CHRISTINA GAULUHANGA NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM
AGIZO la Rais Dk. John Magufuli kuwabana wafanyabiashara wanaokwepa kodi nchini, limeanza kuwa mwiba baada ya mabasi ya Kampuni ya Usafirishaji Dar es Salaam (UDA), kukamatwa kutokana na kukwepa kodi.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, alisema mabasi tisa ya UDA yalikamatwa kutokana na kukiuka sheria za mlipakodi.
Mbali na UDA, Kayombo alisema TRA pia iliyakamata mabasi ya kampuni nyingine kutokana na kushindwa kulipa kodi ambapo walitumia kampuni ya udalali ya Majembe Auction Mart.
MTANZANIA ilitembelea yadi ya Majembe na kukuta mabasi ya UDA yakiwa ndani. “Sisi kama TRA tulifuata taratibu zote za kuwasiliana na wateja wetu kuhusu kulipa kodi ya Serikali, lakini jitihada zilishindikana hadi tulipoamua kukamata mali zao, huku pia wakitakiwa kulipa faini zote zinazohitajika,” alisema.
Kayombo alisema operesheni ya TRA kuwakamata wafanyabiashara wanaokwepa kodi ni endelevu nchi nzima na hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa kwa wanaokaidi kutekeleza sheria.
Hata hivyo, Kayombo hakutaka kuzungumzia kwa undani kuhusu kiwango cha kodi ambacho hakikulipwa na UDA, akidai kuwa hiyo ni siri ya mlipakodi na mamlaka yenyewe. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UDA, Robert Kisena, alithibitisha kukamatwa kwa mabasi yake ambayo alisema uzembe huo ulifanywa na idara yake ya uhasibu.
Kisena alisema muda wa kulipia kodi ulikuwa umefika, lakini idara yake ya uhasibu haikuweza kulipa viwango vinavyotakiwa.
“Ni kweli kuna magari yetu matatu au manne yamekamatwa na tatizo kubwa ni kodi ya magari, ambayo tulijua mtu wetu wa uhasibu amelipa, lakini kumbe alikuwa hajalipa,” alisema Kisena huku akisisitiza kuwa taratibu za kuyakomboa magari hayo zimefanyika ambapo wamekwishalipia gharama zilizokuwa zinahitajika.