28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

NJAA NA UBINAFSI NDIO CHANZO CHA LIGI KUU KUPOROMOKA

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

LIGI Kuu Tanzania Bara inaelekea ukikongoni, huku kukiwa na matukio lukuki ambayo huenda yakawa ndio chanzo cha kuporomoka kwa ubora wa ligi hiyo.

Matukio hayo ni pamoja na  dosari za waamuzi ndani ya uwanja, kashfa ya upangaji matokeo na kashifa za Kamati za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupendelea upande mmoja wanapotoa uamuzi wao.

Kwa kipindi kirefu dosari hizo zinatajwa kuwa chanzo cha Ligi Kuu kuwa na timu mbili kati ya Simba na Yanga, huku nyingine zikilalamika kuonewa.

Waamuzi wamekuwa wakilalamikiwa sana kuhusu uamuzi wao ndani ya uwanja, kutokana na kugubikwa na utata mwingi, hasa katika michezo mikubwa ya Simba na Yanga.

Vitendo vinavyofanywa na waamuzi ni kama tunakwenda hatua mbili mbele lakini tano nyuma, kwa kushindwa kutoa haki ndani ya uwanja.

Klabu hizo mbili zimekuwa zikitajwa mara kadhaa katika kudumaza soka nchini wakitumia ushawishi wao wa mtaji mkubwa wa mashabiki walionao.

Pia kuwapo kwa viongozi wanaofanya uamuzi wao kwa mahaba ndani ya TFF kitendo hicho kimetajwa kuwa ni miongoni mwa mambo yanayoirudisha nyuma tasnia ya mchezo wa soka nchini.

Viongozi hao kupitia kamati wanazoziongoza wamekuwa wakilalamikiwa kufanya vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikiongezeka msimu hadi msimu.

Kingine ni matumizi ya fedha na kuwahadaa wachezaji kufanya vitendo ambavyo si vya kimichezo ndani ya uwanja, pia kimechangia kuondoa ladha ya mchezo huo.

Kwa ujumla njaa na tamaa za fedha vimekuwa chanzo cha matatizo na soka letu kuporomoka kwa kupanga matokeo ya mchezo hata kabla ya kuchezwa.

Tumeshuhudia mara kadhaa wachezaji  kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu na uongozi wa klabu zao kwa madai ya kupokea fedha kutoka kwa timu pinzani na kusababisha kupoteza mchezo wao.

Aidha, janga la klabu kukosa wadhamini pia ni tatizo lingine linalotajwa kuondoa ushindani ndani ya Ligi Kuu, huku nyingine zikikiri kushindwa kujiendesha kutokana na ukata wa fedha.

Kwa haraka haraka yapo mambo mengi ambayo yanatakiwa kushughulikiwa ili msimu ujao uoneshe mabadaliko kwa kurejesha imani kwa wapenzi wa soka nchini.

Ukiachana na hilo, lilikuwapo suala la wapi panastahili kufanyika fainali za Kombe la FA, linaloandaliwa na TFF, kati ya Mbao FC dhidi ya Simba, kabla ya kuamuliwa fainali hiyo kuchezwa Mei 28 mwaka huu, Jamhuri, mjini Dodoma.

Jibu la kwanza lilitolewa na Rais wa Shirikisho hilo, Jamal Malinzi, kuwa itachezeshwa droo kabla ya kufanya uamuzi.

Hivi kwa wanaofuatilia masuala ya soka ulimwenguni, kuna ambaye hajui fainali za kombe la dunia zinafanyika wapi, fainali za Uefa zinafanyika wapi au lile kombe la FA pale England fainali zake zitafanyika wapi? iweje fainali za FA za Tanzania hazikujulikana mapema kabla  ya  kuchezwa mechi za nusu fainali.

Kwa hali hii, TFF wanahitaji kubadilika  kifikra na maarifa namna ambavyo tutaendesha Ligi kwa haki bila ya dalili za ubabaishaji kama ambavyo inatokea sasa.

 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles