30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MWANAMUME ANAYEJITAMBUA HATISHWI NA MAFANIKIO YA MWANAMKE

Na Christian Bwaya


UPO ukweli usiosemwa wazi kuwa wanaume wengi wanawaogopa wanawake wenye mafanikio. Wanawake waliosoma, wenye mali na fedha, wenye madaraka makubwa katika jamii, wanakuwa na mtihani mkubwa kuanzisha na kudumisha uhusiano na wanaume.

 

Hali hii inachangiwa na mambo kadhaa. Kwanza, hulka ya wanaume kuwa kichwa cha familia. Ni dhahiri wanaume wengi wanapenda kujihakikishia hadhi ya juu kuliko wanawake. Kwa mfano, mwanaume wa kawaida anatamani kujihakikishia nafasi yake kama kiongozi wa familia kwa uwezo wake wa kumwongoza, kumwamrisha na kumdhibiti mwanamke.

 

Katika kuhakikisha kuwa hilo linawezekana mwanamume huyu hujitahidi awe na sifa za ziada kama vile kuwa na umri mkubwa zaidi, fedha zaidi na madaraka zaidi. Haya yote kwa pamoja yanajenga utamaduni wa kutafuta mwanamke dhaifu asiye na sifa alizonazo yeye ili kujihakikishia madaraka zaidi.

 

Lakini pili, kwa upande mwingine, baadhi ya wanawake nao wana hulka ya kupenda kupambana na mamlaka ya wanaume. Pengine kwa kuchoka kunyanyasika na kuwa chini ya udhibiti wa wanaume, inapotokea wanapata mafanikio kuwazidi waume zao, huanza kutishia heshima  na hadhi ya mwanamume.  

 

Kwa mfano, mwanamke mwenye uwezo mkubwa wa kifedha kuliko mumewe anaweza kuanza kujiona hana sababu ya kumsikiliza mume wake. Fedha zinakuwa ni fursa ya ‘kujikomboa’ dhidi ya utawala wa mwanamume jambo ambalo linaweza kuwatisha wanaume.

 

Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia kuwa  katika siku za nyuma, tofauti ya kijinsia ilikuwa dhahiri. Mila na desturi za wakati huo, kwa mfano, zilimnyima mwanamke fursa ya kujengewa uwezo sawa na mwanamume. Katika familia nyingi, mtoto wa kiume ndiye aliyepewa upendeleo kielimu na kijamii. Upendeleo huo ulimwezesha mtoto wa kiume kuwa na nafasi nzuri ya kupata mafanikio zaidi ya mwanamke. Katika mazingira hayo, haikuwa ajabu kwa mwanaume kumzidi mwanamke.

 

Mambo yamebadilika. Wanawake wa kileo wanayo fursa sawa na wanaume katika maeneo yote muhimu ya maisha. Wanawake wanakwenda shule sawa na wakati mwingine hata kuwazidi wanaume. Fursa ya kusoma imewafungulia milango wanawake kuajiriwa na kupata nafasi ambazo hapo awali zilikuwa haki ya wanaume.

 

Hapa tunapata masomo mawili makubwa. Mosi, mwanaume wa sasa hawezi kuendelea kutegemea udhaifu wa mwanamke kama kigezo cha kujihakikishia hadhi ya kuwa kichwa cha familia. Kuendekeza ukandamizaji dhidi ya wanawake kama namna ya kulinda heshima ya mwanaume ni jambo lisilowezekana.

 

Tulikofika haiwezekani tena kurudi nyuma. Mwanamume mwenye mawazo ya kumzidi mwanamke kielimu, kifedha, kimadaraka kama mbinu ya kujihakikishia heshima ya kichwa cha familia anaweza asifanikiwe.

 

Somo la pili ni haja ya kuondoa utata wa kimajukumu baina ya wanawake na wanaume. Wanaume kwa wanawake, kwa pamoja, wasipuuze nafasi zao katika familia.

Tukianza na upande wa mwanamume, kujitambua ni muhimu. Kujitambua huleta kujiamini. Mwanamume anayejiamini anaelewa fika kuwa kichwa cha familia maana yake ni uwezo wa kuelewa majukumu. Kujiamini kunaondoa haja ya kumfokea, kumpiga, kumdhalilisha, kumwamrisha na hata kumdhibiti mwanamke.

Mwanamume wa sasa anahitaji kuelewa kuwa yeye ndio tishio la kweli la hadhi yake. Asipojiamini na kuelewa nafasi yake atakuwa anahatarisha nafasi yake kama kichwa cha familia. Ndio kusema mwanamume imara, mwanamume anayejiamini, anayejitambua na kuelewa wajibu wake, hatishwi na uimara wala mafanikio ya mwanamke.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles