29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

POINTI ZA MEZANI ZINAVYOIPA SURA MBAYA SOKA LA TANZANIA

ABDUL MKEYENGE


HALI ya uwepo kwa uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) unaotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu ndiyo unaotajwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya soka nchini kuwa ni moja ya kitu kinachozalisha madudu mengi hivi sasa.

Kutaka kurejea uongozini kwa baadhi ya viongozi na viongozi wengine kutaka kuingia madarakani imefanya viongozi walioko madarakani hivi sasa kusahau majukumu yao kwa Watanzania na kujikita katika kampeni za kutetea viti vyao.

Hili ndilo linaloufanya mpira wa miguu uonekane kuchekesha, si kingine. Kila kiongozi aliyeko madarakani anatazama jinsi gani atakuwa sehemu ya viongozi wa mkondo ujao. Ukishakuwa na kiongozi wa namna hii, tarajia kukutana na ‘sinema’ hizi unazozishuhudia wakati huu.

Matukio tunayoendelea kuyaona ni kutokana na kukosa uongozi thabiti unaoweza kujipanga vyema na kuusimamia mpira wenyewe ili kuepusha hali iliyoko. Kama viongozi wakuu hawajali na kinachoendelea, nani atatoka kusikojulikana aje kujali?

Kama Watanzania tumefikia hapa, hatuna tena ujanja. Viongozi wa TFF wametugueza mateka wao na wanatuendesha vile wanavyotaka. Kama tungekuwa na uongozi imara unaosimamia masilahi ya soka la Tanzania tusingesikia kelele tunazozisikia hivi sasa. Tungekuwa tumejikita kuzungumza, kuandika mafanikio ya soka la Tanzania, lakini haiko hivi, kila siku ni matatizo tu!

Wakati uongozi wa Jamal Malinzi ukielekea ukiongoni, matatizo ndiyo yamezidi kuongezeka. Kila unapomalizika mwezi mmoja kwenda mwezi mwingine ndivyo ambavyo hata matatizo yanapishana kama miezi. Ni nadra mwezi kuisha bila kutokea tatizo lolote lile ndani ya mpira wetu.

Kinachoharibu ni kusemekana kwamba viongozi wenyewe wamekuwa wagumu kukutana na wadau kuzipokea changamoto, badala yake viongozi wamekuwa watu wa kujifungia ndani ya ofisi zao wakipigwa na ‘AC’. Japo ushauri si lazima uchukuliwe, lakini wadau wanatakiwa kusikilizwa. Siamini kama tunaweza kutengeneza nyumba moja kisha tuanze kugombania fito. Siamini.

Achana na matatizo yote yaliyopita huko nyuma, suala la klabu za Simba na Kagera Sugar kuzigombania pointi tatu ni jambo linalogonga vichwa vya wapenda soka, japo jana suala hilo lilitarajiwa kutolewa maamuzi yake.

 

Jambo hili limekuwa zito na kufanya hadi watu wa taasisi mbalimbali za soka kuingilia kati na wengine kunyoosheana hadi vidole vya macho. Lakini ukubwa wa jambo hili umekuzwa na TFF na kamati zake ambazo zimeshindwa kusimamia ndani ya kanuni zao na badala yake suala hilo kuhamia kwenye utashi wa watu binafsi.

 

Kanuni za Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) ziko wazi kabisa kama itafahamika mchezaji amecheza mechi ana kadi tatu za njano katika michezo iliyopita haruhusiwi kucheza mchezo unaofuata na akicheza adhabu yake inajulikana. Na kama mchezaji hakuwa na kadi kimsingi hapo hakuna kesi inayoweza kuwafanya watu kuwa makini kuisikilizia muda wote.

 

Ripoti ya mwamuzi ndiyo kauli ya mwisho ya kuamini kutokana na kila tukio la tofauti na maadili ya mchezo wa soka lazima lilipotiwe ndani ya ripoti. Inasemekana ndani ya ripoti hiyo ya mwamuzi inaonyesha mchezaji wa Kagera Sugar, Mohamed Fakhi, alipata kadi katika mchezo wa timu yake dhidi ya African Lyon, lakini mchezaji mwenyewe amepinga kuwa hakupewa kadi siku hiyo.

 

Mkanganyiko ya Kamati ya Saa 72 na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuhusu jambo hilo unatokea wapi mpaka ripoti ya mwamuzi inashindwa kusikilizwa? Aibu iliyoje kwenye mpira wetu waliitwa hadi African Lyon waliocheza na Kagera Sugar, Fakhi ili kujiridhisha na ushahidi. Kama hatutaki kuiamini ripoti ya mwamuzi tutaiamini ripoti ya mtu gani mwingine?

 

Kuwakusanya pamoja, Fakhi, African Lyon na kuwaleta mbele ya kamati waamuzi ni kutafuta ushahidi wa vurugu ambao hauwezi kutupa majibu sahihi zaidi ya ripoti ya mchezo husika. TFF na kamati zake ilitakiwa kulitolea ufafanuzi suala hili kwa kutumia ripoti tu ili kila mmoja arudi kwenye maendeleo ya kuujenga mpira wa Tanzania.

 

Ni Tanzania tu ambako unaweza kukutana na hali hii na Watanzania wenyewe hawaonekani kujali sana. Lakini licha ya hali hii ni muda sasa wa TFF na kamati zake kutazama upya baadhi ya kanuni zake na kuachana na timu kupata ushindi wa mezani.

 

Inakosesha ladha ya soka kwa timu iliyotoa kila ilichonacho kwa ajili ya kushinda mechi uwanjani na baadaye wanakuja kupokwa ushindi. TFF na kamati zake isimamie vyema kanuni ya timu itakayofanya vitendo vya namna hii ikutane na faini, lakini timu iliyoshinda wabaki na ushindi wao.

 

Katika hili wanachama wa Simba na mashabiki wao wamekuwa kipaumbele kusema hata kikosi cha vijana ‘Serengeti Boys’ kinaenda Gabon kwa ajili ya njia ya mezani, lakini watu hao walipaswa kujua rufaa ya TFF kwa timu ya vijana kwenda Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na rufaa ya Simba kwa TFF na kamati zake ni rufaa mbili tofauti. Hizi ni rufaa mbili tofauti.

 

Timu ya taifa vijana ya Congo DR, ilivunja miiko kwa kumchezsha mchezaji mwenye umri mkubwa ‘kijeba’. Na adhabu za namna hii ziko wazi kwa CAF ndio maana hatukuisikia kelele za mashabiki wa Congo DR, walijua wamefanya kosa na walihitaji adhabu ya kuondolewa. Lakini sehemu ya Simba ni masuala ya kikanuni tu, lakini sio Kagera Sugar kupokwa ushindi wao.

 

Suala la Simba, Kagera Sugar linahitaji busara za kilichoandikwa na waamuzi wa mchezo wa Kagera Sugar na African Lyon. Vingine vyote tunavyovisikia tutakuwa tunadanganyana. Haijalishi ni kweli mchezaji alipewa kadi au hakupewa. Haijalishi kama mwamuzi aliandika kweli mchezaji alipata kadi au hakupata. Tunahitaji kuziamini ripoti za waamuzi. Kama hatuamini ripoti zao tutamuanini nani mwingine

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles