29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

JKT ilivyotekeleza jukumu la madawati

jktNa Sajini Lucas Mpullani

APRILI 12 mwaka huu, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Magereza nchini walipewa jukumu la kutengeneza madawati yenye thamani ya Sh bilioni 6 ambayo yatasambazwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Hatua hiyo ilifuatia baada ya Rais Dl. John Magufuli kutoridhishwa na kasi ya utengenezwaji wa madawati ambapo utengenezaji wake ulikabidhiwa kwa baadhi ya vyombo vya Ulinzi na Usalama kupitia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Magereza.

Fedha hizi ziligawiwa kwa Jeshi la Magereza na Kamandi ya Jeshi la Kujenga Taifa ili kutengeneza madawati 120,000 ingawa mpaka sasa taasisi hizo zimeshakabidhi madawati 61,385 ambayo yametengenezwa kwa miezi mitatu.

Uongozi wa juu kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Kamandi ya JKT, walikabidhi kazi ya kutengeneza madawati kwa Kikosi cha Mgulani na Kikosi cha Ruvu.

Jeshi la Kujenga Taifa kama moja ya kamandi ilipewa jukumu hilo kutokana na uwepo wa nguvu kazi ya vijana, ambao kwa kiasi kikubwa wameweza kufanya kazi hiyo kwa weledi wa hali ya juu kwa kushirikiana na maafisa na askari waliopo.

Wakati Kikosi cha Mgulani chini ya Luteni Kanali, Erasmus Castory Bwegoge, kikimaliza lengo lao la kutengeneza madawati zaidi ya 8,000 kikosi cha Ruvu kiliweza kutengeneza madawati 35,044.

Makamanda hawa wa vikosi cha Mgulani na Ruvu JKT wamekuwa makini kuhakikisha madawati hayo yanatengenezwa kwa ufanisi wa hali ya juu huku wakiwa bega kwa bega katika kuyachomolea, kuyaunga, kupaka rangi na kuhakikisha wameyasafirisha kwenda sehemu husika.

“Kwa kiasi kikubwa wana hali na kazi hiyo ambayo inaonekana imefika kwao kama bahati kwani kwa wale ambao walikuwa hawajui kuchomolea wameweza kujifunza kuchomelea ilihali wale waliokuwa hawawezi kupaka rangi kwa sasa wamefundishwa na kuwa watu wazuri katika kupaka rangi,” anasema Luteni Kanali Mbuge.

Mmoja wa vijana wa kujitolea, Masha Mphuru, kutoka kikosi cha Mgulani, anapongeza hatua ya Rais Magufuli kuwatupia jicho wanafunzi walioko mashuleni kwani usikivu utaongezeka na kufanya vijana kuongeza bidii.

“Kipindi nilichosoma mimi nilikaa kwenye dawati nilipofika darasa la tano na kuendelea lakini kwingine kote nilikuwa nikikaa chini kitu ambacho kilituletea usumbufu sana kwa kuandika na hata kujifunza hati vizuri,” anasema Mphuru.

Kijana mwingine Charles Chidumule kutoka kikosi cha Ruvu, anasema; “Leo naweza kuchomelea na hata kupaka rangi tena kwa ustadi wa hali ya juu, nimejifunza uzalendo, ujasiriamali, kupenda kazi na jinsi ya kuishi na wezangu pasipo kutofautisha dini zetu.

Naye Mkuu wa Usalama na Utambuzi wa Kikosi cha Ruvu, Benedictor Kivunja, na Joseph Magomba wa Mgulani, wanasema katika kuwasimamia vijana wa kujitolea wameweza kutambua kuwa wengi wanapenda kufanya kazi.

“Tumekuwa nao tangu awali, wamekuwa wakijituma sambamba na kujiongoza pasipo kuhitaji kusimamiwa,” anasema Kivunja.

Naye Mteule daraja la pili Joseph Magomba kutoka Mgulani aliwataka vijana hao kutokuvimba vichwa na kujisahau pindi mtakapo pata ajira.

Mkuu wa Kikosi cha Ruvu, Luteni Kanali Charles Mbuge, na Msaidizi wake ambaye kwa sasa ni Msahauri wa Mgambo Wilaya ya Bagamoyo, Meja Idd Musira, wanawataka maafisa na askari kufanya kazi kwa ushirikiano, weledi na kujituma ili kukamilisha kazi ya kutengeneza madawati na Rais aweze kuendelea kuwa na imani na vyombo vya ulinzi.

Hadi sasa Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Magereza wamekabidhi madawati 61,385 na kugawiwa kwa mikoa 15 ambayo ni Dar es Salaam iliyopata madawati 5,370, Pwani 4,833, Morogoro 5,970, Lindi 4,295, Mtwara 5,370 na Ruvuma 4,832.

Mikoa mingine ni Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi, Tanga na Visiwa vya Unguja, Pemba ambayo imepata madawati 6,444. Mikoa mingine inasubiri awamu ya pili ya mradi wa madawati 60,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles