23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

PABLO ESCOBAR NDIYE ALPHA NA OMEGA WA COCAINE

Na Luqman Maloto


ALPHA na Omega ni herufi za mwanzo na mwisho katika mpangilio wa herufi za Kigiriki. Alpha na Omega ni utambulisho wa Kristo na Mungu katika Kitabu cha Ufunuo.

Ndani ya Kitabu cha Ufunuo, aya ya 1:8, 21:6 na 22:13, Yesu anarudia maneno kuwa Mungu ndiye Alpha na Omega. Kwa Wayahudi, Alpha na Omega humaanisha kuwa Mungu ndiye Kwanza Kati na Mwisho.

Katika Uislamu, Alpha na Omega hubeba tafsiri ya majina mawili kati ya 99 ya Mungu, kwamba ndiye wa-Mwanzo na wa-Mwisho.

Tafsiri pana ni kuwa Alpha na Omega ni kutimia kwa jambo, kwamba kunakuwa na mwanzo mpaka mwisho wake. Unaweza kutafsiri pia kuwa Alpha na Omega maana yake ni kila kitu.

Kwamba Mungu ni wa kila kitu duniani, kwa maana kile kisicho na ridhaa yake hakiwezi kutendeka. Hulinda na kuzuia yasitokee kwa utashi wake, vilevile huruhusu na kuacha yatokee kwa sababu maalumu.

Shetani pia anaweza kuitwa Alpha na Omega katika ulimwengu wa dhambi. Hii ni kwa sababu kila dhambi itendekayo waziwazi na kwa siri, hutafsiriwa kuwa shetani ndiye chanzo na mwenye kusababisha.

Mtu anapochaguliwa kuwa Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu, maana yake huyo ni Alpha na Omega kwa nchi yake, ndani ya kipindi ambacho anakuwa kwenye hatamu.

Hivyo, yapo maeneo mengi yenye akina Alpha na Omega. Inategemea na nguvu, umuhimu na thamani. Hata Tandale, kwa Mtogole huitwa Mahakama ya Simu, kwamba pale ndipo Alpha na Omega kwa wizi wa simu kwa mtindo wa uchomoaji.

ALPHA NA OMEGA WA COCAINE

Pablo Emilio Escobar Gaviria, kwa umaarufu kabisa mwite Pablo Escobar, huyu ndiye Alpha na Omega wa biashara ya dawa za kulevya hususan cocaine.

Tangu Desemba 2, 1993 alipofariki dunia mpaka sasa, hajatokea mwingine ambaye amefikia viwango vyake kwa utajiri, mtandao mkubwa na kiwango cha kuogopwa.

Pablo alikuwa tajiri mwenye fedha nyingi mno. Wakati wake hakukuwa na binadamu aliyekuwa anaingiza fedha nyingi kwa siku kama yeye duniani. Hata hivyo, mapato ya Pablo yanabaki kuwa makisio tu.

Sababu ni kwamba mzunguko wa kifedha wa Pablo haukuwa wa kupitia benki au taasisi halali za kifedha, hii ni kwa sababu fedha zake zote zilikuwa haramu. Hivyo, haikuwa rahisi kutambua alikuwa na utajiri mkubwa wa kiasi gani.

Pablo akitumia genge lake la Medellin (Medellin Cartel), alipenda biashara ya cocaine na biashara hiyo nayo ikampenda. Na kwa mapenzi hayo ya pande mbili, aliweza kutengeneza utajiri ambao ni simulizi za vizazi vyote.

Kutokana na jeuri ya fedha, Pablo alilifanya genge lake la Medellin kuwa Serikali ndogo ndani ya Serikali ya Colombia na nyingine duniani ikiwamo Marekani. Alikuwa na askari wake ambao walimkamata aliyemtaka kisha kumuua waliyemkusudia.

Enzi zake ilikuwa maofisa wa polisi wakiingia kwenye anga zake, kwanza aliwashawishi kwa fedha, walipokubali kupokea hongo hiyo ilikuwa salama yao lakini walipogoma kuchukua rushwa, kilichofuata ni kuuawa.

Mpaka anafariki dunia, Pablo alikuwa na rekodi ya kuua mamia ya watu, wengi wakiwa polisi aliowaona wanoko, wengine ni wafanyabiashara wenzake wa dawa za kulevya aliotofautiana nao au wafanyakazi wake aliobaini au kuwahisi wanamsaliti.

Colombia walimwita El Zar de la Cocaina (The Tsar of Cocaine), yaani Mfalme wa Cocaine. Hata hivyo alikuwa na majina mengi, kama vile Don Pablo (Sir Pablo), El Padrino (The Godfather), El Patron (The Boss), El Senor (The Lord), El Magico (The Magician) na El Pablito, yaani Little Pablo.

UNAPASWA KUMJUA PABLO

Pablo aliabudiwa na watu kwa fedha zake. Alisambaza dawa za kulevya kwa nafasi kubwa. Alifikisha shehena zake kokote duniani alipotaka. Yote hayo aliyafanikisha kwa sababu ya nomino hii; Fedha.

Alimiliki ndege 15 kubwa na helikopta sita ambazo zilifanya kazi ya kubeba shehena za cocaine kutoka kituo kimoja kwenda kingine, vilevile kumkusanyia fedha.

Kipindi Pablo akiwa Pablo kweli, alikuwa akisafirisha cocaine tani 15 kila siku kwenda Marekani. Mzigo huo makisio yake ni dola 700 milioni ambazo kwa thamani ya sasa ni dola 1.3 bilioni, Sh 2.9 trilioni kwa sarafu ya Tanzania.

Zingatia kuwa fedha hizo alitengeneza kwa kuingiza cocaine Marekani peke yake. Tambua kuwa Pablo alikuwa anasambaza dawa za kulevya akitokea Medellin, Colombia na kufika duniani kote.

Benki ilikuwa kwenye nyumba zake na katika hilo, alipata wakati mgumu mno kuzipanga fedha zake kutokana na wingi. Kila ndege yake iliposafirisha mzigo, iliporejea ilirudi na fedha.

Kutokana na hali hiyo, kila wiki, Pablo alikuwa na bajeti ya dola 1,000, sawa na Sh 2.2 milioni kwa ajili ya kununulia mipira ya kufungia fedha, yaani rubber bands.

Alipokuwa hai, hakuna binadamu aliyekuwa anamfikia kwa wingi wa fedha. Mpaka anafariki dunia, taasisi za kiusalama Colombia, Marekani na Umoja wa Mataifa, zilizohusika na upelelezi wa dawa za kulevya, zilifanya makadirio kuwa alikuwa na utajiri unaofikia dola 30 bilioni, ambazo kwa thamani ya sasa ni dola 57 bilioni.

Fedha hizo dola 57 bilioni, sawa na Sh 127.5 trilioni, bado zinamfanya Pablo kuwa mmoja wa matajiri wakubwa kabisa duniani. Kwa fedha hizohizo bila kuongeza, maana yake hivi sasa angekuwa tajiri nambari 5 duniani, nyuma ya Bill Gates, Warren Buffett, Jeff Bezos na Amancio Ortega.

Kwa utajiri huo, angekuwa anamzidi tajiri kijana wa Facebook, Mark Zuckerberg ambaye anashika nafasi ya tano ulimwenguni kwa sasa, akimiliki dola zake 56 bilioni, Sh125.2 trilioni.

Hapohapo zingatia pia kuwa fedha hizo ni makisio tu, maana inaaminika kuwa Pablo alikuwa na fedha nyingi mno ambazo alikuwa anazizika kwenye udongo, na ni yeye na watu wake wawili waliokuwa wanajua mahali zilipofukiwa.

Sababu ya kuamini kuwa utajiri wa Pablo ni zaidi ya huo unaotajwa ni kuwa inakadiriwa kuwa kwa mwaka alikuwa akitengeneza faida ya dola 21.9 bilioni, thamani ya sasa dola 42 bilioni, Sh 96 trilioni.

Kwa mantiki hiyo basi, kwa vile benki za Pablo zilikuwa ardhini alikokuwa anafukia maboksi, masanduku na ndoo zilizojaa dola, inaaminika kuwa fedha nyingi za mtu huyo mbaya hazijavumbuliwa mpaka leo.

Shirika la Ujasusi wa Kimataifa la Marekani (CIA), linaeleza kuwa kiasi cha fedha ambazo zimeshagunduliwa kuwa ziliachwa na Pablo ni kidogo mno, kwamba kiasi kikubwa ambacho kinakaribia asilimia 100 ya utajiri ulioachwa na mtu huyo mbaya, bado hakijagundulika.

Ipo nadharia kuwa wauza unga wengine waliwahi kuchimba na kujimilikisha mabilioni ya dola za Pablo, mara tu tajiri huyo alipotagazwa kuwa amekufa. Hata hivyo, msisitizo mkubwa umeendelea kuwapo ndani ya ardhi ya Colombia, hususan kwenye mji wa Medellin, kuna fedha nyingi za Pablo ambazo hazijagunduliwa.

 

UPO MFANO HUU

Ukitaka maajabu ya fedha za Pablo, kutana na kisa cha mzee mkulima maskini wa Colombia. Anaitwa Mariena Cartolos na umri wake ni miaka 66.

Cartolos alipewa ruzuku na Serikali ya Colombia dola 3,000, sawa na Sh 6.7 milioni, baada ya kuomba serikalini kuwa alihitaji kuanzisha kilimo cha michikichi na kuvuna kisha kuzalisha mafuta ya mawese.

Kilimo hicho, Cartolos alikianzisha kwenye ardhi ambayo inamilikiwa na familia yake kwa zaidi ya miaka 200 iliyopita. Alifanya hivyo ili kuunga juhudi za Serikali za kuhamasisha kilimo.

Wakati Cartolos alipokuwa anaandaa shamba lake, aliamua kuchimba shimo la kupitisha mipira ya maji kwa ajili ya umwagiliaji shambani kwake. Alipokuwa akichimba shimo kwa ajili ya njia ya mipira ya maji, Cartolos alikutana taswira ambayo hakuielewa.

Alipofikia nchi kadhaa chini, kila alipochimba, jembe lilidunda, akagundua kulikuwa na plastiki. Cartolos alipochimba zaidi akagundua plastiki lingine. Akazichimba na kuzitoa. Alipozifungua ndipo alikutana na maajabu ya Pablo.

Kiasi cha fedha, dola 600 milioni, Sh1.34 trilioni, zilikutwa ndani ya madumu sita makubwa ya ujazo wa lita 150 kila moja. Baada ya kuona fedha hizo, Cartolos alichanganyikiwa.

Kutokana na hofu kubwa, Cartolos aliamua kuzisalimisha fedha hizo kwa Serikali ya Colombia. Na Serikali ya Colombia ilipozikamata, wala hawakujiuliza sana, walijua tu hizo ni fedha za Pablo.

Itaendelea wiki ijayo…

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles