28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

CUF LIPUMBA, MEYA JACOB WAINGIA KATIKA VITA YA MANENO

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


CHAMA cha Wananchi (CUF) Wilaya za Ubungo na Kinondoni, ambao wanamunga mkono Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba wameingia katika vita ya maneno na Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob  baada ya kiongozi huyo kutangaza ufadhili wake kwa CUF upande wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Katibu wa CUF Wilaya ya Kinondoni, Mohamed Mkandu, alisema hatua ya Meya Jacob kutangaza kuchangia kiasi cha Sh milioni 100 ili kumpinga Prof. Lipumba, kinawafanya sasa waanze kumuona kama adui yao ambaye watapambana naye kwa kila njia.

“Huyo meya ni mtu wa ajabu sana, sasa anaingia mambo ya CUF kwa kutangaza yupo tayari kutoa vijana wa Chadema kwenda kumtoa Profesa Lipumba ofisi za CUF zilizopo Buguruni. Tunasema kama anaweza ana ajaribu kufanya hilo analotaka kulifanya nasi tupo tayari tunamsubiri.

“Anafanya matumizi mabaya ya fedha za wananchi wa Ubungo kwa kuwa kinara wa kuwapa watu fedha ili wafanye vurugu, ni vema atambue hii si kazi ya meya,” alisema Mkandu.

Alisema wapo tayari kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kufuatilia kwa karibu taarifa za baadhi ya miradi inayotekelezwa katika Wilaya ya Kinondoni na kudai kuwa Jacob alikuwa anajipa tenda mwenyewe alipokuwa meya wa Kinondoni.

“Tumekaa na wanachama wetu na tumeazimia kuwa Mwenyekiti wa CUF ni Lipumba kwa mujibu wa Katiba ya chama chetu na anayetaka kufanya aina yoyote ya vurugu tutamdhibiti,” alisema.

Mkandu aliwataka wanachama waliofanya kikao katika Hoteli ya Vina waandike barua ya kuomba radhi kabla vikao halali vya kikatiba havijawachukulia hatua za kinidhamu.

 “Katika matawi yote ya CUF ni marufuku kuwatukana viongozi na mwanachama akisikia arekodi na kuwatumia viongozi.

“Tutahudhuria katika vikao vyao vyote vitakavyoitishwa na wanachama wa CUF wanaomuunga mkono Maalim Seif ili kukilinda chama chetu,” alisema Mkandu.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa Wilaya ya Ubungo,  Ally Makwilo, alimshangaa Meya Jacob kutaka kutoa Sh milioni 100 kumwondoa Profesa Lipumba wakati kuna changamoto nyingi katika wilaya hiyo.

“Ubungo kuna matatizo lukuki, ikiwamo shida ya maji, madawati, madawa hospitali na barabara nzuri. Lakini meya anashindwa kuelekeza fedha hizo za umma kwenye kuboresha huduma za jamii. Na si hilo, hana kipato cha kuwapa Sh milioni 100 kina Mtatiro,” alisema Makwilo.

Akijibu tuhuma hizo, Meya Jacob alisema yeye anaamini katika Umoja wa Katiba ya Wananchi ndiyo maana hata Naibu Meya wa Manispaa ya Ubungo anatokana na CUF.

“Niko tayari kuchangia CUF kwa kiasi chochote kwa kuwa ni moja ya vyama vinavyounda Ukawa. Iwapo CUF watahitaji vijana kwenda kuwasaidia, pia niko tayari, ” alisema Meya Jacob.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,085FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles