24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WENGER: KELELE ZA MASHABIKI ZINAWACHANGANYA WACHEZAJI

LONDON, ENGLAND


KOCHA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger, amewataka mashabiki wa timu hiyo kupunguza kelele za kumtaka aondoke kwa kuwa zinawachanganya wachezaji wao kuelekea michezo iliyobaki.

Mashabiki wa timu hiyo wamekuwa wakiandamana kila mara huku wakimtaka kocha huyo kuondoka kutokana na timu yao kufanya vibaya katika baadhi ya michezo yao msimu huu.

Hata hivyo, kocha huyo ameshindwa kuzuia hisia zake na kuweka wazi kuwa kuondoka kwake kutatokana na kufikia makubaliano na uongozi na si vile ambavyo wanataka mashabiki hao.

Katika michezo 12 ya mwisho ambayo Arsenal wamecheza, wameweza kupoteza michezo saba katika michuano mbalimbali.

Leo hii timu hiyo ya Arsenal inatarajia kushuka dimbani ugenini kwenye Uwanja wa Middlesbrough katika michuano ya ligi kuu, ambapo kwa sasa Arsenal inashika nafasi ya saba baada ya kucheza michezo 30, hivyo Wenger amewataka mashabiki wa timu hiyo kuwa na utulivu ili wachezaji wake warudi katika hali yao ya kawaida na kuipigania timu yao.

“Timu kwa sasa inapambana kuhakikisha inafanya vizuri katika michezo iliyobaki, kuna wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao wanaweza kubadilisha matokeo muda wowote, lakini ninaamini mashabiki wanachangia wachezaji hao kucheza chini ya kiwango.

“Kelele za mashabiki zinawafanya wachezaji kuwa na wasiwasi juu ya uwepo wangu ndani ya klabu hiyo, hivyo ni wakati sasa wa kutulia kusubiri hadi mwisho wa ligi ili mambo mengine yaendelee, lakini kwa sasa kikubwa ambacho kinatakiwa ni kuhakikisha timu inapewa sapoti kubwa ili iweze kumaliza nafasi za juu.

“Wapo wachezaji wanaotarajia kumaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu na bado wapo kwa ajili ya kuipigania timu hadi siku ya mwisho, hivyo umoja unatakiwa ili kuipigania timu,” alisema Wenger.

Hata hivyo, inasemekana kuwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 67 tayari amekaa na uongozi wa timu hiyo juu ya kuongezewa mkataba wa miaka miwili na amedai kuwa muda mfupi ujao kila kitu atakiweka wazi juu ya uwepo wake ndani ya timu hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles