24.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

PROFESA KABUDI ABANWA BUNGENI

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA


WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi amejikuta katika mgumu baada ya baadhi ya wabunge kudai amenukuu vibaya moja ya aya za Quran.

Prof. Kabudi aliombewa mwongozo na wabunge wakimshutumu kwa kauli yake wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Konde Khatibu Said Haji (CUF).

Mbunge huyo alitaka kujua ni nani mwenye Mamlaka kikatiba ya kugawa mipaka kati ya Rais wa Tanzania  na yule wa Zanzibar.

Akijibu swali hilo, Prof. Kabudi alisema Rais wa Tanzania ndiye mwenye Mamlaka kikatiba katika masuala yanayohusu muungano.

Mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim Seleman (CUF), aliomba mwongozo wa kiti huku akitaka Prof.  Kabudi  kuwaomba msamaha Waislamu wote kwa kusema uongo bungeni kuwa kitabu cha Quran kina aya mbili zinazokinzana.

“Mwenyekiti (Mwenyekiti wa Bunge, Musa Zungu)  Waziri wakati akijibu swali la Mheshimiwa , Khatibu alituchanganya sana aliposema iwapo aya mbili za Quran zitagongana. Je anao ushahidi kuwa zipo aya mbili katika Quraan ambazo zimegongana,”  alihoji mbunge huyo.

Aliomba mwongozo akitaka apewe majibu kama mtu yoyote au Waziri kama anaruhusiwa kusema uongo bungeni.

Kwa upande wake, Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji, (CUF)  alimtaka Waziri Prof. Kabudi kuomba msamaha kwa Waislamu na kukiri kuwa yeye ni Profesa wa sheria na sio wa Quraan

“Mimi narudia mle mle mheshimiwa Kabudi alipojibu swali langu alinipointi kuwa mimi ninajua aya mbili ndani ya Quraan zinapogongana jambo ambalo mimi nikiwa kama muislamu siwezi kulikubali kwani nitakuwa nimeukosea uislamu na nimemkosea Mungu na nitakuwa nimejitoa katika uislamu wangu.

Akijibu mwongozo huo, Profesa Kabudi aliwaomba radhi Waislamu wote ambapo alidai kuwa anaheshimu dini zote.

“Kwa hiyo naomba kabisa kwa Waislamu wote wajue kwamba nawaomba radhi.

“Na kama nimesema hivyo naomba mnisikilize…… naomba mnisikilize  sentensi hiyo ifutwe kwenye Hansard si kwa sababu ninyi mmesema bali ni kwa dhamira yangu ninaheshimu dini zote

“Naheshimu kwa dhati dini zote ikiwa ni dini ya kiislamu mimi ninaye mjomba mwislamu, Sheihe  Mustapha Mwendi  pia ninayo heshima kubwa kwa dini ya kiislamu kwani  mwaka 1961 na 1962 nilisoma madrasa katika msikiti wa Mlelwa pale Kilimatinde Manyoni .

Alisema anayoheshima kubwa kwa Waislamu kwa sababu mke wake Amina ana chimbuko la uislamu lakini pia ana heshimu dini zingine.

“Ninayo heshima kubwa kwa Waislamu kwa sababu ya mke wangu ninayempenda sana Amina ni muislamu na chimbuko lake ni la kiislamu, nauheshimu ukristo nauheshimu uhindu pia wale ambao Mungu amewanyima kujua daraja lao hadi  wanapokaribia mauti,” alisema Waziri Prof. Kabudi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles