23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAALIM SEIF ALIA MCHEZO MCHAFU CUF

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu mambo yanayoendelea ndani ya chama hicho. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu,(Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui, Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Shahali Mngwali(kulia) na Mjumbe wa Kamati ya Uongozi, Severina Mwijage. PICHA NA LOVENESS BERNARD.

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wananchi (CUF), kikiongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, leo kinatarajia kuiburuta mahakamani Ofisi ya Wakala wa Usajili na Udhamini (RITA), kutokana na kukiuka taratibu za sheria za wadhamini.

Pia Maalim Seif amesema wanaamini ndani ya miezi mitatu ijayo haki yao kuhusu kunyimwa ushindi katika uchaguzi wa Zanzibar itapatikana.

Aidha chama hicho kitawasilisha maombi yao Mahakama Kuu kuitaka isimamishe kesi nyingine zote walizofungua kuhusu mgogoro wao ndani ya chama hadi hapo shauri linalohusu uhalali wa uamuzi wa RITA litakapoamuliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Maalim Seif, alisema chama kimepatwa na mshtuko mkubwa baada ya kusikia RITA imeghushi na kufanya isivyo halali kwa kuwapa aliowaita ‘genge’ la Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa uhalali wa kuwa na Bodi ya Wadhamini.

Alisema RITA ni taasisi kubwa inayobeba uhai wa Watanzania kwani ndiyo inayotoa vyeti vya vifo, vizazi na wosia, hivyo kufanya tukio kama hilo ni aibu kwao.

“Hili ni la kushangaza sana, kama tunaweza kuiamini taasisi kubwa  kama hii kushirikiana na ‘genge’ la Profesa Lipumba kufanya hiki ilichokifanya leo, ni hatari sana kwa afya ya taifa,’’ alisema Maalim Seif.

Alisema kilichofanyika kwa RITA si mageni kwao kwani waliwahi kuyaeleza Aprili 9, mwaka huu, hivyo taasisi hiyo imetekeleza ilichoagizwa kufanya kwa kutoa kile alichodai usajili feki.

Maalim Seif alisema CUF ina taarifa isiyo ya shaka kwamba Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Emmy Edson, amepata shinikizo la kusajili wajumbe wa Bodi ya Udhamini kwa upande wa Profesa Ibrahim Lipumba na kuhujumu majina yaliyokuwa kihalali.

Alisema hiyo imedhihirika katika barua aliyomwandikia Kaimu Katibu Mkuu ambaye alidai cheo hicho hakipo kwenye Katiba ya CUF, hivyo wamebaini usajili wa wajumbe wa bodi wa upande wa Lipumba umezingatia barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa yenye kumb. Na. 322-362-14-23 ya Aprili 4, mwaka huu.

“Hudson amekuwa akijitetea kwa kuweka wazi kuwa mtu mahsusi wa kutoa majibu ya kwa nini yamesajiliwa hayo majina ya Bodi ya CUF ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi, lakini pamoja na kwamba utetezi huo haumwondoi kutiwa hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka, ila sheria inamtaka kujiridhisha na nyaraka zinazowasilishwa kwake na waombaji,’’ alisema Maalim Seif.

Aliendelea kufafanua kuwa Bodi ya Wadhamini ya CUF ilisajiliwa mwaka 1993 kwa kufuata taratibu  na kupatiwa hati za usajili  Na. ADG-T-1127.

Alisema CUF imeendelea kuheshimu na kutekeleza matakwa ya sheria hiyo kwa kuweka sawa kumbukumbu za bodi yake na kufanya mabadiliko kila ilipobidi.

Maalim Seif alisema kilichofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa kumshawishi Mtendaji wa RITA ni kosa la jinai na ikizingatiwa kuwa Oktoba 2016 alishakamilisha uhakiki wa utekelezaji wa masharti ya usajili  kwa vyama vya siasa nchini.

Alisema baada ya kugundua njama mbalimbali zinazofanywa upande wa Profesa Lipumba kufuta kesi zilizokuwa zimefunguliwa na ambazo zinamwelemea licha ya kutumia nguvu za dola, waliamua kufungua akaunti mpya ya benki ili kumwezesha kupata ruzuku Sh milioni 360.

“Wameamua kumwondoa  madarakani Katibu Mkuu Maalim Seif na hivyo kufanikisha njama za kuwapokonya haki yao Wazanzibari kwa maamuzi yao 2015.

“Hakuna shaka kwamba njama na hujuma ya kudhibiti CUF inafanywa na dola na kwa hali hiyo utawala wa Serikali ya awamu ya tano, haiingii akilini kama mtumishi yeyote wa umma  anaweza kuwa na ujasiri wa kufanya makosa makubwa ya kijinai wazi wazi namna hii,’’ alisema Maalim Seif.

Alisema kuwa chama kimesikitishwa na hatua za mawakili wao waliopatiwa barua mbili zilizosainiwa na aliyemwita  mfuasi wa Lipumba, Thomas Malima, akijitambulisha kuwa ni Katibu wa Bodi kuwaondoa mawakili hao.

Mawakili hao ni Juma Nassor, Daimu Halfani na Hashim Mzirai waliokuwa wakisimamia chama kisheria na kumwajiri wakili Makubi Kunju Makubi.

Pia alisema barua nyingine ikiombwa kufutwa kwa shauri namba 21 la mwaka huu linalomkabili Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi la fedha za ruzuku zilizoidhinishwa naye Sh milioni 369.

Kuhusu kupata haki yao ndani ya miezi mitatu, alifafanua kuwa anaamini mahakama na kwa uwezo wa Mungu itapatikana bila tatizo lolote.

Maalim Seif aliwataka wanachama wanaomuunga mkono kufika Mahakama Kuu leo kufungua kesi dhidi ya RITA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles