25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

PANGUAPANGUA UWT YAVURUGA MADIWANI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT),  umefanya mabadiliko ya makatibu wa wilaya, ambapo baadhi ya watumishi wake ambao ni madiwani wa viti maalumu wamejikuta wakipelekwa nje ya halmashauri zao.

Mabadiliko hayo yamekuja ikiwa ni mwezi mmoja baada ya CCM kupitisha mabadiliko ya katiba yake katika Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika Machi 12, mwaka huu, mkoani Dodoma.

Mabadiliko hayo yameeleza wazi kuwa hivi sasa mtu mmoja cheo kimoja, tofauti na zamani ambapo baadhi ya viongozi ndani na nje ya chama hicho walikua wanajilimbikizia vyeo.

Uhamisho huo umetajwa kuwavuruga baadhi ya makatibu ambao pia ni madiwani wa viti maalumu katika halmashauri zao wanazotumikia.

Baadhi ya makatibu waliohamishwa na maeneo wanayokwenda kwenye mabano ni Huba Issa anayetoka Kinondoni kwenda Newala), Monica Nyagu (Kongwa – Manyoni), Joan Mazanda (Dodoma Mjini – Singida Vijijini), Mwashamba Shekue (Tanga Jiji – Kilindi) na Hilda Mdaki (Gairo – Rombo).

Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu wa UWT Taifa, Amina Makilagi alisema mabadiliko hayo hayawazuii madiwani hao kutekeleza majukumu yao.

 “Sisi kazi yetu haihusiani na udiwani wake, amekuwa diwani hilo ni jukumu lake yeye mwenyewe, mkataba wetu sisi ni kufanya kazi mahala popote.

“Yeye mwenyewe atajipanga atajua anatekelezaje wajibu wake, mkataba wetu na yeye ni kufanya kazi Tanzania nzima, hata kama akiwa ni mbunge tunamtegemea afanye kazi za UWT na ndiyo maana hivi sasa tumerekebisha kanuni zetu za uchaguzi kwamba kila mtu awe na nafasi moja ya uongozi,” alisema Makilagi.

Alisema tangu mwaka 1995 baadhi ya makatibu walikuwa ni madiwani lakini hilo halikuathiri udiwani wao bali ni namna tu ya kujipanga.

“Akiwa ni mtumishi anakwenda popote huo ndiyo mkataba wetu, kumhamisha kituo cha kazi hakumwondolei ukaazi wake wa kawaida,” alisema. 

TAMISEMI

Kulingana na sheria za serikali za mitaa, diwani anapaswa kuishi ndani ya halmashauri husika na kama asipohudhuria vikao vitatu anakuwa si diwani tena.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, alisema leo atakutana na Katibu Mkuu wa UWT, Amina Makilagi ili kujadili hali hiyo.

“Kwa kweli kesho (leo) nitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kulisema hili baada ya kukutana na Katibu Mkuu wa UWT, ingawa tunajua kwamba katibu ni mwajiriwa na mwajiri anaweza kumtumia atakavyo ila kwa kuwa ni mwakilishi wa wananchi hapa ndipo tunaposema inahitajika busara zaidi.

“… nami tayari nimeshapokea kesi mojawapo hapa Dodoma yupo mtumishi wa UWT ambaye ni diwani na amepangiwa kwenda kwenye kituo cha kazi kingine sasa kwa hali hii ninaamini baada ya kukutana na kujadiliana kwa kina na Katibu Mkuu (Makilagi) tutapata mwafaka wa pamoja ila kifupi bado kuna contradiction (mkanganyiko),” alisema Simbachawene.

Hivi karibuni Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilitangaza nafasi za waajiriwa wote wa jumuiya za chama zitakuwa chini ya chama hicho.

Hata hivyo taarifa zisizorasmi zinaeleza kuwa uhamisho huo unadaiwa kufanywa, huku ikielezwa kuwa hakuna kikao chchote cha jumuiya kilichokaa kujadili uhamisho wa watumishi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles