Ndugai: Iwe isiwe lazima JPM aongozewe muda

0
1071

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amesema kuwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, amemtaka Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM) kuja na azimio la kutaka Rais Dk. John Magufuli aongezewe muda baada ya mwaka 2025 na iwe isiwe lazima iwe hivyo hata kama hataki.

Kauli hiyo ya Ndugai ilikuja baada ya Mbunge Kessy kuomba Bunge kumwongezea muda Rais Magufuli mara baada ya kumaliza kipindi chake cha pili cha uongozi mwaka 2025.

Akichangia jana mjadala wa azimio la kumpongeza Rais Magufuli kwa namna alivyoliongoza taifa katika mapambano dhidi ya janga la ugonjwa wa corona, Kessy alisema anatakiwa kuongezewa muda wa kuongoza nchi mara baada ya 2025.

“Labda nyinyi hamsumbuliwi, mimi nasumbuliwa, kuna nchi zingine wanapingwa na wameuawa kwa ajili ya corona. Katiba sio msahafu, inabadilishwa wakati wowote na anakuwa sio Rais wa kwanza, alazimishwe atake asitake, haiwezekani kumwachia nafasi, nataka alazimishwe tu,” alisema Kessy.

Wakati akiendelea kuchangia Spika Ndugai alisema: “Mheshimiwa ngoja twende kwenye Uchaguzi Mkuu turudi, naamini wote tunarudi, hilo lishike uwe nalo na azimio litapita kwa kishindo atake asitake ataongeza muda (Rais Magufuli.”

Akiendelea kuchangia, Kessy alisema ifikapo Uchaguzi wa Oktoba Watanzania wanatakiwa kupiga kura mara mbili ya kumchagua Rais Magufuli na nyingine aendelee kuongoza baada ya mwaka 2025.  

“Tunapongeza tunapongeza mpaka lini, aendelee tu hii Katiba sio msahafu, tupige kura Oktoba aongezewe muda, haitakiwi gharama mara mbili, akikataa tumlazimishe,” alisema Kessy.

Spika wa Bunge, Ndugai aliungana na Kessy kwa kudai kwamba Bunge hilo ndilo lenye mamlaka ya kutengua hilo, hivyo atake asitake ni lazima aongezewe muda.

“Nikuhakikishie Bunge hili ndiyo lina mamalaka ya kutengua hilo, yeye amekuwa nani asiombwe, lazima aongezewe muda atake asitake,” alisema Ndugai.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here