25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

RC Makonda wewe si malaika kuna siku utakosea tu

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

NA JOHN MADUHU, MWANZA

NILIWAHI kutoa angalizo katika mojawapo ya makala za Gumzo la Rock City kwa Rais John Magufuli, kuhusu mwenendo wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Nilitoa angalizo hilo baada ya mkuu huyo kutamka kupitia vyombo vya habari kuwa hamtaki aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe (marehemu), kwa madai kuwa amehusika kuhujumu mapato ya kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo.

Kauli hiyo tata aliitoa wakati wa uzinduzi wa daraja la Kigamboni mwaka huu, na kusababisha Rais Magufuli kuamua kumsimamisha kazi Kabwe, ili kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwake na RC Makonda.

Katika angalizo hilo, nilielezea namna RC Makonda pamoja na viongozi wa aina yake wanavyoweza kutumia mwanya wa kuwahujumu viongozi wanaofanya nao kazi kwa viongozi wa juu katika mikutano ya hadhara ili kutimiza malengo yao au kuficha udhaifu wao.

Nilieleza kuwa Rais Magufuli anapaswa kuwa makini na viongozi wa aina ya Makonda, ambao ili waonekane wanafanya kazi lazima wawadhalilishe viongozi walio chini yao, kwa lugha nyepesi ni kutaka kusafiria nyota zao ili kujijengea uhalali wa kuwepo madarakani.

Tumeshuhudia tena namna alivyotaka kusafiria nyota ya Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina wa Polisi, Simon Sirro, baada ya kumtuhumu kuwa alipokea fedha na kuruhusu matumizi ya shisha.

RC Makonda alimweleza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuwa alikataa kuhongwa Sh milioni 50 kutoka kwa wafanyabiashara kumi, hivyo kutokana na kukithiri kwa matumizi ya shisha licha ya kupigwa marufuku huenda kulitokana na fedha kupenyezwa kwa Kamanda Sirro pamoja na wasaidizi wake.

Makonda pia alitaka kumvuruga Waziri Mkuu Majaliwa baada ya kumchomekea kuwa kuna taarifa kuwa ameruhusu matumizi ya shisha, jambo ambalo Waziri Mkuu aling’aka na kumtaka RC Makonda asimamie maagizo ya Serikali, vinginevyo atatumbuliwa.

Baada ya kupita kwa sakata hilo ambalo tayari vyombo vya ulinzi na usalama vinachunguza ili kupata ukweli wake, mkuu huyo wa mkoa ameibuka na kauli nyingine tata baada ya kueleza kuwa watumishi zaidi ya 100 waliopo katika ofisi yake ni mzigo na wanaofanya kazi hawazidi wanne.

Mengi yameandikwa katika magazeti pamoja na mitandao ya kijamii kuhusu matukio hayo mawili yanayomhusu Makonda, Gumzo la Rock City linapenda kumueleza RC Makonda kuwa nafasi za kisiasa zina muda wake, si kazi za kudumu kama zilivyo nyingine.

Historia kuhusu RC Makonda inaonyesha ni kijana ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitumiwa na wanasiasa kutoa kauli zenye kulenga kuwadhalilisha na kujitafutia sifa katika jamii pasipo kujua madhara ya siasa anazofanya.

Kupanda kwake vyeo hadi kufikia nafasi aliyonayo hakutokani na uwezo alio nao kielimu au uzoefu katika utumishi wa umma au uzoefu katika nafasi za kisiasa, ni kutokana na makundi ya kutafuta uongozi wa nchi ndiyo yaliyomwibua si vinginevyo.

Tuhuma za rushwa alizozitoa mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa dhidi ya Kamishina Sirro hazikupaswa kutolewa na kiongozi mwenye wadhifa wa ukuu wa mkoa, ila alifanya hivyo kwa lengo la kutaka kuficha udhaifu wa uongozi alio nao.

Kwa bahati nzuri nimewahi kufanya kazi kwa karibu na Kamishina Sirro akiwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Sirro si mtu wa rushwa na kama angelikuwa ni mtu wa rushwa asingekuwa katika utumishi wa Jeshi la Polisi hadi leo hii.

Kamishina Sirro, ambaye naweza kumwelezea ni mmoja kati ya maofisa wa polisi wasio na dharau, majivuno wala kujikweza, ni mtu anayeweza kufikika kirahisi na mtu yeyote, binafsi nimewahi mara nyingi kukaa naye akiwa Mwanza katika mazingira ya nje ya kazi na kubadilishana mawazo kwa lengo la kujenga nchi yetu.

Kuna mambo makubwa matatu ambayo Kamishina Sirro aliyafanya Mwanza na kama angelikuwa mtu wa tamaa angepata fedha nyingi na leo hii angelikuwa ni bilionea na si mtu wa kuchafuliwa kwa Sh milioni 50 ambazo Makonda anadai kuwa huenda Kamanda Sirro alizipokea kwa wafanyabiashara wa shisha.

Akiwa kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mwanza mwaka 2010, huku Lawrence Masha akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kamanda Sirro alikataa hila zote zilizotaka kufanywa na wanasiasa ili kupindisha matokeo ya ubunge wa Jimbo la Nyamagana.

Sirro alilazimika kwenda makao makuu ya Jiji la Mwanza na kumtaka msimamizi wa uchaguzi kutangaza matokeo haraka ili kuepusha jiji hilo kutumbukia katika machafuko, ieleweke kuwa wakati huo Masha alikuwa ni bosi wa Sirro.

Sirro angeliweza kutii amri ya Masha na kusimamia kutangaza matokeo ambayo yangemweka Masha madarakani, alisimamia haki pasipo woga wa aina yoyote na kama ni fedha angeliweza kuzipata wakati huo, kilichotokea kumhusu Sirro kinaeleweka baada ya uchaguzi.

Sirro akiwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza aliingia katika majaribu baada ya kutokea kwa mauaji ya aliyekuwa Katibu wa CCM wa Kata ya Isamilo, marehemu Bahati Stephano.

Katibu huyo ilidaiwa kuuawa kutokana na maelekezo ya aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, Leonard Bihondo, Kamanda Sirro aliongoza operesheni ya kumsaka meya huyo na kumtia mikononi.

Kwa fedha alizokuwa nazo Bihondo asingeshindwa kumhonga Kamanda Sirro, nakumbuka namna Sirro alivyokuwa akitembea na baadhi ya vielelezo kuhusu kesi hiyo na kuna siku alinitania kuwa wakati mwingine hata akiingia bafuni kuoga vielelezo hivyo alikuwa akiingia navyo akiogopa kuhujumiwa.

Mtego mwingine uliomuimarisha Sirro kikazi ni kesi ya tuhuma za kutaka kuuawa kwa Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni, zilizoeleza kuandaliwa na Mwenyekiti wa sasa wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Titus Kamani.

Kiongozi huyo alisimama kidete katika kusimamia haki za pande zote mbili, hatimaye suala hilo likafikishwa mahakamani, hakukuwa na tuhuma zozote za rushwa ili apindishe haki.

Gumzo la Rock City linapenda kutoa ushauri wa bure kwa RC Makonda kukaa na kujitathimini upya kuhusu mwenendo wake kisiasa, asiendelee kutumia staili ile ile ya kuchafua wenzake ili ajinufaishe kisiasa.

Dunia imebadilika sana, Makonda asidhani kwamba yeye ni msafi sana, maana zipo tuhuma lukuki zinatolewa kuhusu mwenendo wake wa kiuongozi tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo.

Yapo madai kuwa anahusika katika mtandao wa wafanyabiashara wasio waaminifu, ambao wanamfadhili katika shughuli mbalimbali zinazohusu miradi.

Kuna msemo usemao si kila king’aacho ni dhahabu, RC Makonda huenda baadhi ya viongozi wanakuona kuwa wewe ni dhahabu lakini wana Dar es Salaam ndio wenye majibu sahihi.

Na katika dunia hii wapo watu wanajiona ni miungu watu na wengine kama Makonda wanajiona ni malaika kwa maana kuwa hawawezi kukosea ama kuteleza. Ninachoweza kusema RC Makonda, wewe si malaika, ipo siku wembe unaowanyolea wenzako nawe utakunyoa.

Naomba kuwasilisha.

[email protected]

0767642602

0784 642602

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles