22.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 5, 2024

Contact us: [email protected]

Pengo asisitiza amani miaka 150 Kanisa Katoliki

Na ESTHER MBUSSI-DAR ES SALAAM


ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema anasikitishwa na migogoro kati ya makanisa nchini huku akisisitiza watu kuendelea kuomba amani.

Pengo ameyasema hayo  Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu miaka 150 ya uinjilishaji wa kanisa hilo ambayo itafanyika kuanzia Novemba 2-4, wilayani Bagamoyo Mkoa  wa  Pwani.

“Ni jambo linalosikitisha kama watu wanafuta amani kwa maana ile ile ya kusaidia watu na malengo ni yale yale lakini hayafikiwi, kuhusu nyaraka hizo ni vitu ambavyo vinaweza kupata tafsiri kulingana na watu mbalimbali.

“Katika kuadhimisha miaka 150 ningetamani matokeo yawe ni kuimarisha   unjilishaji na ilete muungano kwa wananchi licha ya tofauti ya  dini na imani tuliyo nayo tupige hatua zaidi ya kuwa wamoja,” alisema.

Miaka 150 ya kanisa hilo

Alisema kanisa linajivunia kuwa katika miaka 150 ujumbe wa injili haukubaki Bagamoyo au Zanzibar ilikoanzia, bali imeenea sehemu zote na kuna wakristu wengi walioipokea  injili hiyo.

Alisema sababu hiyo ndiyo imelifanya kanisa kusherehekea kwa sababu  ingekuwa injili imeishia Bagamoyo leo wasingefanya hivyo.

“Pamoja na injili lakini kanisa pia limekuwa chanzo cha elimu kwa ujumla.

“Kwa mfano mambo ya kusoma na kuandika yameanzishwa na hao wamisionari kiasi kwamba sasa tunaweza kupata taarifa na mambo mengine kutokana na kazi waliyoianza Wamisionari tangu mwanzo.

“Kanisa daima limejitahidi kutoa huduma za jamii yaani elimu, tiba, mambo ya madawa… kuna sehemu shule za sekondari hazikuwapo, zilikuwapo za kanisa tu.

“Tunashukuru serikali imejitahidi kutoa huduma hizo kwa upana lakini zipo sehemu ambazo kwa muda mrefu hazikuwa na huduma kama hizo kama posta yaani mawasiliano, ambazo ziliendeshwa na kanisa.

“Lakini tunajua zaidi haya ni majukumu ya serikali na sasa hivi inakazana ishike huduma hizi.

Hili ni jambo la kufurahisha kwa sababu ndiyo kazi ya serikali na dini na taasisi mbalimbali zinaweza tu kusaidia katika kutekeleza huduma hizo,” alisema Kardinali Pengo.

Historia ya Kanisa

Kardinali Pengo   akizungumzia historia ya kanisa hilo,   alisema limekuwapo   nchini kwa miaka 150  likianzia Zanzibar.

“Wamisionari   nchini walifika Bagamoyo mwaka 1868 na ndiyo mwaka ambao uinjilishaji ulianzishwa Tanzania Bara   na nchi jirani.

“Katika Kipindi chote cha miaka 150, Kanisa linajivunia kuenea  ujumbe wa injili nchini na sehemu mbalimbali katika mwambao wa nchi za Afrika   Mashariki.

“Pia kanisa limekuwa chanzo cha elimu na tumeheshimu uhuru wa kuabudu katika taifa letu,” alisema.

Uhuru wa kuabudu

Akizungumzia uhuru wa kuabudu nchini, Kardinali Pengo alisema upo kwa sababu licha ya tofauti za  dini watu wamekuwa wakishirikiana kwa pamoja.

“Nadhani wote tunaona tunao uhuru wa kuabudu, sina maana kanisa katoliki libaki peke yake, ila ukweli ni kwamba ibada zinafanyika kutokana na madhebeu yaliyopo.

“Dini kama dini hapa walau hapa Mashariki mwa Afrika hatugombani, wanaweza wakawapo watu wachache wawe wakristu au waislamu, watu wa dini tofauti wakawa na maelekeo tofauti na wengine lakini huwezi ukasema ni dini fulani inaleta wasiwasi wa amani katika taifa lile,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles