23.7 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Penalti zaing’oa Kili Stars Chalenji Cup

mtanzania kila siku safiSiah.inddNA MWANDISHI WETU

PENALTI mbili za timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, zilizopigwa na kiungo Jonas Mkude na beki Shomari Kapombe, zimeing’oa timu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Chalenji baada ya kuchezwa na kipa Abel Mamo wa Ethiopia na kuwavusha wenyeji hao katika hatua ya nusu fainali.

Mamo alizicheza vema penalti hizo na kuiongoza Ethiopia kutinga hatua hiyo kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 4-3, kufuatia dakika 90 matokeo kwisha kwa sare ya bao 1-1 na sasa Ethiopia itavaana na Uganda kwenye nusu fainali itakayoanza keshokutwa.

Kili Stars ndiyo ilikuwa ya kwanza kufunga bao la kuongoza dakika ya 25, lililofungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ kwa kichwa, akimalizia kona iliyochongwa na kiungo Said Ndemla, bao lililodumu hadi mpira huo unakwenda mapumziko.

Kipindi cha pili Ethiopia walibadilika na kuanza mpira kwa kasi na ikafanikiwa kupata penalti iliyoonekana kuwa na utata dakika ya 56, baada ya Yissak Bereket kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki Kapombe.

Marudio ya picha za televisheni yalionyesha kuwa kabla ya Kapombe kugusa miguu ya Bereket na kuanguka chini, beki huyo alianza kuugusa mpira kwanza, lakini mwamuzi akaamuru ipigwe penalti ambayo ililalamikiwa sana na wachezaji wa Kili Stars, hadi kupelekea beki Kelvin Yondani kulimwa kadi ya njano.

Mkwaju huo wa penalti ukafungwa vema na Gathuoch Panom dakika ya 57, aliyemtesa kipa wa Kili Stars, Said Mohamed, aliyeruka kulia na mpira kupigwa upande wa kushoto kwake na kupelekea dakika 90 kwisha kwa sare hiyo.

Hapo ndipo mchezo ulipoelekea hatua ya kupigiana mikwaju ya penalti ili kupata mshindi. Ukiondoa Mkude na Kapombe waliokosa kwa upande wa Kili Stars, waliofanikiwa kufunga ni nahodha Bocco,  Himid Mao na Hassan Kessy, huku wenyeji Ethiopia wakipata zote kupitia kwa Panom, Mohammed Nasser, Ashelew Tamene na Behaylu Girma.

Licha ya Kili Stars kutolewa, imefanikiwa kuondoka na rekodi bora kwenye michuano hiyo, ikiwa haijafungwa mchezo wowote ndani ya dakika 90, kwenye hatua ya makundi ikitoka Kundi A, iliambulia ushindi mechi mbili dhidi ya Somalia (4-0) na Rwanda (2-1) kabla ya kulazimishwa sare ya 1-1 dhidi Ethiopia, ambao ndio waliowatoa robo fainali.

Kutolewa huko kwa Kili Stars kumefuta ndoto za Kocha Mkuu Abdallah Kibadeni ‘King’, aliyekuwa amepania kurejea na ubingwa wa michuano hiyo Tanzania na kufuta ukame wa kutolichukua kombe hilo kwa miaka mitano tokea ilivyolitwaa mara ya mwisho 2010.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,745FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles