OFISA MTENDAJI, MWENYEKITI WAUAWA KIBITI

0
539
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga,

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MAUAJI ya viongozi wa vijiji na askari polisi yameendelea kutokea katika Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani na kuzidi kuzua hofu kwa wananchi.

Usiku wa kuamkia jana, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mangwi, Kata ya Mchukwi, Shamte Makawa na Mwenyekiti wake, Maiko Nicholaus, waliuawa kwa kupigwa risasi na baadaye nyumba zao kuchomwa moto.

Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, alikiri kutokea kwa mauaji hayo.

Alisema pia Mwenyekiti wa Kitongoji cha Londo, alijeruhiwa na kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akipatiwa matibabu.

“Ni kweli viongozi wawili wameuawa na mmoja amejeruhiwa, ni mtendaji Kijiji cha Mwangi na mwenyekiti wake, mauaji yalitokea saa 3 usiku.

“Taarifa zilichelewa kuja, tumezipata asubuhi, kwa sababu tukio lilipotokea ni maeneo ya mbali ya vijijini na tunaendelea kufanya uchunguzi,” alisema Lyanga.

Mmoja wa viongozi wa eneo hilo ambaye hakuwa tayari kutajwa jina gazetini, alisema mauaji yanayoendelea wilayani humo yamezidisha hofu kwa wananchi.

“Wananchi wana hofu, wanasema kama viongozi wanaisha shida zao watazipeleka wapi, wafanye nini ili waweze kuwa salama,” alisema kiongozi huyo.

Matukio ya mauaji katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani yamekuwa yakishika kasi kwa sasa, huku ikielezwa kwamba zaidi ya watu 40 wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

 ACT WAZALENDO

Chama cha ACT Wazalendo kimemshauri Rais Dk. John Magufuli aitishe Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa na kutoa maazimio ya kukabiliana na mauaji yanayoendelea katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji.

Kimesema kinatarajia Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama itakwenda katika wilaya hizo kuzungumza na wananchi ili kupata maarifa ya kuishauri na kuisimamia Serikali kudhibiti mambo na kuimarisha usalama.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Mohammed Babu, aliviomba vyombo vya ulinzi na usalama kushirikiana na wananchi kutokomeza mauaji hayo.

“Tunaungana na wananchi wote na wapenda amani nchini Tanzania kulaani vikali mauaji hayo.

“Tunayaona mauaji hayo kama tishio na jaribio juu ya uhuru wetu na usalama wa taifa letu, mambo ambayo yanatuunganisha wote bila kujali itikadi, dini, hali ya kiuchumi wala rangi.

“Hatuamini kwa namna yoyote kuwa wauaji hao ni watu wenye nia njema wala ajenda ambayo njia pekee ya kuifikia ni kupitia mauaji ya Watanzania wenzao. Hawa ni wahalifu na wanaostahili nguvu ya umoja wetu dhidi ya udhalimu wao,” alisema Babu.

Chama hicho pia kilipinga kamata kamata inayoendelea dhidi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) katika wilaya hizo kwa kile ilichodai kuwa hilo ni moja ya mambo yanayoondoa umoja.

“Ni muhimu vyombo vya ulinzi na usalama navyo vishiriki kujenga umoja wa wananchi katika wakati huu mgumu kwa taifa kwa kutenda haki kwa wananchi wa maeneo haya bila kuonekana vinafanya uonevu,” alisema Babu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here