24.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 30, 2022

Contact us: [email protected]

‘Obama na Kim Jong-Un’ wanapokutana ana kwa ana

maxresdefaultKAMWE dunia haikuwahi na wala haitarajii kumuona Rais wa Marekani, Barack Obama na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un wakiwa pamoja walau kwa picha wakitabasamu kwa furaha.

Pamoja na kuwa viongozi wenye uhasama hata uwe mkubwa kiasi gani kupatana ni jambo linalowezekana, kwa wawili hao haitarajii kutokea kutokana na kiwango cha sasa cha uhasama na muda ambao Obama amebakiza kabla ya kustaafu mapema mwaka ujao.

Uhusiano baina ya mataifa hayo mawili haujawahi kuwa mzuri kwa miaka mingi licha ya majaribio ya kuondoa hali hiyo na Obama amemuwekea binafsi kiongozi huyo wa Korea vikwazo pamoja na kuorodhesha utawala na maofisa wake waandamizi katika mataifa wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu.

Hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na utawala wa Kim Jong-Un kuendelea kufanya majaribio ya makombora ya nyuklia kinyume na maazimio ya Umoja wa Mataifa (UN) na kuleta wasiwasi kwa mataifa washirika wa Marekani kama vile Korea Kusini na Japan.

Kwa hali kama hiyo, iwapo itatokea wakawa eneo moja la mkutano au tukio, kila upande utahakikisha kukutana baina yao kamwe hakutokei.

Lakini wakati kwa Obama na Kim halisi hali ikitarajia kuwa hivyo, kwa ‘mapacha wao’ yaani watu walioondokea kufanana nao, ijapokuwa hawana uhusiano wowote, mkutano baina yao hali ni tofauti.

Picha za watu hao Reggie Brown (35) mkazi wa Los Angeles, anayefanana na Obama pamoja na anayejitambulisha kwa jina moja kama Howard (37) raia wa Hong Kong zinatamba mitandao baada ya wawili hao kukutana na kutumia siku pamoja, kwa namna ambayo iliwashangaza na kuvutia wengi waliowaona.

Brown mwenye umri wa miaka 35 alianza kufahamika duniani mwaka 2011 wakati alipoonekana jukwaani katika mkutano wa uongozi wa chama cha Republican uliooneshwa moja kwa moja katika televisheni.

Howard yeye aliingia Marekani kukutana na Brown, ambapo kufanikisha safari hiyo akiwa kwao Hong Kong aliendesha shughuli za uchangishaji fedha dola 1.500 sawa na Sh milioni 3 kwa ajili ya safari hiyo.

Wawili hao wakapanga kukutana wakati wa sherehe za utoaji tuzo maarufu za Oscar mjini Los Angeles, ambako walikuwa kivutio kikubwa kwa wapita njia.

Viongozi hao bandia walijaribu kutumia nyuso zao maarufu kuingia ukumbini – lakini kabla ya jaribio la kuingia, muda mwingi waliombwa kupiga picha na watalii na wapita njia wengi.

Lakini pamoja na umaarufu wa nyuso zao, wawili hao hawakufanikiwa kuingia katika hafla hiyo.

Howard (37), alisema: “Mara tulipoingia Hollywood Boulevard tulijikuta tukiwa tumezungukwa na watu.

“Tulifuatwa njia nzima na watu walitaka kupata picha pamoja nasi.

“Kwa taswira yangu, inayojulikana kwa uhasama na Marekani, niliweza kutokwa na kauli kama ‘hamjambo Wamarekani wajinga’ na ‘kifo kwa Marekani’.

“Hakika lakini watu walifurahi sana siku hiyo.”

Reggie, anayehesabika kama mtu mwenye kufanana na kuweza kuigiza sauti na nyendo za Rais Obama kuliko wengine wote duniani alisema pia alishangazwa na mwitikio waliopokea.

Alisema: “Ilisisimua, watu wanataka kukuona na kila mtu anataka kupata picha ya kuwaonesha marafiki na familia zao.

“Nikiwa na Howard ilipendeza hakika, ni askari mzuri, askari mbaya.

“Alichokuwa akifanya ni kumaanisha kile anachopaswa kuwa na watu waliipenda staili yake. Mimi nilikuwa nikitabasamu na kupungia mkono.

“Mwanamke mmoja raia wa Brazil alikuja na kusema; ‘Obama, nakupenda sana,’’ kisha akamtazama mwenzangu Howard kwa jicho baya kusema, ‘‘unapaswa kurudi kwenu Korea’.”

Howard aliongeza “Reggie ni mtu anayefanana na kuigiza vizuri kuhusu Obama kuliko wote wakati mimi ni pekee ninayafanana na Kim Jong-un.

“Wamarekani wengi walitaka picha na Reggie lakini niliona watalii wengi wa China walitaka picha nami.

“Mwenzangu ana soko Amerika ya Kaskazini lakini mimi ni maarufu zaidi Asia,” alisema.

Barani Asia Kim Jong-Un ana mashabiki wengi akiwamo Wang Lei, kutoka Nanjing, jimbo la Jiangsu nchini China ambaye amepitia kisu ili kumfanya afanane na kiongozi huyo wa Korea.

Baada ya kufanikiwa upasuaji, Wang amekuwa akifanya maigizo mbalimbali sawa sawa na matendo ya dikteta huyo wa Korea ikiwamo kuwa sambamba na mkewe.

Ukiachana na hilo kabla ya tukio la Oscar, Howard aliweza kuingia wakati wa utoaji tuzo za Grammys na kupiga picha na mwanamuziki wa kike anayelipwa zaidi Katy Perry.

Anasema: “Nilimuonesha akitembea kunipita na hivyo nikasimama na kusema ‘Katie Perry’ kwa sauti sawa kabisa na ya Kim Jong-un.

“Nilimuuliza je unaijua?”

“Alionekana kubabaika na kuonesha mshangao– hivyo sijui iwapo alitambua kama ni mtu ninayefanana na Kiongozi wa Korea Kaskazini au la.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,436FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles