26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

N’GOLO KANTE, MTU NA BAHATI YAKE

NA BADI MCHOMOLO

MUNGU akikuwashia taa ya kijani na kumaanisha kuwa wewe ni mtu wa mafanikio, basi wataalamu wanasema hata kama utakuwa unauza mbilimbi basi utatajirika, unaweza kusikia mbilimbi ni dawa ya ugonjwa mkubwa duniani.

Katika soka mafanikio hayawezi kuja kirahisi kama baadhi ya watu wanavyodhani, ila dawa kubwa ni kujituma kwa kiasi kikubwa na nidhamu ya hali ya juu.

Yuko wapi Ronaldinho Gaucho ambaye alitikisa dunia kwa muda mchache, lakini akashindwa kulinda heshima yake na kipaji alichopewa peke yake na Mungu, kuna mambo aliyachanganya na soka hatimaye akaondoka mapema kwenye soka huku ulimwengu wa soka ukiwa bado unamhitaji.

Lionel Messi na Cristiano Ronaldo bado wanaendelea kufanya makubwa katika soka kutokana na kujituma kwao na nidhamu waliyonayo bila kujali bahati walizonazo.

Kiungo wa klabu ya Chelsea, N'Golo Kante, hakuwa na jina kubwa msimu miwili iliyopita, lakini aliweza kujitambulisha vizuri kwenye michuano ya Ligi Kuu nchini England msimu wa 2014/2015 akiwa na klabu ya Leicester City, huku akitokea kwenye kikosi cha Ligi daraja la pili cha Caen cha nchini Ufaransa.

Mchezaji huyo hana historia kubwa sana katika mikiki mikiki ya soka. Alianza kucheza soka katika kikosi cha Boulogne, ambacho kilikuwa kinashiriki Ligi daraja la kwanza. Katika kikosi hicho alijiunga tangu 2012 hadi 2013, huku akiwa amecheza michezo 38 na kufunga mabao 3 kabla ya kujiunga na Caen ambapo alicheza jumla ya michezo 75 na kufunga mabao 4.

Wakati anakipiga katika kikosi cha Caen, Mkurugenzi wa sasa wa klabu wa Everton, Steve Walsh, awali alifanya kazi katika kikosi cha Chelsea na Leicester City, huku akiwa anafanya kazi kubwa ya kuwatafuta wachezaji ambao walizisaidia timu hizo kutwaa mataji.

Akiwa Leicester City mwaka 2015, Mkurugenzi huyo alimuona Kante akiwa anafanya yake katika kikosi cha Caen, kisha kufanya mazungumzo na klabu ya Leicester City na kufanikiwa kuinasa saini yake. Hakuna ambaye alikuwa anaujua uwezo mkubwa wa mchezaji huyo, lakini michezo michache ndani ya Ligi Kuu msimu huo akiwa na kikosi cha Leicester dunia ilianza kumtambua.

Alifanya makubwa sana katika safu ya kiungo, huku akiweza kuunganisha mawasiliano mazuri kati ya kiungo na washambuliaji ambao ni Riyad Mahrez na Jamie Vardy, kisha kuifanya klabu hiyo ionekane bora katika ushirikiano.

Mungu aliwaangazia taa ya kijani timu ya Leicester City na kufanikiwa kutwaa ubingwa msimu uliopita, huku Kante akifanikiwa kutajwa mchezaji bora wa Ligi Kuu nchini England msimu huo. Wakati anafanya makubwa katika safu ya kiungo ndani ya Leicester City, kocha wa Chelsea, Antonio Cante alishindwa kuzuia hisia zake na kuitaka saini ya mchezaji huyo.

Kante aliweza kuwaaga wachezaji wenzake ndani ya Leicester City baada ya kutwaa ubingwa, huku akiwaambia kuwa anakwenda kujaribu maisha ya soka kwenye klabu nyingine. Kuondoka kwake kulileta pengo kubwa ndani ya Leicester kama mabingwa watetezi.

Wengi waliamini kuwa ujio wa mchezaji huyo ndani ya Chelsea unaweza kumfanya asionekane sana kama ilivyo katika kikosi cha Leicester City kwa kuwa Chelsea ina viungo wenye uwezo wa hali ya juu kama vile Cesc Fabregas na Eden Hazard, lakini kumbe ujio wake ulizidi kuleta ushindani kwa wachezaji hao, lakini Kante bado alikuwa na nafasi yake kutokana na kujituma kwake na nidhamu aliyonayo.

Mashabiki wa Chelsea waliweza kumsahau kiungo wao, Ramires, ambaye alitimkia nchini China baada ya kumalizika kwa msimu, huku nafasi hiyo ikizibwa vizuri na Kante, kumbe Mungu alimwashia taa ya mafanikio katika soka, huku ujio wake ndani ya Chelsea haukuwa wa bure.

Kutokana na kupambana kwake, ameiwezesha klabu hiyo kutangaza ubingwa msimu huu, huku ikiwa imebaki michezo mitatu kumalizika kwa Ligi hiyo, ina maana mchezaji huyo analitwaa taji hilo mara mbili kwa misimu miwili mfululizo, huku akiwa na timu mbili tofauti.

Hata hivyo, mchezaji huyo msimu huu amechukua tuzo nyingine ya mchezaji bora nchini England, aliyechaguliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za soka nchini humo, kutokana na mchango wake kuwa mkubwa ndani ya kikosi hicho.

Baadhi ya mashabiki na wadau mbalimbali walidai kuwa mchezaji huyo anaifanya Chelsea ionekane kuwa na wachezaji 12 ndani kutokana na uwezo wake kuonekana kuwa wa zaidi ya mchezaji mmoja. Wapi atalitafuta taji hilo kwa mara ya tatu mara baada ya kumalizika kwa msimu huu?

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles