26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

CAG AIBUA MAPYA SEKTA YA ELIMU

*Aonya hatua zisipochukuliwa wanafunzi wataendelea kufeli


Na ELIZABETH HOMBO – DODOMA

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, amebaini uhaba mkubwa wa miundombinu na samani katika shule za msingi na sekondari nchini.

Kutokana na hilo, ameonya lengo la kuondoa kiwango cha ujinga katika jamii linaweza lisifikiwe endapo hatua za uboreshaji hazitachukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine.

Alisema uhaba wa miundombinu ya shule na samani, unasababisha kuwapo kwa matokeo mabaya ya wanafunzi katika shule hizo.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2015/16, iliyowasilishwa bungeni Alhamisi iliyopita na Profesa Assad, mahitaji ya madawati katika shule za sekondari ni 64,675, yaliyopo ni 36,043 na upungufu 28,632 sawa na asilimia 44.

Alisema kwa upande wa maabara, mahitaji ni 5,896, zilizopo ni 2,432 upungufu 3,495 sawa na asilimia 59, huku vyoo mahitaji ni 81,173 vilivyopo 20,510, upungufu 60,663 sawa na asilimia 75.

“Nyumba za walimu mahitaji ni 56,000, zilizopo 11,017, upungufu 44,983 sawa na asilimia 80, mabweni mahitaji ni 876, yaliyopo 347, upungufu 529 sawa na asilimia 60, mahitaji ya madarasa ni 209,773, yaliyopo 109,767, upungufu 100,006 sawa na asilimia 48.

“Mahitaji ya madarasa katika shule za msingi ni 44,000 yaliyopo 23,630 upungufu 20,370 asilimia 46, vyoo 90,988 vilivyopo 57,017 upungufu 33,971 asilimia 37.

“Kwa upande wa nyumba za walimu, mahitaji 69,047 zilizopo 19,500 upungufu 49,547 asilimia 72, madawati 397,652 yaliyopo 278,443 upungufu 119,209 sawa na asilimia 30,”alisema Profesa Assad.

 Alisema alibaini ufaulu wa wanafunzi katika shule za sekondari za Serikali, unapungua mwaka hadi mwaka.

Profesa Assad alisema ukaguzi wake, ulibaini uwezo wa wanafunzi wa kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya kawaida na ile ya ngazi ya juu unapungua kila mwaka.

“Hii inaashiria uhaba wa miundombinu na samani katika shule ni changamoto kubwa inayoikabili sekta ya elimu katika mamlaka za Serikali za mitaa na nchi kwa ujumla,” alisema Profesa Assad.

Alisema kukosekana kwa miundombinu muhimu ya shule kunaweza kuendelea kuathiri ubora wa elimu katika shule za msingi na sekondari.

Kutokana na hilo, Profesa Assad alipendekeza menejimenti ya mamlaka za Serikali za Mitaa na Serikali kwa ujumla kuweka mikakati ambayo itaboresha miundombinu ili kuimarisha ubora wa elimu.

Alisema mikakati hiyo ni pamoja na kutenga fedha zaidi katika ujenzi wa miundombinu ya shule na kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa ufanisi wa ubora wa elimu.

Profesa Assad alisema kuna uhaba wa walimu wa sayansi katika shule za sekondari na waliopo wachache kutopangiwa shule kwa uwiano sawa.

“Ukaguzi niliofanya katika Idara ya Elimu ya Sekondari kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa katika mwaka wa fedha 2015/16, umebaini uhaba mkubwa wa walimu wa sayansi 3,438 na wataalamu wa maabara 1,087 kwa ajili ya kufundisha masomo ya sayansi katika shule za sekondari.

“Ukaguzi wangu uligundua zaidi walimu wa sayansi wachache waliopo walisambazwa bila kuwa na uwiano mzuri kwenye shule za sekondari ndani ya halmashauri, hali iliyofanya baadhi ya shule kuwa na idadi kubwa ya walimu wa sayansi na kuacha Shule nyingine bila hata kuwa na mwalimu mmoja wa sayansi.

“Katika baadhi ya halmashauri, walimu wa sayansi walipelekwa makao makuu ya halmashauri na kupangiwa majukumu ambayo hayahusiani na ufundishaji. Kwa mfano, walimu wa hisabati na teknolojia ya habari na mawasiliano katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.

“Baadhi ya halmashauri walimu walikuwa hawatumiki kikamilifu mfano mzuri ni Manispaa ya Morogoro ambapo walimu wa sayansi wenye sifa za shahada ya uzamili katika masomo ya sayansi na hisabati, walipelekwa kufundisha katika shule za sekondari za elimu ya kawaida badala ya kuwapanga kufundisha elimu ya juu ya sekondari,” alisema.

Alisema hali hiyo inadhihirisha wazi kuwa rasilimali watu haitumiki ipasavyo.

Alizishauri menejimenti za halmashauri kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuja na mikakati inayotekelezeka ili kumaliza tatizo la walimu wa sayansi kwa kuhamisha walimu wa sayansi ambao ni wahitimu wa shahada.

Hivi karibuni utafiti uliofanywa na Taasisi ya HakiElimu kuhusu utekelezaji wa Serikali wa kutoa elimu bure, ulionyesha kukumbana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.

Mwanzoni mwa mwaka 2016, Serikali ilitangaza kutoa elimu ya msingi bila ada katika waraka wa elimu namba 5 wa mwaka 2015, iliahidi kugharamia utoaji wa elimu ya msingi na wazazi watagharamia nauli, vifaa, sare za shule na matibabu ya watoto wao.

Katika utafiti huo, HakiElimu ilibaini changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na fedha za ruzuku hazifiki shuleni kwa wakati sambamba na kutozingatia idadi ya wanafunzi kama ambavyo inapaswa.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, John Kalage, alisema utafiti huo umeonyesha baadhi ya shule zenye wanafunzi wachache zinapata fedha zaidi kuliko zenye wanafunzi wengi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,371FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles