31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

SLAA AELEZA SABABU ZA KUTOMPA POLE LISSU

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


BALOZI mteule, Dk. Willibrod Slaa ameeleza sababu za kutompa pole Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka jana.

Dk. Slaa ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, alitoa kauli hiyo jana wakati akihojiwa na kipindi cha 360 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Clouds.

“Suala la Lissu nilishachokozwa sana kwenye mitandao ya kijamii kuwa kwanini sijatoa pole sasa mimi sioni kama pole inalazimishwa.

“Kama binadamu hakuna anayependa mwenzake aumizwe lakini matukio ya kuumiza yametokea mara nyingi sana nchini, sasa mimi si chombo cha dola kunyooshea kidole mtu, sheria inasema kama kuna mtu unamhisi unaenda polisi,” alisema.

Alipoulizwa endapo amekutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “Nitaongea naye vipi na mwenyekiti wa chama wakati mimi nilishaachana na siasa za vyama.”

Alipoulizwa iwapo Mbowe akimpigia atakubali kuonanana naye alisema: “Sasa itategemeana na mazingira ya kuonana.”

Akizungumzia mwenendo wa siasa za upinzani hapa nchini, Dk. Slaa alisema haumfurahishi kwa sababu alishiriki kujenga upinzani lakini haoni chama chenye sera zilizonyooka.

“Mwelekeo wa siasa za upinzani nchini haunifurahishi, baada ya uhuru mwaka 1963 kulikuwa na vyama vingi, baadaye vikaanza kufa vyenyewe kwa sababu vilikatisha tamaa wananchi na baadaye vikaondoka kisheria.
“Sasa naona tena dalili hizo za mwaka 1963 kwa sababu hatuelekei pazuri…wanaongea juu juu lakini mikakati ya utekelezaji hakuna.

“Sioni uimara wa vyama na mkakati wa kutupeleka mbele, wanachofanya wanasubiri kiongozi wa serikali atoe kauli halafu wanakuja na kusema hili sio lakini hakuna sera mbadala,” alisema Dk. Slaa.

Kuhusu kuzuiwa mikutano ya siasa alisema hakubaliani na marufuku ya siasa kwa kuwa Bunge ndiyo ilipitisha lakini pia hakuna hati yoyote iliyotolewa na Rais John Magufuli kwamba mikutano ni marufuku.

“Sikubaliana na taratibu kuwa mikutano imepigwa marufuku, lakini mara kadhaa nimekuwa nahoji hawa wanasiasa wanionyeshe hati yoyote iliyotolewa na rais  kuwa mikutano imepigwa marufuku kwa sababu rais anafanya kazi kwa kufuata sheria,” alisema.

Mbunge huyo wa zamani wa Karatu pia alizungumzia ndoa yake na Josephine Mushumbusi akisema siasa za hapa nchini zilichangia asifunge ndoa lakini alipofika Kanada alifanya hivyo.

“Nimefunga ndoa yangu baada ya kuachana na siasa za Tanzania kwa sababu ilichangia mimi kutofunga ndoa. Nilipofika Kanada haikuchukua muda nikafunga ndoa katika Kanisa Katoliki la karibu na nyumbani kwangu ninakoishi,” alisema.

Dk. Slaa ambaye Novemba 23 mwaka jana aliteuliwa kuwa balozi na Rais Magufuli, aliulizwa endapo amekuja nchini kuapishwa lakini alisema amekuja nchini kushughulikia usajili wa hospitali ya CCBRT ambayo yeye ni mwenyekiti.

“Familia yangu nimeiacha Kanada, wengine wanajua, sikuja kwa sababu ya ubalozi. Mimi ni Mwenyekiti wa CCBRT, ndicho kimenileta na wengine mnafahamu katika nchi yetu mambo mengi yanafanyika,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa mabadiliko ya sheria, CCBRT inatakiwa kujiandikisha upya vinginevyo itafutwa.

Mwanasiasa huyo ambaye kwa sasa anaishi nchini Kanada alitangaza kuachana na siasa kutokana na kutofautiana na chama chake kilipomkea Edward Lowassa aliyehama kutoka CCM na baadaye kupitishwa kuwa mgombea urais kupitia muungano wa Ukawa.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles