za nchi washirika zikazawadiwa kandarasi za kuzijenga upya kwa malipo ya kunyonya malighafi ya mafuta yanayopatikana kwa wingi katika nchi hizo.

Kwa hiyo wakati Trump akishikilia msimamo wake wa kuiangamiza IS, anapaswa kufahamu namna nchi yake inavyonufaika na migogoro ya Mashariki ya Kati kama nilivyotoa mfano wa Libya na Irak, kwamba si ugaidi tu kama dunia inavyoaminishwa, bali kuna biashara kubwa inafanyika nyuma ya pazia.

Pia, si biashara tu, bali Marekani inajiingiza katika migogoro ya namna hiyo tangu enzi na enzi ili kulinda masilahi yake katika majukwaa ya kimataifa.

Kuthibitisha hoja yangu, tutafakari uchambuzi wa Aubrey Bailey aliowahi kuutoa mwaka jana, akisema kinachotokea katika nchi za Mashariki ya Kati kisiishangaze dunia, kwa sababu Marekani inaisaidia Irak katika vita ya kuwaondoa IS.

Kwamba Marekani hiyo hiyo haiipendi IS, lakini inaupenda utawala wa Saudi Arabia unaoipenda IS. Pia haimpendi Rais wa Syria, Bashar Assad na wanafurahia mapigano yanayotaka kumng’oa madarakani yanayofanywa na IS, ingawa hawaipendi. Alisema Marekani haiupendi utawala wa Iran, ingawaje unaisaidia Irak kuwaangamiza IS.

Tafsiri ya uchambuzi wa Bailey ni kwamba, baadhi ya marafiki wa Marekani wanawaunga mkono maadui zake, baadhi ya maadui zake ni marafiki zao kwa namna moja au nyingine, kwa kuwa baadhi yao wanapigana na maadui zake wengine.

Aidha, hawataki maadui zake wawapige maadui zake wengine kwa sababu wakishinda watakuwa maadui hatari zaidi kwa Marekani kwa kuwa ilijiingiza katika vita ya kupambana na ugaidi katika nchi ambazo awali hazikuwa na magaidi, bali ilipoingia tu ndipo ugaidi nao ukaibuka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles