25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi: Dada aliyelalamika kubakwa, kupigwa ni mfungwa anatafutwa

Na JANETH MUSHI-ARUSHA
WAKATI video fupi ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimwonyesha mwanamke akidai kutaka kulawitiwa na bosi wake na kupigwa na polisi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shanna, amesema mwanamke huyo ni Oliver Yassenti na anatafutwa na jeshi hilo ili akatumikie kifungo chake cha mwaka mmoja jela.

Alisema Oliver alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na Mahakama ya Mwanzo Mto wa Mbu, baada ya kukutwa na hatia ya kuiba tairi mbili za gari aina ya Scania zenye thamani ya Sh milioni 2.4.

Shanna alisema Oliver alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na mahakama hiyo akiwa hayupo mahakamani.

Wakati jeshi hilo likisema hivyo, kupitia video zilizosambaa kwenye mitandao mwishoni mwa mwaka jana na kuanza kuzunguka tena hivi karibuni, dada huyo alidai Mkurugenzi wa Mto wa Mbu Service Station, Deepyen Barmeda, alimtaka kimapenzi kinyume na maumbile.

Jana Kamanda Shanna aliliambia gazeti hili kuwa wanamtafuta mtuhumiwa huyo ambaye tangu hukumu yake inasomwa mwishoni mwa mwaka jana hajapatikana.

“Hajapatikana hadi sasa, bado ameeendelea kujificha, tunaendelea kumtafuta, tumeenda sehemu zote walizotueleza ila hayupo, tunaendelea na juhudi za kumtafuta,” alisema Kamanda Shanna.

Alisema jeshi hilo limefanya upelelezi wa kina kuhusiana na malalamiko yaliyotolewa na Oliver ambaye ni mkazi wa Mto wa Mbu, Wilaya ya Monduli.

Kamanda Shanna alisema wamebaini Oliver alikuwa anatuhumiwa kwa kesi ya wizi wa tairi mbili za gari aina ya Scania zenye thamani ya Sh milioni 2.4, wakati akiwa mtumishi katika Kituo cha kuuzia mafuta cha Mto wa Mbu Service Station.

 Alidai jalada la wizi lilifunguliwa Oktoba 24 mwaka jana Kituo cha Polisi Mto wa Mbu na baada ya kesi hiyo kufunguliwa, Jeshi la Polisi lilianza kufanya upelelezi na ilibainika mtuhumiwa aliiba tairi hizo Oktoba 23 mwaka jana ambapo alikodi guta kuzibeba.

“Guta hiyo ilikuwa inaendeshwa na vijana wawili ambao walipeleka matairi hayo nyumbani kwa Debora Josephat eneo la Kona ya Engaruka, kilometa mbili toka eneo la tukio.

“Siku mbili za nyuma (kabla ya tukio) Oliver alimfuata Debora kumuomba hifadhi ya tairi hizo nyumbani kwake na kumhakikishia ni mali yake hali ambayo ilimuondoa shaka Debora akakubaliana naye,” alidai Kamanda Shanna.

Alidai baada ya tukio hilo la wizi, polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne, ambao ni Debora aliyekutwa na tairi hizo nyumbani kwake, vijana wawili waendesha guta; Idd Miraji na Samwel Kimaro, ambao wote kwa pamoja walimtaja Oliver kwamba ndiye aliyewakabidhi tairi hizo ili wapeleke kwa Debora kuhifadhi.

“Baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika, Oktoba 28, 2019 watuhumiwa wote walifikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Mto wa Mbu kwa kosa la wizi,” alisema Kamanda Shanna.

Kamanda Shanna alidai Desemba 12 mwaka jana mahakama hiyo ilimtia hatiani Oliver na kumhukumu kwenda jela miezi 12.

Alisema siku ya hukumu mtuhumiwa hakufika mahakamani na watuhumiwa wengine watatu ambao ni Debora, Idd na Samweli waliachiwa huru baada ya mahakama kubaini hawana hatia.

 “Jeshi la Polisi bado linaendelea kumtafuta mfungwa Oliver kwa ajili ya kwenda kutumikia kifungo baada ya kuhukumiwa na mahakama na pia kwa tuhuma za kusambaza habari za uongo kupitia vyombo vya habari,” alisema Kamanda Shanna.

Alidai malalamiko ya Oliver kwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mto wa Mbu kumtaka kimapenzi, kupigwa na kuombwa rushwa toka kwa Mkaguzi wa polisi Jacob na aliyekuwa Mkurugenzi wake (Deepyen) kumtaka kufanya naye mapenzi kinyume na maumbile, hayana ukweli kwa kuwa alishindwa kuthibitisha na hakuna shahidi yeyote aliyemuunga mkono.

“Upelelezi huo ulibaini kwamba Oliver mara baada ya kuona kesi hiyo (ya wizi) imekaa vibaya kwake, akatumia mbinu hizo za kutafuta huruma kupitia vyombo vya habari ili kuzuia hatua zaidi za mahakama,” alisema Kamanda Shanna.

MTUHUMIWA ASIMULIA

Awali kupitia video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Oliver alidai baada ya mume wake kufariki alihamia kwa rafiki yake ambaye alisikia kuna kazi katika kituo cha mafuta.

“Aliniunganisha na mfanyakazi wa kituo hicho ambaye pia aliniunganisha na Mhindi nikapata kazi, wakati naendelea kufanya kazi mkuu wa kituo aitwaye Ngoro akanifata akaniambia nimlipe fadhila zake kwa kutembea naye kimapenzi, nikatembea nae, nikawa mpenzi wake.

“Siku moja bosi wangu (Deepyen) akaniita, akaniambia amegombana na mwanamke wake ambaye amezaa naye mtoto mmoja na amempiga ameteguka mkono, hivyo akaniambia niwe namsaidia kumchua, nikawa namsaidia kweli.

“Siku ya kwanza nikamkuta yuko uchi akiwa amejifunga taulo, akajifanya limedondoka, siku iliyofuata nikamkuta uchi wa mnyama nikawa naogopa kwenda kumfanyia usafi.

“Siku iliyofuata sasa nikawa naogopa, akaniita tena, kwa sababu ni bosi na nilikuwa napenda kazi yangu nikaenda. Siku hiyo nikamkuta yuko uchi, wakati natoka nakimbia akanivuta kifuani kwake akaniambia ‘Oliver usiogope’. nikamwambia hapana bosi.

“Akaniambia nisiogope atanifanyia vitu vikubwa, nikamwambia hapana, kilichonishangaza na kunisikitisha bosi akawa ananitaka kinyume na maumbile, nikakimbia nje nikarudi upande wa supermarket, kabla sijatoka pale nikamwambia bosi naenda kukuripoti kituo cha polisi,” alidai Oliver.

Alidai wakati amekaa nje kwenye kiti alishangaa kuona gari la polisi likiwa na mgambo wawili ambao walianza kumpiga makofi, mateke na kumvuta nywele hadi zikakatika.

“Nikapelekwa kituo cha polisi na kuwekwa lock-up, nikauliza kosa langu ni nini, akaniambia tena nisiongee akarudia kunipiga, akanivuta pale mpaka chupi yangu ikachanika, akanitolea kashfa.

“Dhamana ikakataliwa akaniambia ndugu zangu watoe Sh 100,000 ila ndugu zangu hawakuwa na hiyo hela, wakafanikiwa kumpa 20,000 wakachukua nikapata dhamana nikawa nahudhuria kituoni.

“Mara kidogo nashangaa kesi iko mahakamani, mara matairi yameletwa sijui yametoka wapi na mashahidi wa uongo, nikimuongelesha hakimu na nilikuwa naumwa nina maumivu, namwelewesha hakimu damu zilikuwa zinanivuja huku chini, lakini hataki kunielewa.

“Baba yangu mdogo akaniwekea dhamana, siku nimeshindwa kwenda nimelazwa pale Rhotia na daktari mkuu ndiye alinitibu. Ndugu zangu wakaenda na cheti cha hospitali, hakimu hakusikiliza akamweka ndani baba yangu mdogo wakasema bila Sh 500,000 hawezi kutoka, wakaongea pale wakatoa 300,000 akaachiwa.

“Wakamwambia baba mdogo ajitoe kunidhamini, akajitoa na dadangu mkubwa akanidhamini, ila naye alipoenda kupeleka ruhusa naye akawekwa ndani na kila ndugu zangu wakienda kuniwekea dhamana wanakamatwa.

“Nimeenda kwa RPC, RCO nimehojiwa nimewaeleza wakasema niandike maelezo ili nipewe PF 3 ila sikupewa, ndugu zangu wanateseka, watoto wangu wananitegemea, mama yangu ni mzee sina kitu chochote naomba msaada,” alidai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles