Taharuki yatanda kushambuliwa kwa Mbowe

0
2813
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimjulia hali Freeman Mbowe

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

IKIWA ni takribani miaka mitatu tangu aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) kushambuliwa kwa risasi jijini Dodoma Septemba, 7 2017, wakati akihudhuria vikao vya Bunge, juzi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe naye alishambuliwa pia akiwa jijini humo kuhudhuria vikao vya Bunge.

Wakati tukio hilo likitokea, Polisi wametaka lisihusishwe na masuala ya kisiasa na kwamba ni la kihalifu kama yalivyo matukio mengine, huku Spika wa Bunge, Job Ndugai akiwatoa hofu wabunge kwa kusema Dodoma ni sehemu salama kwa wabunge kuishi.

Mbowe ambaye kwa mujibu wa polisi alishambuliwa juzi usiku na watu watatu ambao hawajafahamika, jana alipelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

KAULI YA NDUGAI

Jana akizungumza bungeni, Spika Ndugai alisema amemtembelea  Mbowe na kwamba hajaumia sana, hivyo wanasubiri taarifa kutoka kwa madaktari ili waeleze kwa kina tatizo ni nini.

Akizungumza jioni jana wakati wabunge wakichangia azimio la kumpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa namna alivyoliongoza taifa katika mapambano dhidi ya janga la corona, Spika Ndugai alisema jana asubuhi alimtembelea Mbowe na kumkuta akiendelea vizuri.

Ndugai akilizungumzia tukio hilo, alisema; “nimepata nafasi ya kumtembelea leo (jana) asubuhi nikaongea nae, kwa ujumla hayupo katika hali mbaya, alikuwa akipata chai asubuhi, amepata tatizo mguu wa kulia, ni kitu kama  ‘dislocation’, sio kuvunjika kwa mfupa, madaktari wanajua vizuri, kwahiyo yupo madaktari wanamwangalia, wamenambia watatupatia ushauri wao.

“Kwa jambo lenyewe lina taarifa nyingi kwani inasemekana jana (juzi) mpaka saa sita usiku alikuwa mahali, kwahiyo lina hadithi nyingi, kwahiyo inaniwia vigumu, lakini niseme msichukulie kama hivyo mnavyosikia,” alisema Ndugai.

Alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuja na maelezo ni kitu gani, juu ya nini kimempata Mbowe.

“Watakaosema halisi ni vyombo vya ulinzi na usalama, kwahiyo niwaombe (polisi) mtoke mapema mtoe taarifa. Waelezeni kilitokea nini, isiwe ni kazi yangu, ni kazi ya vyombo vya ulinzi na usalama. Mimi naamini kesho (leo) jioni tutakuwa na kiasi fulani cha kusema,” alisema Ndugai.

Aliwahakikishia wabunge kwamba Dodoma ni sehemu salama kwa kuishi na wala wasiwe na wasiwasi.

“Niwahakikishie waheshimiwa wabunge Dodoma ni salama kabisa, ni salama kabisa kabisa, tumekaa hapa tangu mwezi wa nne mwanzoni hadi sasa ni mwezi wa sita, hakuna aliyepoteza sikio, hakuna aliyepoteza jicho, hakuna aliyechomoka mkono, hakuna aliyekatika kidole, Dodoma ni salama,” alisema Ndugai.

LIJUALIKALI: MBOWE ALIDONDOKA

Akizungumza bungeni jana, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali (Chadema) alisema si kweli kwamba Mbowe ameshambuliwa bali amedondoka wakati akipanda ngazi.

“Inawezekaneje KUB (Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni) atembee usiku wa manane awe hana mtu wa kumsaidia, anatembea peke yake na wao (Chadema) wanasema ni chama chenye umakini, hivi unakuwa makini unashindwa kujilinda wewe kiongozi mkuu unatembea peke yako.

“Halafu hizi ndio akili mbadala, hii sasa ndio akili mbadala, kwenye vikao unajifanya ‘live’ ila usiku unaenda baa mnakunywa mnalewa, tungeweza kukaa kimya, kwa sababu wameingiza siasa.

“Eti Serikali, mtu anataka kukuumiza akuvunje leo kwa ajili ya uchaguzi wa mwezi wa 10, Serikali wamekupa askari leo wasubirie wakuvunje ka-mguu.

“Watanzania naomba mfahamu mwenyekiti hii ni michezo inafanyika, na ukitaka kujua ni usanii kwanini kaenda Ntyuka na sio General, kaenda private (hospitali binafsi) ili afichiwe. Haya mambo huwa tunayafanya.

“Mheshimiwa Rais Magufuli na Serikali ya CCM nataka niwaambie mpo sehemu sahihi na salama, huu ujanja ujanja hautawafikisha (upinzani) sehemu yoyote, ni kujipotezea muda, huku ni sehemu ya kufanya dili zao tu,” alisema Lijualikali.  

NDUGAI TENA

Baada ya maelezo ya Lijualikali, Ndugai alisema; “wabunge huu ni mchnago wa Lijualikali, mambo haya yanatuhusu sisi, nadhani mnaelewa kwanini nimeshindwa kueleza mtu aliyeumizwa hawezi kupelekwa katika kituo cha afya.”

Spika Ndugai alisema amepokea barua kutoka kwa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee akiomba Bunge liwapatie ndege kumsafirisha Mbowe ili akapate matibabu zaidi.

Alisema Bunge limekataa kutoa ndege hiyo kwani utaratibu anayelazwa ni lazima rufaa iwe imetoka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ama Benjamin Mkapa.  

“Hapa nina barua nimeikuta ya Halima Mdee anaomba usafiri wa ndege ili tumsafirishe, sasa utaratibu wetu wa rufaa lazima ziwe zimetoka katika hospitali za rufaa kama General na Benjamin Mkapa, ni vigumu kutoka katika kituo cha afya,” alisema Ndugai.

Alisema Rais Dk. Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wamefika katika Hospitali ya Ntyuka kumjulia hali Mbowe.

“Mwenzetu ameumia, lakini nimeenda kumuona na Waziri Mkuu amemuona na Rais ameenda kumuona, tumetekeleza wajibu wetu, lakini isiingizwe siasa wakati jambo hili halipo kabisa,” alisema Ndugai.

Aliitaka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi watoe taarifa haraka ya nini kinachoendelea.

“Waziri wa Mambo ya Ndani, Polisi watoe taarifa haraka ya kile kipande kwa sababu jamii kuirudisha katika mstari ni kazi, polisi watoke waseme,” alisema Ndugai.  

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here