23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

SUMAYE AONYA UCHAGUZI KINONDONI

PATRICIA KIMELEMETA


WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), Jeshi la Polisi na wasimamizi wa uchaguzi wa ngazi zote kusimamia haki katika uchaguzi ili waweze kumtangaza mshindi ambaye atashinda kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kinondoni.

Sumaye ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Salum mwalimu alisema iwapo vyombo vya uchaguzi vitaegemea upande mmoja vinaweza kusababisha migongano.

Alisema vyombo hivyo vinapaswa kusimamia haki na wajibu wao ili kuhakikisha uchaguzi huo unamalizika kwa utulivu na amani.

“Tunajua Mkurugenzi wa NEC, wasimamizi wa uchaguzi pamoja na viongozi wa Jeshi la Polisi ni wateule wa Rais, lakini kwa mujibu wa sheria za nchi wana mamlaka ya kusimamia uchaguzi kwa uhuru na haki bila ya kukipendelea chama chochote, jambo ambalo linaweza kupunguza misuguano,’’ alisema Sumaye.

Alisema vyombo hivyo vinapaswa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha kuwa mgombea atakayeshinda amechaguliwa na wananchi wenyewe.

Alisema katika kampeni kumekuwa na matukio mbalimbali ya uvunjifu wa amani yanayojitokeza lakini mpaka sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na kwamba jambo hilo likifumbiwa macho linaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Naye Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila alisema wamemwandikia barua msimamizi wa uchaguzi kuhusu malalamiko yao mbalimbali lakini hawajajibiwa.

Alisema chama hicho kinaendelea na msiamamo wake wa kutokuwa na imani na msimamizi wa uchaguzi kwa sababu anaipendelea CCM.

Alisema kwa mujibu wa taarifa ya NEC ya mwaka 2015, Jimbo la Kinondoni lina jumla ya wapiga kura 262,490, kata 10, vituo vikubwa vya uchaguzi 101 na vituo vidogo vya uchaguzi 611.

“Kuna tetesi tumesikia kuwa NEC imepunguza idadi ya vituo vidogo vya kupigia kura 40 kwa madai kuwa havijakidhi idadi ya wapiga kura, lakini tunaendelea kusubiri taarifa kutoka kwao ila tunachojua sisi ni kwamba wapiga kura wa Kinondoni ni 262,490,’’ alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles